Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-18 20:35:47    
Maisha ya wakazi wa mji mkongwe wa Xi'an

cri

  

   Xi'an, mji mkuu wa mkoa wa Shanxi, magharibi mwa China ni mji wenye historia ndefu wa China. Mji huu uliwahi kuwa mji mkuu wa enzi 13 katika historia ya China. Japokuwa hivi sasa mji huo wenye idadi ya watu karibu milioni 6 umekuwa ni mji wa kawaida, lakini bado ni mji muhimu wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika sehemu ya magharibi mwa China. Maisha ya wakazi wa Xi'an yanabadilika kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini China.

    Pembezoni mwa ukuta wa mji wa Xi'an unaohifadhiwa vizuri, imejengwa bustani inayozunguka mji yenye urefu wa kilomita 15. Kwenye bustani hiyo, imepandwa miti, nyasi na maua ya aina mbalimbali, kila siku wakazi wapatao elfu kumi hivi wanacheza mchezo wa chess, ngoma na kupumzika kwenye bustani hiyo. Pia watu wanaweza kuendesha mashua kwenye mto unaozunguka mji huo.

    Wasikilizaji wapendwa, mliyoisikia ni opera ya Qing ambayo inaimbwa sana na wazee na wa makamo katika mikoa mingi ya kaskazini magharibi mwa China. Kijana Liu Hui alisema:

   "Napenda kuimba Opera ya Qing tokea utotoni, kwa sababu wazazi wangu wanapenda kuimba opera hiyo, sasa naweza kuimba kama aina kumi za opera ya Qing." 

    Wakazi wa Xi'an wanapenda sana kula chakula chenye pilipili, mjini Xi'an, kuna vyakula vingi vitamu, kama vile mkate unaowekwa kwenye supu ya ng'ombe na mbuzi, nyama za ng'ombe na mbuzi zinazotengenezwa kwa kuwekwa viungo vya aina mbalimbali , jeli za choroko?keki ya matunda yaitwayo persimmon na kadhalika. Bwana Zhao Yugong mwenye umri wa miaka 57 ameishi mjini Xi'an tangu utotoni, na anapenda sana vyakula vya maskani yake Xi'an. Alisema:

    "Tumezoea sana kula nyama ya ng'ombe iliyotengenezwa kwa kuwekwa viungo vya aina mbalimbali, na jeli za choroko, nitajisikia vibaya kama nisipopata vyakula hivyo kwa muda mrefu. Niliwahi kuishi nchini Russia kwa miezi miwili, kila siku nilikuwa nakula chakula cha mtindo wa magharibi, ilikuwa ni vigumu sana kwangu kukizoea chakula hicho. Niliporudi nchini China, kitu cha kwanza kufanya kilikuwa ni kutafuta jeli ya choroko. Karibu wakazi wote wa Xi'an wana uzoefu huo, binti zangu wawili wote wanafanya kazi katika miji mingine, kila wakirudi nyumbani jambo la kwanza pia ni kula bakuli moja ya jeli ya choroko."

    Bwana Zhao alisema kuwa, chakula anachopenda zaidi ni mkate unaotiwa kwenye supu ya nyama za ng'ombe na mbuzi, ambacho ni moja ya vyakula vitamu sana vya mjini Xi'an, na katika mji wa Xi'an, mikahawa ya chakula hicho ipo kila mahali. Supu ya nyama za ng'ombe na mbuzi hupikwa kwenye sufuria kubwa, mtu anaweza kupata harufu yake nzuri hata akiwa mbali. Mteja akiingia mkahawani, hupewa mkate uliotengenezwa kwa unga wa ngano. Mteja hutakiwa kuukata mkate yeye mwenyewe kuwa vipande vidogo vidogo, kuviweka katika bakuli na kumkabidhi mpishi bakuli lake, mpishi anaviweka vipande vya mkate kwenye supu pamoja na nyama za mbuzi au ng'ombe na tambi za mchele. Baada ya hapo huzichemsha kidogo na kuweka kitunguu na kisibiti kidogo, baada ya hapo kitoweo hicho kitamu kinakuwa tayari. Umaalum wa kula chakula hicho ni mteja mwenyewe kuukatakata mkate kuwa vipande vidogo vidogo. Nyama za ng'ombe na mbuzi si kama tu zina ladha nzuri, bali pia zina virutubisho vizuri. Kutokana na sababu hiyo chakula hicho kimeenezwa nchini kote, na mikahawa inayotengeneza chakula hicho pia ipo hapa Beijing.

    

    Wakazi wa Xi'an wanaupenda sana mji wao. Ukuta mkongwe, mahekalu, kasri na mitaa yote imehifadhiwa vizuri. Wakazi wa mji huo pia wana tabia ya kukusanya mapambo ya kale kama vile picha, vyombo vya kauri, sarafu, na sanaa za mikono. Ukiingia ndani ya nyumba za wakazi wa Xi'an, huwezi kukosa kuviona vitu kadhaa vya mapambo ya kale.

    Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya uchumi na kuinuka kwa hali ya maisha, mabadiliko mengi pia yametokea katika mji wa Xi'an , na wakazi wa mji huo wana wakati zaidi kufurahia maisha yao. Hivi sasa wanaweza kuonja chakula cha mtindo wa magharibi, na kununua vitu katika maduka yaliyojaa bidhaa. Katika sikukuu au mwisho wa wiki, wakazi wa mji huo wanapenda kutembelea katika ukumbi wa sanamu za askari na farasi, hekalu la Daying, na mahali pengine penye alama ya Xi'an. Vitongoji vya Xi'an pia vina desturi ya kuwa na magulio. Bwana Zhao Yugong anayefahamu sana desturi ya Xi'an alisema kuwa, ili kuwafahamisha watoto wake desturi ya mji huo, kila akitembelea magulio hayo huambatana na watoto wake.

    "Huwa tunawapeleka watoto kutembelea magulio katika vitongoji ili kuwafahamisha kuwa, licha ya maduka makubwa ya kujihudumia vyakula na vitu mjini, pia wanaweza kununua vitu vingi kwenye soko wazi kama vile goroli."

    Licha ya kufurahia mandhari ya huko, kama ilivyo kwa wakazi wa miji mingine nchini China, wakazi wa Xi'an pia wanapenda kutalii katika sehemu nyingine nchini China na nchi za nje, ili kujionea kwa macho yao wenyewe dunia hiyo yenye mambo mazuri. Kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii ya sehemu ya magharibi nchini China, wakazi wa Xi'an wamekuwa na mahitaji makubwa zaidi kwa hali yao ya makazi na kutalii nje. Baadhi ya wakazi wameweza kununua nyumba mpya na magari madogo, wakiwa wanafurahia faida mbalimbali yanayoletwa na maendeleo ya uchumi nchini China.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-18