Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-06 22:20:52    
Makala ya nne ya chemsha bongo:Mambo ya kidiplomasia ya China inayoshikilia nia ya amani na kanuni za kujitawala na kujiamulia mambo

cri
    Leo tunawaletea makala ya nne yaani makala ya mwisho ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya. Leo tunawafahamisha hali ya jumla kuhusu Mambo ya kidiplomasia ya China na mawasiliano kati ya China na nchi mbalimbali duniani.

    Wasikilizaji wapendwa, kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu wa China mwaka 1949 kulikomesha historia ndefu ya uvamizi na kukandamizwa na nchi za nje kwa taifa la China. Tangu hapo China ilifuata njia ya kujitawala na kujiamulia mambo na kuanzisha uhusiano wa amani na kirafiki na nchi mbalimbali duniani.

    Tokea siku ya kuzaliwa kwa China mpya, China ilianza kushikilia sera ya kidiplomasia ya amani ya kujitawala na kujiamulia mambo katika kuendeleza uhusiano na nchi nyingine duniani. Zaidi ya miaka 50 iliyopita, sera hiyo ya kidiplomasia ya China haijabadilika hata kidogo bila kujali mabadiliko ya namna gani yaliyotokea duniani.

    Mwaka 1954, yaani kabla ya miaka 50 iliyopita China, India na Burma (yaani Myanmar ya hivi sasa) zilitetea kwa pamoja kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani kuhusu kuheshimu mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi; kutoshambuliana; kutoingilia mambo ya ndani; kuwa na usawa na kunufaishana; na kuishi pamoja kwa amani. Kanuni hizo tano ni ufafanuzi kamili zaidi kuhusu sera ya kidiplomasia ya amani ya kujitawala na kujiamulia mambo ya China mpya.

    Kanuni hizo zimekuwa kanuni za kimsingi zinazotambuliwa duniani siku hadi siku katika kushughulikia uhusiano kati ya nchi na nchi. Kutokana na msingi wa kanuni hizo tano, China na nchi 165 duniani zimewekeana uhusiano wa kibalozi, na imeanzisha mawasiliano na ushirikiano karibu na nchi na sehemu zote duniani katika nyanja za uchumi na biashara, sayansi na teknolojia, na utamaduni.

    "Amani na maendeleo ni masuala mawili makubwa ya zama hivi", huu ni uchambuzi wa kimsingi kabisa wa China kuhusu hali ya dunia ya sasa. Ilipoingia katika karne ya 21, ingawa mabadiliko makubwa na yenye utatanishi yalitokea katika hali ya dunia, lakini uchambuzi huo wa China bado haujabadilika.

    Kuhusu mambo ya kidiplomasia, China inatetea kuuwezesha uhusiano wa kimataifa kuwa wa kidemokrasia, kupinga umwamba na siasa za kimabavu. China inatetea kuwa nchi kubwa au ndogo, yenye nguvu au dhaifu, zote ziwe sawa katika kushiriki mambo ya kimataifa. Kuhusu kutatua migogoro ya kimataifa, China siku zote inatetea kufanya mazungumzo badala ya mapambano, kupinga matumizi ya nguvu au kutishia kwa nguvu; kuhusu ustaarabu tofauti wa aina mbalimbali wa binadamu, China inatetea kuhifadhi aina mbalimbali za ustaarabu wa binadamu, na kutetea kuwa na aina tofauti za ustaarabu tofauti wa aina mbalimbali na mifumo tofauti ya jamii duniani, pamoja na njia za maendeleo za nchi mbalimbali, zote zinapaswa kuheshimiwa ili kupata maendeleo kwa pamoja katika hali ya kutafuta maoni ya pamoja na kuweka kando maoni tofauti.

    Katika miaka ya hivi karibuni, shughuli za ugaidi zimekuwa zikipamba moto siku hadi siku. Suala la usalama linafuatiliwa na nchi nyingi zaidi na wananchi wake. Kuhusu suala la usalama, China siku zote inatetea kupinga ugaidi na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugaidi duniani; wakati huo huo, China inatetea kuwa na wazo jipya kuhusu usalama, kuwa na mawazo ya kuaminiana ili kupata usalama, kufanya mazungumzo ili kuhimiza usalama, na kupinga kutumia vigezo viwili katika mapambano dhidi ya ugaidi; China inaona kuwa, mapambano ya kijeshi hayawezi kuleta usalama wa kudumu, China inapinga vitendo vya kushambulia mamlaka ya nchi nyingine kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na kupinga kuhusisha mapambano dhidi ya ugaidi na mataifa fulani au dini fulani.

    Hadhi ya Umoja wa Mataifa pia ni suala ambalo limekuwa likifuatiliwa na jumuiya ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni. Kuhusu suala hilo, China inatetea kulinda heshima ya Umoja wa Mataifa na kulinda hadhi ya maamuzi ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia masuala makubwa ya kimataifa, na pia inatetea kuheshimu sheria za kimataifa na kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa zinazotambuliwa duniani kote.

    Kwa mfano kuhusu suala la Iraq, China siku zote inashikilia kuwa lazima kutafuta ufumbuzi wa kisiasa ndani ya Umoja wa Mataifa, na kupinga kuanzisha vita dhidi ya Iraq bila idhini ya Umoja wa Mataifa. Na kuhusu suala la mageuzi ya Umoja wa Mataifa, China ikiwa ni mmoja wa wajumbe watano wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, inaunga mkono Umoja wa Mataifa kufanyiwa mageuzi, na kuunga mkono upanuzi wa baraza la usalama na kuongeza idadi ya wajumbe wa kudumu wa baraza hilo.

    Kuhusu masuala mengine makubwa ya kimataifa, China inatetea kuwa utandawazi wa uchumi wa dunia unapaswa kuwa wenye manufaa kwa nchi zote, na nchi zilizoendelea zinapaswa kuwajibika zaidi katika kuondoa umaskini na kuboresha mazingira.

     Wasikilizaji wapendwa, sasa tayari tumewafahamisha sera na utetezi wa kidiplomasia wa China, sasa tunapenda kuwafahamisha kuhusu hali ya mawasiliano kati ya China na nchi mbalimbali duniani.

    China ni nchi kubwa zaidi kuliko nchi nyingine zote zinazoendelea duniani. Kuimarisha mshikamano na ushirikiano na nchi nyingi zinazoendelea ni msingi wa sera ya kidiplomasia ya China. China na nchi nyingi zinazoendelea za Asia, Afrika na Latin Amerika zilikumbwa na ajali za kihistoria zinazofanana, na pia zina lengo la pamoja la kulinda uhuru wa nchi na kutimiza maendeleo ya uchumi.

    China ikiwa nchi pekee inayoendelea iliyo mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, katika miaka mingi iliyopita imefanya juhudi kubwa za mwakilishi wa nchi zinazoendelea katika Umoja wa Mataifa, na imetoa mchango kwa ajili ya kulinda haki na maslahi ya halali ya nchi zinazoendelea.

    Bara la Afrika ni bara kubwa lenye nchi nyingi zaidi zinazoendelea. China inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano na nchi za Afrika, kushikilia kuendeleza kwa kina ushirikiano kati ya China na Afrika katika nyanja zote kwa msingi wa kanuni za kuwa na usawa na kunufaishana, kutafuta ufanisi halisi wa maendeleo ya aina mbalimbali ili kupata maendeleo ya pamoja. Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lililoanzishwa mwaka 2000 limekuwa utaratibu muhimu wa kufanya mashauriano ya kirafiki na kusukuma mbele ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi za Afrika.

    China ni moja ya nchi yenye majirani wengi zaidi duniani. China inashikilia sera ya ujirani mwema, kujenga mazingira ya usalama na kutimiza maendeleo ya pamoja na nchi jirani. Naibu mkurugenzi wa idara ya Asia katika wizara ya mambo ya nje ya China Bibi Fu Ying alisema:

    China inataka kudumisha ujirani mwema ili kushirikiana na nchi jirani zake katika kujenga mazingira ya urafiki, amani, utulivu, na kujitahidi kupata maendeleo na usitawi wa pamoja.

    China vilevile inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano na nchi zilizoendelea, inatetea kuwa nchi na nchi zinapaswa kutojali tofauti za mifumo ya jamii na itikadi, kuheshimiana, kutafuta maoni ya pamoja wakati wa kuweka kando migongano, ili kupanua ushirikiano wa kunufaishana.

    China pia inatoa mchango mkubwa katika kutatua matatizo makubwa ya kikanda. Kwa mfano, ili kusukuma mbele utatuzi wa kiamani suala la nyuklia la peninsula ya Korea, China imehimiza mara kwa mara kufanyika kwa mazungumzo ya amani ya pande mbalimbali, na kusukuma mbele kuanzishwa kwa utaratibu wa mazungumzo ya pande 6 ya Beijing, kazi hiyo ya China ilisifiwa na pande mbalimbali zinazohusika. Waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing alipotoa hotuba alisisitiza kuwa, China itafuata daima njia ya maendeleo ya amani, alisema:

    Umaalum mkubwa wa maendeleo ya China ni maendeleo ya amani. Njia yetu ya maendeleo ni njia ya kulinda amani ya dunia, kushiriki kwa juhudi katika ushirikiano wa usawa na kunufaishana na kusukuma mbele maendeleo ya pamoja. Maendeleo ya amani ya China yataleta fursa kwa nchi jirani na dunia nzima.

    Wasikilizaji wapendwa, mpaka hapo ndiyo tumekamilisha matangazo ya makala ya nne yaani makala ya mwisho ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 55 ya China mpya. Sasa tunatoa maswali mawili.

    Swali la kwanza: Mpaka sasa China ina uhusiano wa kibalozi na nchi ngapi duniani?

    Swali la pili: Sera ya kidiplomasia ya China inahusu nini? Katika swali hili mnaweza kueleza kutokana na jinsi mlivyosikia matangazo yetu.

    Na tutarudia matangazo ya makala 4 za chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 55 ya China mpya kuanzia tarehe 26 mwezi Septemba katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Makala hizo nne zimekwishawekwa kwenye tovuti yetu ya kiswahili katika kipindi cha sanduku la barua, karibuni mtembelee tovuti yetu. Msisahau anuani yetu ni www.cri.cn. chagua kiswahili.