Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-03 21:16:38    
Kujifunza lugha za kigeni utotoni ni bora zaidi

cri

    Utafiti uliofanywa hivi karibuni na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha London, Uingereza umegundua kuwa kufahamu lugha za aina mbili au zaidi kunaweza kubadilisha muundo wa ubongo wa binadamu. Utafiti huo umethibitisha kisayansi ufahamu wa watu wengi kuwa watoto wana uwezo mkubwa zaidi kuliko watu wazima katika kujifunza lugha, na kuwa binadamu akijifunza lugha ya kigeni akiwa mdogo, ataweza kufahamu na kuikumbuka vizuri zaidi lugha hiyo.

    Toleo jipya la jarida la "Nature" nchini Uingereza linasema kuwa mtaalamu wa mishipa ya fahamu wa Chuo Kikuu cha London Bw. Andre Maicanri na wenzake wamegundua kuwa chembe za rangi ya kijivu zilizoko kwenye neva inayofanya kazi ya kuongea ndani ya ubongo wa watu wanaojua lugha za aina mbili ni nyingi zaidi kuliko zile za watu wanaojua lugha ya aina moja tu, tena watu hao wakijifunza lugha za kigeni mapema zaidi, chembe za rangi ya kijivu ndani ya ubongo zinakuwa nyingi. Kiasi cha chembe za rangi ya kijivu kinahusiana na kiwango cha ufahamu wao kuhusu lugha za kigeni. Mtu mmoja akijifunza lugha ya aina ya pili baada ya kuwa na umri wa miaka 35, mabadiliko ya kimsingi yatatokea pia katika ubongo wake, isipokuwa mabadiliko hayo ni madogo sana ikilinganishwa na mtu aliyejifunza lugha ya pili akiwa bado mtoto.

    Katika utafiti wao, Bw. Macanri na wenzake walichukua watu zaidi ya 80 wa rika ya namna moja, wanaoongea lugha ya Kiingereza toka utotoni mwao na wenye kiwango sawa cha elimu. Watu 25 kati ya watu hao wanaongea Kiingereza tu, wengine 25 walijifunza lugha ya kigeni kabla ya kuwa na umri wa miaka 5 na watu wengine 33, walijifunza lugha ya kigeni wakiwa wakubwa kidogo. Waligundua kwa kulinganishwa na watu wanaoongea lugha ya aina moja na watu waliojifunza lugha ya kigeni wakiwa na umri toka miaka 10 hadi 15, chembe za rangi ya kijivu zilizoko katika ubongo wa upande wa kushoto kwenye ngozi ya mbele kabisa za wale wanaojua lugha za aina mbili ni nyingi zaidi. Bw. Macanri alisema, "kwa kuangalia kiasi cha chembe za rangi ya kijivu tu, ninaweza kujua ufahamu wao kuhusu lugha ya kigeni."

    Hivi sasa, wanasayansi bado hawajafahamu vizuri sababu ya kuongezeka kwa chembe za rangi ya kijivu zilizoko katika ubongo wa watu hao, pengine ni kutokana na kuongezeka kwa ukubwa chembe moja moja za neva, au kuongezeka kwa jumla ya idadi ya chembe za neva au kuongezeka kwa uhusiano kati ya chembe na chembe. Katika hatua ijayo, Bw. Maicanri na wenzake watafanya utafiti ili kujua kama kuongezeka kwa chembe za rangi ya kijivu kunaendana na idadi ya lugha za kigeni anazojua binadamu au la.