Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-08 19:01:15    
Historia ya mji wa Kaifeng

cri
    Kaifeng ni mji wenye historia ndefu sana nchini China. Zaidi ya miaka 1000 iliyopita, wafalme 9 wa enzi ya kale ya Song ya kaskazini ya China wote waliufanya mji huo kuwa mji mkuu wa madola yao. Ingawa miaka mingi imepita, lakini mabaki mengi ya kale ya utamaduni yaliyoko hivi sasa mjini Kaifeng, bado yanaonesha usitawi na neema ya mji huo katika zama za kale na historia yake ndefu. Hivyo watalii wengi wanapenda kufanya utalii katika mji huo wa kale.

    Mji wa Kaifeng uko katika mashariki ya mkoa wa Henan nchini China, na ni mmoja kati ya miji mikubwa 7 ya kale nchini China. Mji huo ulikuwa kituo cha siasa, uchumi na utamaduni cha China, pia ulikuwa ni mmoja kati ya miji yenye usitawi mkubwa kabisa duniani katika zama za kale. Kwa kuwa mji huo uko kwenye sehemu ya chini ya mtiririko wa Mto Manjano yaani Mto Huanghe, ulikumbwa na mafuriko makubwa mara 6 katika historia yake, na hata ulifanyiwa ukarabati mara kadhaa. Kutokana na ukarabati huo majengo ya kale ya mji huo ni yenye mitindo tofauti, majengo mengi ya enzi mbalimbali za kimwinyi za China bado yamehifadhiwa vizuri.

    Jumba la Kaifeng lililoko kwenye sehemu ya kati ya mji wa Kaifeng lilikuwa ofisi za maofisa wa enzi mbalimbali za kale. Lakini jumba la asili lilitoweka zamani, jumba la hivi sasa lenye eneo la hekta 4 lilijengwa upya mwaka 2003 kwa kufuata ramani ya enzi ya Song ya kale na kufunguliwa kwa watalii. Mtindo wa ujenzi wa jumba hilo na historia ya asili ya jumba hilo vinastahili kukumbukwa na watu.

    Kila asubuhi mlango wa Jumba la Kaifeng hufunguliwa ili kuwakaribisha watalii. Ukuta wa jumba hilo ni mnene na mrefu, inasemekana kuwa ukuta kama huo uliojengwa zamani kwa madhumuni ya kukinga mashambulizi. Vita ikitokea askari walikuwa wanaweza kupanda haraka kwenye ukuta huo ili kuzuia mashambulizi. Lakini ukuta uliojengwa upya sasa unawarahisishia watalii kupanda juu kuangalia mandhari, hata kwenye jukwaa la ukuta huo kuna meza, vitu vya mawe na vibanda vya mapumziko.

    Ndani ya Jumba la Kaifeng kuna picha za wafalme watatu wakuabudiwa wa enzi za kale ambao inasemekana kuwa waliwahi kufanya kazi katika Jumba la Kaifeng. Na kwenye ukuta wa mashariki na magharibi ya ukumbi wa kufanyia ibada, zilichorwa picha zinazoonesha mfalme wa enzi ya song akiwaongoza askari kupata ushindi katika vita vya kupambana na mashambulizi kutoka nje.

    Ndani ya Jumba la Kaifeng kuna jengo moja lililokuwa likitumika kufanyia mitihani au kutoa hotuba kwa wanafunzi wa enzi za kale. Kutoka kwenye picha zilizochorwa kwenye kuta za ukumbi wa ghorofa ya chini ya jengo hilo, watalii wanaweza kufahamishwa utaratibu wa mtihani wa kupewa nafasi za kushika nyadhifa kwenye kasri la kifalme katika enzi ya Song ya kale. Picha zilizochorwa kwenye kuta ziligawanywa katika sehemu 15 ambazo zilichorwa picha zikionesha wanafunzi wakijiandikisha, hadi kushiriki duru tatu za mitihani mpaka kupata ushindi katika mitihani na kushika wadhifa na kupata heshima na maisha ya fahari. Wanafunzi wenye sura za aina mbalimbali za furaha na huzuni walichorwa vilivyo kwenye picha hizo za ukutani.

Idhaa ya kiswahili CRI 2004-11-08