Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-02 19:39:49    
Makala ya wasikilizaji 1102

cri
    Msikilizaji wetu mwingine Ras Franz Manko Ngogo wa Klabu ya wasikilizaji wa CRI Kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua pepe yenye majibu ya maswali ya makala za chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya. Aidha ametoa maoni yake kuhusu China na miaka 55 ya ujuzi wake wa maendeleo katika nyanja za uchumi, diplomasia, elimu na mikoa ya makabila madogomadogo inayojiendesha na maendeleo yake kwa ujumla.

    Anasema kwa muda wa miaka 55 tu kwa China kufikia kiwango cha maendeleo iliyonayo sasa, ni hatua kubwa ikilinganishwa na nchi zilizofikia kiwango hicho lakini kwa miaka zaidi ya mia mbili na huku wakitumia mabavu kufikia lengo hilo.Anasema yeye binafsi anaweza kutoa ushahidi wa miaka 30 iliyopita ya China mpya kujiendeleza. Ilikuwa mwaka 1971, pale aliposikia wachina wakivuma sana nchini mwake Tanzania, ambapo walishirikiana na kuwasaidia Watanzania katika nyanja kama vile za afya na ujenzi. Hadi sasa kumbukumbu hiyo bado ipo, kwani watoto wengi walioitwa China sasa ni watu wazima wenye familia zao.

    Anasema kwa maana hiyo na mfano huo, yeye ana imani kuwa China ni kweli ina maendeleo na itazidi kuendelea mbele siku hadi siku kwa sababu ya mfumo wao mzuri wa utawala, ushirikiano na moyo wao wa kufanya kazi kwa bidii bila kutegeana. Hali hiyo ndiyo imeufanya uchumi wa China ukue kwa kasi ya asilimia 9 hadi kufikia mwaka jana 2003. Pia China kama inavyojulikana Jamhuri ya watu wa China, ina uhuru mkubwa na hata viongozi wake ni waadilifu. Hayo ni baadhi ya mambo yaliyochangia serikali ya China kuwawezesha wananchi wake zaidi ya milioni mia mbili kuondokana na umaskini.

    Anasema China kwa kuwajali wananchi wake wa maeneo yote bila ubaguzi, kumeonesha nia yake ya kueneza elimu kote nchini na hiyo kupitisha sheria ya elimu ya lazima ya miaka 9 kwa kila mwananchi. Hilo lilikuwa wazo la busara kutoka kwa viongozi wake wenye mtizamo wa maendeleo. Anasema wakati huohuo wazo likawajia na kutambua haswa maeneo yanayofaa kupewa kipaumbele, hapo ndipo vijiji vikapewa kipaumbele. Basi fedha zaidi za elimu zikatengwa kwa ajili ya elimu vijijini ambako watu wana uwezo wa chini.

    Bwana Ngogo anasema demokrasia ni moja ya jambo linalopewa nafasi kubwa nchini China. Anatoa mfano suala la serikali kwa kuwapa uhuru wa kujiendesha watu wa makabila madogo madogo 55 ya China, kitu ambacho kinastahili kuigwa. Hilo tu halitoshi kwani mwenye heshima kwao basi hata nje huheshimiwa na kuaminika. China ina marafiki wengi kote duniani, kwa kigezo hicho China imejipatia uhusiano wa kibalozi na nchi 165 kote duniani.

    Anaendelea kusema kuwa China imejiwekea malengo muhimu, na mkakati wa kujijengea heshima ndani na nje ya nchi. Pia inaimarisha sera yake inayohusu ujirani mwema, ambayo inapinga umwamba na msimamo wa kimabavu, na kutetea aina mbalimbali za ustaarabu na mifumo ya maisha. Na kwa upande wa usalama, inapinga ugaidi na kutetea mapambano dhidi ya ugaidi. Kwa hilo pia China inaamini kuwa mapambano ya kijeshi hayawezi kuleta maelewano ya kudumu.

    China ikiwa ni mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, inalinda na kutetea heshima ya Umoja wa Mataifa, inaunga mkono mageuzi na upanuzi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Ama kwa upande wa bara la Afrika, China ina mawasiliano ya kutosha na bara la Afrika kwa kushirikiana katika masuala ya maendeleo, na kufikia hatua ya kuunda baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika mnamo mwaka 2000.

    Bwana Ngogo anaeleza matumaini yake kuwa akiwa kama mkulima mdogo mwenye elimu ya chini, ni mtu anayependa maendeleo, mwenye mtizamo wa mbali na hamu ya kujua, kuelimika na kisha kujulisha na kuwaelimisha wengine. Amevutiwa na mfumo halisi wa maisha, uongozi, ushirikiano, juhudi, maendeleo na msimamo wa watu wa China.

    Anasema China ikiwa ni nchi inayoongoza nchi nyingine zinazoendelea, imempa changamoto ya kuizuru na kupata japo mwanya wa kuona walau chembe ya haya yote iliyojifanyia yenyewe. Anasema kama akifika China, bila shaka atazingatia kupata mwanga wa jinsi ya kuwa balozi mzuri wa wananchi wa nchi yake Tanzania.

Idhaa ya Kiswahili 12-11-2004