Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-05 17:36:19    
Bara la Afrika laonesha kutilia maanani hifadhi ya mazingira

cri

    Kamati ya tuzo ya Nobel ya Norway muda si mrefu uliopita ilimpa tuzo ya amani ya Nobel naibu waziri wa mazingira na malighafi za kimaumbile ya Kenya Prof. Wangali Maathai, ili kumsifu kwa juhudi zake katika kuhifadhi mazingira na maendeleo endelevu. Jambo hilo limeonesha ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa kwa mazingira ya bara la Afrika.

    Tangu utamaduni wa kigeni kupelekwa na wakoloni barani Afrika, bara la Afrika ambalo binadamu alikuwa na uhusiano mzuri na maumbile kwa miaka milioni kadhaa, sasa linakabiliwa na msukosuko mbaya wa mazingira. Mtaalamu anayefanya utafiti kuhusu historia ya mazingira ya Afrika Bwana Ke Ying amewahi kusema kuwa, baada ya wakoloni kulivamia bara la Afrika, uchumi wa soko huria duniani umebadilisha uchumi wa kimaumbile, maendeleo mabaya yamesababisha uharibifu wa misitu, matumizi ya kupita kiasi ya mbuga, mmomonyoko wa ardhi, mabadiliko ya hali ya hewa, ukame, njaa na maambukizi ya maradhi. Wakoloni waliharibu utaratibu wa kisiasa wa bara la Afrika, kuharibu uwezo wa jadi wa kushirikiana na kupambana na matatizo. Isitoshe, tokea karne iliyopita, nchi za Afrika zilipata uhuru katika muda tofauti na zilikuwa zinazingatia ongezeko la uchumi bila kujali hifadhi ya mazingira. Matatizo la mazingira, pamoja na migongano ya kisiasa na kikabila yanasababisha wakimbizi. Hivyo nchi za Afrika zinapaswa kufuata njia ya maendeleo endelevu inayounganisha vizuri maumbile na maendeleo.

    Bara la Afrika ni bara maskini. Nchi za Afrika zimekwisha tambua kuwa, lazima zifuate njia ya kuhifadhi mazingira na maendeleo endelevu. Kwa hivyo, nchi kadhaa za Afrika zimeanza kushughulikia pamoja suala la mazingira, kusawazisha misimamo kuhusu suala la hifadhi ya mazingira, kuanzisha kwa pamoja sehemu ya hifadhi za wanyama na mimea, na kutafuta maendeleo endelevu ya nguvukazi, jamii na uchumi yanayoambatana na hifadhi ya mazingira.

    Baadhi ya nchi za Afrika mashariki zimeshatunga sheria ya kupiga marufuku kutumia mafuta yenye risasi. Mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, serikali ya Rwanda ilitangaza kupiga marufuku kutumia mifuko wa plastiki nchini kote, na kueneza matumizi ya vikapu vya mianzi na vinginevyo ili kuzuia uchafuzi kwa mazingira. Bibi Maathai aliyepata tuzo ya amani ya Nobel alianzisha harakati ya ukanda wa kijani mwaka 1977, katika miaka 30 iliyopita, aliwahamasisha wanawake kupanda miti karibu milioni 30.

    Japokuwa nchi za Afrika zimefahamu umuhimu wa hifadhi ya mazingira na kuanza kufanya juhudi za kuhifadhi mazingira, lakini bara la Afrika bado linakabiliwa na hali mbaya ya mazingira. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa, mazingira ya Afrika yanakabiliwa na tishio kubwa lisilowahi kutokea hapo kabla. Tokea mwaka 1968, kiwango cha mvua barani Afrika kimekuwa kikipungua mwaka hadi mwaka. Katika miaka 10 toka 1990 hadi 2000, eneo la misitu barani Afrika lilipungua kwa hekta milioni 50, na katika miaka 30 ijayo, ongezeko la idadi ya watu, vita, mabadiliko ya hali ya hewa na uvamizi wa viumbe kutoka nje yataleta tishio kubwa kwa mazingira ya Afrika. Ikiwa nchi za Afrika hazitachukua hatua mwafaka haraka, uchafuzi wa hewa na maji utazidi kuwa mbaya, wanyama na mimea pori itatokomea kwa wingi, na ukame utatokea mara kwa mara.

    Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP limeona kuwa, mapambano dhidi ya tatizo la mazingira barani Afrika yanategemea juhudi pamoja za nchi za Afrika na jumuiya ya kimataifa, kama vile kupunguza mzigo wa madeni, kuongeza misaada kutoka nje, kuingiza ustadi wa hifadhi ya mazingira, na kuziruhusu nchi za Afrika kuuza bidhaa zao kwa usawa kwenye soko la kimataifa.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-05