Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-02 16:41:35    
Mji wa magari uliojengwa porini

cri

    Wuhan ni mji mkubwa kabisa katika sehemu ya kati ya China. Karibu na mji huo kuna mji wa magari. Magari mengi yanayojulikana sana nchini kama Fukang, Elysee, Xsara na Picasso yanatengenezwa katika mji huo. Mji huo ni mahali kilipo Kiwanda cha Magari cha Shenlong kilichoanzishwa kwa ubia kati ya Kiwanda cha Magari ya Dongfeng ya China na Viwanda vya Magari ya PSA, Citroen na Peugeot.

    Mji wa magari ya Shenlong uko karibu na mji wa Wuhan, mtu akiingia mji wa magari, ataona barabara nyingi na karakana kubwa zilizojengwa kwenye kando mbili za barabara. Kiongozi mmoja wa kampuni hiyo ya magari bibi Li Xiaoqing alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kabla ya miaka zaidi ya miaka kumi iliyopita, sehemu hiyo ilikuwa ni pori. Alipoeleza hali ya zamani kabla ya kujengwa kwa kiwanda cha magari, bibi Li Xiaoqing alisema,

    "Tulipofika hapa, kulikuwa na ardhi kidogo yenye udongo wa rangi ya manjano. Ingawa mazingira ya wakati ule yalikuwa magumu, lakini walikuwa na matarajio makubwa na maendeleo ya uzalishaji wa magari. Hivyo walichapa kazi kwa bidii na kutojali uchovu. Gari dogo la kwanza la Fukang lilitengenezwa mwezi Septemba mwaka 1995, na siku hiyo watu wote walikuwa na furaha kubwa."

    Hali ya zamani ya pori na umwitu imetoweka kabisa, badala yake ni hali ya pilikapilika za uzalishaji mali. Katika karakana ya kumalizia, mwandishi wetu wa habari aliona magari yaliyoko katika mstari wa uzalishaji, yakisogea mbele polepole huku wafanyakazi wakifunga vipuri kwa haraka. Magari madogo ya kampuni ya Shenlong yanakamilishwa katika karakana hiyo na kupelekwa nje kutoka huko. Bibi Xing Yan wa idara ya uhusiano ya kampuni ya Shenlong alimwambia mwandishi wetu wa habari,

    "Katika mwanzo wa mstari wa uzalishaji, tunaona misingi ya magari tu, kunakuwa hakuna kitu chochote ndani yake, lakini baada ya kupita sehemu mbalimbali za kazi, magari mapya yanayopendeza yanatoka moja baada ya lingine."

    Magari ya aina tofauti yanatengenezwa katika mji wa magari na kupelekwa katika sehemu mbalimbali nchini China. Habari zinasema kuwa katika mwaka 1998, Kampuni ya Magari ya Shenlong ilikuwa inatengeneza magari laki 1 na elfu 50 pamoja na injini za magari laki 2. Licha ya hayo kampuni hiyo ilijenga kiwanda cha injini za magari chenye eneo la mita za mraba laki 5 katika mji wa Xiangfan, sehemu ya kaskazini magharibi ya mji wa Wuhan. Hivi sasa Kampuni ya Magari ya Shenlong imekuwa na mtaji wa Yuan za Renminbi bilioni 7 na kuwa moja ya kampuni kubwa tatu nchini China.

    Maendeleo makubwa na ya kasi ya Kampuni ya Magari ya Shenlong yamesifiwa sana na mwekezaji wa upande wa Ufaransa. Meneja wa upande wa Ufaransa alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

    "Ninaona ushirikiano kati ya China na Ufaransa ni wa kufurahisha, na tena ni wenye ufanisi mkubwa. Nasema hivyo kwa sababu ushirikiano huo umetumia hali bora za pande mbili. Upande wa Ufaransa unatoa teknolojia ya kisasa, na China inafahamu zaidi namna ya kutengeneza magari ya hapa nchini na kuelekeza uzalishaji wa magari kwa kuendana na mwelekeo wa utamaduni wa China. Hivyo hali bora za pande mbili zimeleta ufanisi mkubwa zaidi. Mimi nina imani kubwa juu ya maendeleo ya siku za usoni."

    Katika miaka ya karibuni, pamoja na maendeleo ya uchumi wa China na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya watu wa China, hali nzuri imetokea katika soko la magari madogo nchini China. Mwaka 2003 peke yake, magari madogo milioni 4 na laki 4 yaliuzwa nchini China, na kati ya hayo magari madogo yalikuwa karibu milioni 2. Katika miaka ya karibuni, kiwango cha mauzo ya magari nchini China kiliinuka mwaka hadi mwaka. Habari kutoka kwenye kituo cha takwimu cha taifa nchini zinasema kuwa katika mwaka 2004, mahitaji ya magari nchini China yatachukua nafasi ya tatu duniani na kuizidi Ujerumani.

    Hivi sasa licha ya kuzalisha magari madogo ya Fukang, Kampuni ya Shenlong inazalisha magari madogo ya aina nyingine za ELYSEE, XSARA na PICASSO, ambayo yanapendwa sana na wateja. Mwaka 2004, kampuni hiyo itazalisha PEUGEOT 307, ambayo inapendwa zaidi na wateja. Wafanyakazi wa kampuni hiyo wametiwa moyo sana baada ya kuona kuwa magari yanayozalishwa na kampuni ya Shenlong yanapendwa sana na wateja, kwa upande mwingine kuimarika kwa nafasi zao katika masoko ya magari kumewaletea faida kubwa katika karakana ya kumalizia. Mfanyakazi mmoja Bw. Feng Jun alisema kuwa hali motomoto ya kampuni yao inafanya wafanyakazi wachape kazi kwa bidii kubwa, hivi sasa ameridhika na pato lake, na yeye mwenyewe amenuia kununua gari moja la kiwanda chao.

    Alisema, "Kila siku ninafanya kazi kwa bidii. Kiwango cha mshahara wa wafanyakazi wa kiwanda chetu ni cha juu katika mji wa Wuhan. Wafanyakazi wengi wa kiwanda chetu wanataka kununua magari yanayozalishwa na kiwanda chetu. Mimi pia ninataka kununua moja."

    Hivi sasa, Kampuni ya Magari ya Shenlong inakabiliwa na nafasi ya maendeleo na changamoto kwa wakati mmoja. Kampuni hiyo imeweka lengo la kuzalisha magari madogo yanayopendwa zaidi na watu kuliko magari madogo ya aina nyingine, na imetoa wito wa kujenga kampuni yao kuwa kampuni ya magari ya kiwango cha juu na yenye nguvu ya ushindani duniani.

    Mwanzoni mwa mwaka 1994, ujenzi wa mradi wa kipindi cha pili wenye eneo la hekta 6.6 ulizinduliwa katika mji wa Wuhan. Kutokana na mpango uliowekwa, ujenzi wa mradi huo utakamilika mwaka 2006. Mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo ya magari Bibi Li Xiaoqing alisema kuwa, wakati huo Kampuni ya Magari ya Shenlong itakuwa na uwezo wa kuzalisha magari laki 3 na injini laki 4, na itatoa magari mengi ya aina mpya na kutoa huduma nzuri zaidi kwa wateja wa China.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-02