Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-04 18:21:07    
Mtandao wa inernet waboresha maisha ya wachina

cri

    Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na kituo cha upashanaji habari cha mtandao wa internet cha China imedhihirisha kuwa, ilipofika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, kompyuta zilizounganishwa na mtandao wa internet nchini China zilifikia milioni 87, na kuwa ya pili duniani kwa idadi ya watu wanaotumia mtandao wa internet baada ya Marekani. Mtandao wa Internet unapotoa mchango wake katika maendeleo ya uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni nchini China, na pia umeingia katika maisha ya wachina, na kubadilisha na kuboresha maisha ya wachina. 

    Bwana Li Xiaojun anaishi katika mji wa Fuzhou, mkoani Fujian, kusini mashariki mwa China. Siku kadhaa zilizopita, alikuja Beijing kwa matembezi. Kwa kuwa hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuja Beijing, hivyo alitafuta habari husika na kutafuta nafasi za hoteli kwenye mtandao wa internet. Alisema :

    "Beijing kuna idadi kubwa ya wageni, hivyo si rahisi kutafuta hoteli mara moja, lakini ni rahisi sana kupata nafasi za hoteli kwenye mtandao wa internet, inanisaidia kuokoa wakati mwingi. Kuna tofauti kubwa ya hali ya hewa kati ya Beijing na nyumbani kwetu, hivyo kabla kufunga safari, nilifuatilia hali ya hewa ya Beijing ili kuhakikisha nahitaji kwenda na nguo gani."

    Licha ya kutafuta habari, mtandao wa internet pia umebadilisha hali ya mawasiliano ya wachina. Zamani wachina huwasiliana kwa kupiga simu na kuandikiana barua. Tangu kuanza kutumika kwa mtandao wa internet, watu wengi zaidi hutuma barua pepe au kuwasiliana papo hapo kwenye mtandao wa internet kwa njia ya QQ na MSN. Msichana ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing Li Erdong alisema kuwa, yeye kila wiki atatumia mtandao wa internet. Licha ya kutafuata habari zinazohusika, lengo lake kubwa ni kuwasiliana na wenzake. Alisema:  

    "Nawasiliana na marafiki zangu walioko Canada na Australia kwenye mtandao wa internet, kila wiki tunawasiliana mara mbili au tatu kupitia barua pepe (e-mail)."

    Mtandao wa internet umefupisha umbali kati ya msichana Li Erdong na rafiki zake walioko nchi za nje.

    Kununua vitu kwenye mtandao wa internet ni mabadiliko mengine makubwa yaliyoletwa na mtandao wa internet kwa wachina, hasa kwa wale wasiokuwa na muda wa kwenda dukani. China kuna tovuti kadhaa nzuri zinazouza vitu kama vile "dandan", "taobao", "eachnet", na "alibaba". Watu wanaweza kununua vitu wanavyohitaji nyumbani kwa urahisi sana. Karibu bidhaa zote zinaweza kupatikana kwenye mtandao, kama vile maua, vitabu, video, kompyuta, vyombo vya michezo, vitu vya watoto wachaga na wanyama wanaowapenda na kadhalika. Mteja pia anaweza kupata bidhaa nafuu na huduma bora kupitia mtandao wa internet.

    Licha ya kurahisisha maisha ya wachina, mtandao wa internet pia umeboresha maisha yao. Zamani wachina ilikuwa ni lazima waende kwenye majumba ya sinema au kwenye majumba ya maonesho kutazama filamu au kusikiliza opera. Lakini sasa wanaweza kupata burudani hizo kwa kupitia mtandao wa internet. Isitoshe, vijana wanapenda kuchukua software wa michezo kutoka kwa mtandao wa internet, au kucheza sataranchi (chess) na watu wengine kwenye mtandao. Xu Chi anayeishi katika mji wa Shenyang, kaskazini mashariki mwa China naye anapenda sana kutumia mtandao wa Internet, alisema:

    "Njia za kawaida za kujiburudisha zina kikomo cha wakati na nafasi, lakini mtandao wa internet hauna tatizo hilo. Watu wengi kutoka sehemu mbalimbali wanaweza kucheza mchezo wa aina moja kwa wakati mmoja."

    Matumizi ya mtandao wa internet ya watu wengi pia yamehimiza maendeleo ya biashara ya elektroniki nchini China, wafanyabiashara wa elektroniki wa China wanatoa huduma mpya bila kusita ili kutosheleza mahitaji ya wateja. Mtandao wa utalii wa Yansha mpya ulioanzishwa muda si mrefu uliopita ndio unajitokeza kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya baadhi ya wachina wanaopenda utalii wa kipekee. Kwenye mtandao watalii wanaweza kuchagua njia wanayoipenda na kupanga ratiba, idadi ya watu, namna ya kutalii pamoja na bei. Baada ya kujaza majina yao na kuchagua njia, shughuli zote zinakuwa zimeandaliwa. Mkuu wa mtandao huo bwana Zhao Mingzhe alisema kuwa, japokuwa biashara yao ndiyo inaanza lakini ina mustakabali mzuri. Alisema :

    "Biashara yetu imeingia katika kipindi cha kuagiza kwenye mtandao wa internet badala ya njia ya zamani ya kuagiza kwa kupiga simu. Japokuwa hivi sasa kasi ya maagizo kwenye mtandao wa internet bado ni kidogo, lakini muda si mrefu baadaye, kiasi hicho kitafikia asilimia 50."

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-04