Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-16 16:52:29    
Soko la bidhaa ndogondogo la Dadeng kwa Taiwan

cri

    Jambo la kwanza analofanya asubuhi mfanyabiashara kutoka Taiwan Bibi Lin Lizhen ni kuwapeleka watoto wake wawili katika shule ya msingi ya Dadeng ya mji wa Xiamen. Kisha anakwenda haraka kushughulikia biashara yake katika soko la Dadeng la bidhaa ndogondogo kwa wafanyabiashara kutoka Taiwan. Amekuwa akifanya hivyo kila siku kwa zaidi ya miaka miwili. Bibi Lin alimwambia mwandishi wetu wa habari,

    "Mimi nilizaliwa kisiwani Taiwan, na tulihamia hapa mwaka 2002. Tulikuja hapa kufanya biashara."

    Mahali anapofanya biashara Bibi Lin Lizhen ni soko la bidhaa ndogondogo mjini Xiamen, lililoidhinishwa na serikali ya China mwaka 1998. Hivi sasa hilo ni soko pekee kwa upande wa China bara la bidhaa ndogondogo kwa wafanyabiashara wa Taiwan, ambalo linasaidiwa na baadhi ya sera za nafuu kwa biashara na Taiwan. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya soko hilo Bw. Feng Qi alipoeleza kuhusu kufungua soko hilo huko, alisema,

    "Kisiwa cha Dadeng cha Mji wa Xiamen kiko karibu sana na kisiwa cha Jinmen cha Taiwan, kiasi ambacho ni umbali wa kilomita 1.8 tu katika sehemu iliyo karibu. Hapo zamani huko kulikuwa na shughuli nyingi za biashara kati ya wakazi wa kando mbili za mlango wa bahari ya Taiwan. Kutokana na chanzo cha kihistoria na kisiasa, shughuli hizo za biashara zilikuwa zikifanyika kiholela na hazikusimamiwa ipasavyo. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kufanya biashara kinyume cha sheria. Lengo la kufungua soko hilo ni kuiwezesha biashara ya bidhaa ndogondogo za kando mbili za mlango wa bahari kufanyika kwa utaratibu mzuri."

    Soko la biashara ya bidhaa ndogondogo la Dadeng, ambalo liko katika kisiwa cha Dadeng, sehemu ya kaskazini mashariki ya mji wa Xiamen lilipangwa kuwa na eneo la hekta 85, lakini eneo linalotumika kwa hivi sasa ni hekta 10 tu likiwa na maduka zaidi ya 500. Ujenzi wa soko hilo umegharimu kiasi cha Yuan za Renminbi milioni 45. Soko hilo lina sehemu za biashara, maghala, mahali pa kutia nanga kwa meli za biashara kutoka Taiwan, sehemu ya huduma, forodha, ofisi za karantini, ulinzi wa mpakani na usimamizi wa mambo ya viwanda na biashara, na soko hilo limezungushiwa ukuta na kuwekewa ulinzi mzuri.

    Soko hilo, ambalo linaruhusu wafanyabiashara wa kando mbili kukodi maduka yaliyojengwa ndani yake na kuuza bidhaa za aina 6 zinazotoka Taiwan zikiwa ni pamoja na nafaka, mafuta ya kupikia, chakula, mazao ya jadi ya kilimo na mifugo, nguo na vitambaa, vitu vya sanaa, bidhaa za viwanda vya kazi nyepesi na dawa. Bidhaa zinazoletwa na meli kutoka Taiwan na kuingia kwenye soko hilo la biashara hazitozwi ushuru wa forodha wa bidhaa zinazotoka nje, ambazo zinauzwa kwa wafanyabiashara wenye maduka ndani ya soko hilo kwa uuzaji wa jumla, kisha kuuzwa rejareja kwa wanunuzi ambao kila mmoja anaruhusiwa kununua bidhaa za Taiwan zenye thamani ya Yuan 1,000 kwa siku bila kutozwa ushuru. Habari zinasema kuwa kanuni hiyo inatarajiwa kubadilishwa hadi kuruhusu mnunuzi kununua bidhaa zenye thamani ya Yuan 3,000 kwa siku.

    Soko la Dadeng la bidhaa ndogondogo zilizotoka Taiwan limekuwa linapendwa sana na wafanyabiashara wa Taiwan kutokana na kuwa na utaratibu mzuri na kutekelezwa sera zenye nafuu. Watu wanaokwenda huko kununua vitu, hasa ni watalii waliotoka sehemu mbalimbali za China bara, ambao wanapenda zaidi vipodozi, vitu vya sanaa za kazi za mikono na pombe. Mwandishi wetu wa habari alimuona mtalii mmoja akinunua chupa 10 za pombe maarufu zilizotengenezwa kwa mtama kisiwani Taiwan. Hadi nusu ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya bidhaa zilizouzwa katika soko hilo imefikia Yuan karibu milioni 200.

    Bidhaa zinazotoka sehemu za China bara vilevile zinapendwa na wafanyabiashara na watalii wanaotoka Taiwan.

    Bwana Zheng Qijiang ni mwenyeji wa Xiamen, na amefanya biashara katika soko hilo tangu miaka kadhaa iliyopita. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa soko hilo linafanya kazi ya kuchangia maendeleo ya uchumi wa kisiwa cha Dadeng. Kabla ya miaka kadhaa iliyopita, kisiwa cha Dadeng kilikuwa kisiwa cha pori, lakini hivi sasa uchumi wa huko umeendelezwa kwa kiwango kikubwa. Alisema kuwa hivi sasa kila mwaka anaweza kupata faida ya zaidi ya Yuan laki moja kwa mwaka. Ameweza kununua nyumba mpya, na sasa anafikiria kununua gari.

    Bibi Lin Lizhen kutoka Taiwan pia anaridhishwa na biashara yake. Anasema anatarajia watu wa kando mbili za mlango wa bahari ya Taiwan, wataweza kuzidisha maelewano yao kutokana na shughuli za biashara za pande hizo mbili.

Idhaa ya Kiswhili 2004-11-16