Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-02 19:48:14    
makala maalum

cri
    Msikilizaji wetu Nsorani George Mwita wa Security Group LTD P.O.BOX 18670 Nairobi- Kenya ametuletea barua, akianza kwa salamu. Anasema yeye huko Nairobi anaendelea vizuri. Anasema kuwa lengo hasa la yeye kuandika barua hii ni kutoa shukrani kutokana na barua tuliyomwandikia siku za karibuni.

    Anasema yeye ni M-Kurya anayetoka wilaya ya Kurya, mkoa wa Nyanza nchini Kenya. Kwa vijana wa kabila lake, wanapofikisha umri wa miaka 15 hupaswa kwenda jando. Baada ya hapo inampasa kwenda msituni akiwa na kibuyu kimoja cha maziwa, akiwa huko anatakiwa amtafute Simba amuue halafu atoe ulimi wake. Baada ya hapo anaweza kurudi nyumbani kwa wazee wa kikurya wanaoitwa abagaka binchama, yaani wazee wa mila, akiwa na ulimi wa Simba. Hao wazee huchukua kibuyu kimoja cha maziwa na kingine cha damu ya ng'ombe na kuvipeleka mlimani katika mlima mmoja vikiwa havina kitu.

    Baada ya huo mwezi mmoja hivyo vibuyu hivyo hujazwa maziwa na damu, na sio binadamu anayejaza maziwa na damu ya ng'ombe kwenye hivyo vibuyu bali ni mizimu. Hayo yakikamilika vijana karibu mia tano hufanyiwa tohara wakati wa saa tisa usiku. Na baada ya muda kupita, kijana huambiwa atafute mchumba aoe. Kabla ya kuoa anatakiwa awe na mchumba kwa mwezi mmoja, na baada ya hapo baba yake anaweza kutoa ng'ombe 30 wa kupelekwa kwa msichana kama mahari, na kusibiri kufanya harusi.

    Baada ya harusi na taratibu zote za kuoa, baada ya muda mfupi kijana huhama kutoka kwa baba yake, na kwenda kujenga nyumba yake na kuanza maisha yake na kujitegemea. Hapo huanza kufuga ng'ombe, mbuzi, mbwa, kondoo, kuku, na wanyama wengineo. Baba anapozeeka hutoa wosia, akitaka ng'ombe fulani achinjwe wakati akifa, ili ngozi yake itumike wakati anapozikwa.

    Anamaliza kwa kusema hayo ni maelezo kwa ufupi ya mila za watu wa kabila la Kurya kutoka utoto, ujana, uchumba, harusi, maisha ya ndoa na kifo na mazishi. Anasema kama akiweza ataweza kutuletea picha zinazoonesha hatua hizo kwa watu wa kabila lake.

    Msikilizaji wetu mwingine Ras Franz Manko Ngogo wa Klabu ya wasikilizaji wa CRI Kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua pepe yenye majibu ya maswali ya makala za chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya. Aidha ametoa maoni yake kuhusu China na miaka 55 ya ujuzi wake wa maendeleo katika nyanja za uchumi, diplomasia, elimu na mikoa ya makabila madogomadogo inayojiendesha na maendeleo yake kwa ujumla.

    Anasema kwa muda wa miaka 55 tu kwa China kufikia kiwango cha maendeleo iliyonayo sasa, ni hatua kubwa ikilinganishwa na nchi zilizofikia kiwango hicho lakini kwa miaka zaidi ya mia mbili na huku wakitumia mabavu kufikia lengo hilo.Anasema yeye binafsi anaweza kutoa ushahidi wa miaka 30 iliyopita ya China mpya kujiendeleza. Ilikuwa mwaka 1971, pale aliposikia wachina wakivuma sana nchini mwake Tanzania, ambapo walishirikiana na kuwasaidia Watanzania katika nyanja kama vile za afya na ujenzi. Hadi sasa kumbukumbu hiyo bado ipo, kwani watoto wengi walioitwa China sasa ni watu wazima wenye familia zao.

    Pia anaishukuru Radio China kimataifa kwa kuwa dirisha lililowazi kuonesha hasa jinsi China ilivyo, na jinsi wachina wanavyozikumbuka nchi nyingine zinazoendelea kama za Afrika, ikiwemo Tanzania. Mwisho kabisa Bwana Ngogo ameandika shairi lisemalo: Sera za China zidumu:-

    Ras Manko nina hamu, pokea zangu salamu

    China nimeifahamu, maisha yake matatu

    Imefika yangu zamu, nifanyiwapo karamu

    Wachina kwa majukumu, sera zao zinadumu

    Ni marafiki wa damu, tunao kila awamu

    Watufunza kujikimu, kwa kazi ni muhimu

    Wao ni wataalamu, malengo yetu yatimu

    Wachina kwa majukumu, sera zao zinadumu

    Beti nne sio adimu, mwisho umenilazimu

    Nitawapaka marhamu, na kwa akili timamu

    China kwa ukarimu, uzidi shika hatamu

    Wachina kwa majukumu, sera zao zinadumu.

Idhaa ya Kiswahili 02-11-2004