Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-23 20:38:02    
Mazao ya kilimo salama ya China yanapendwa na watu wa nchi nyingi

cri

    China ni nchi kubwa ya kilimo na ni nchi ya 6 duniani inayosafirisha nje kwa wingi mazao ya kilimo. Hivi sasa si vigumu kuyaona mazao ya kilimo ya China katika nchi yoyote duniani, ambayo yanapendwa na watu wengi.

    Bwana Cyril Sayag kutoka Ufaransa, ambaye ameishi nchini China kwa miaka minne, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kwao Ufaransa wakazi wanaweza kuona mara kwa mara mazao ya kilimo yaliyotoka China. Alisema,

    "Katika kila mji nchini Ufaransa hata kama ni mji mdogo, watu wanaweza kuona migahawa au super market za wachina, hivyo wakazi wanaweza kupata chakula cha kichina kwa urahisi. Wakazi wa huko wanapenda sana kununua chakula cha kichina, mimi mwenyewe nimekula chakula cha kichina mara nyingi, na ninakipenda sana."

    Huenda wewe ni kama bwana Cyril Sayag, unaweza kuona mazao ya kilimo yaliyosafirishwa kwenu kutoka China katika nchi yako, pengine umewahi hata kupata nafasi ya kuonja chakula kilichotoka China, lakini yawezekana kuwa hujui mazao hayo ya kilimo ya kichina namna yalivyozalishwa mashambani na kusindikwa nchini China. Sasa tunakueleza jinsi shughuli za usindikaji za kiwanda kimoja cha usindikaji wa mazao ya kilimo hapa nchini zinavyofanyika.

    Kampuni ya chakula cha kusafirishwa nchi za nje ya Anqiu, iliyoko katika mkoa wa Shandong, sehemu ya mashariki ya China ni kiwanda kikubwa kinachosindika mazao ya kilimo yanayosafirishwa nchi za nje. Kiwanda hicho chenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Yuan milioni 500 na wafanyakazi 6,000 ni moja kati ya viwanda vikubwa 500 nchini China. Mazao ya kilimo yanayosindikwa katika kiwanda hicho ni pamoja na mboga na matunda yanayohifadhiwa katika hali ya baridi, pamoja na chakula cha nyama. Pato la kiwanda hicho kutokana na mauzo lilikuwa Yuan milioni 560, bidhaa zake hasa zinasafirishwa katika nchi za Japan, Korea ya Kusini, Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya.

    Kampuni ya Anqiu inawavutia sana watu, licha ya kuwa karakana zake zimejengwa kwa utaratibu mzuri, ndani pia imepandwa miti na majani mengi yaliyo kama bustani. Ikilinganishwa na mazingira ya kampuni nyingine, mazingira ya ndani ya karakana ya kiwanda hicho yanayohusika moja kwa moja na usafi wa chakula, ni muhimu zaidi. Ili kuhakikisha usafi na usalama wa chakula, wafanyakazi hawaruhusiwi kuingia kwenye karakana kabla ya kusafishwa na kuviua virusi kwa mara kadhaa.

    Katika karakana inayosindika mboga ya spinachi, wafanyakazi wanaovaa sare safi nyeupe za kazi, wanafanya kazi kando ya mstari wa mitambo ya kazi. Meneja mkuu wa kampuni ya Anqiu Bibi Liu Haiyan alisema kuwa, mitambo hiyo ya kisasa ilinunuliwa kutoka nchini Marekani na Japan. Pia alieleza kuhusu kazi ya kuhifadhi mboga ya spinachi katika hali baridi,

    "Bidhaa nyingi za kiwanda chetu zinazalishwa kutokana na mazao ya kilimo, mchakato wa uzalishaji bidhaa zetu ni pamoja na ukaguzi wa malighafi, kusafisha, kusuuza kwa maji moto, kuchambua na kuzihifadhi katika hali ya baridi kabla ya kuzisafirisha nchi za nje." 

    Nchini China, kuna kampuni nyingi zinazosindika mazao ya kilimo yanayosafirishwa nchi za nje kama kampuni ya Anqiu. Mazao yanayosafirishwa kwa nchi za nje ni pamoja na mazao ya majini, nafaka, mboga, nyama na matunda, ambayo katika mwaka 2003 thamani yake ilikuwa ni zaidi ya dola za kimarekani bilioni 20. Mazao hayo ya kilimo yanasafirishwa kwa nchi zaidi ya 200 zikiwemo Marekani, Japan, Korea ya Kusini, Australia na nchi za Umoja wa Ulaya.

    Ili kuwapatia wateja wa nchi za nje chakula safi na salama, idara husika za serikali ya China zimechukua hatua mbalimbali. Idara ya usimamizi wa ubora na karantini ya China inasimamia moja kwa moja ubora wa mazao ya kilimo, ambayo matawi yake yaliyoko katika sehemu mbalimbali yanafanya usimamizi wa ubora kwa mazao ya kilimo toka mwanzo hadi mwisho, ili kuhakikisha ubora na usalama wa chakula kinachosafirishwa nchi za nje.

    Aidha vitengo hivyo vya usimamizi wa ubora pia vinajitahidi na kuchukua hatua kadha wa kadha za kuinua kiwango cha viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo yanayosafirishwa kwa nchi za nje, zikiwa ni pamoja na kampuni kuwa na mashamba yake zenyewe.

    Hapo zamani, mazao ya kilimo yaliyosafirishwa na kampuni za biashara za China kwa nchi za nje yalisindikwa katika nyumba za wakulima, ambayo ubora wake ulikuwa hafifu na ilikuwa ni rahisi kuchafuliwa kutokana na zana na teknolojia hafifu.

    Ili kuhakikisha ubora wa mazao ya kilimo yanayosafirishwa kwa nchi za nje, ubora wa mazao unafuatiliwa toka mazao ya kilimo yakiwa shambani. Idara za usimamizi wa ubora za China toka mwishoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, zilizishawishi kampuni zinazosafirisha mazao ya kilimo nchi za nje, ziwe na mashamba yake. Mkurugenzi wa idara ya usalama wa chakula kinachosafirishwa nje na kuagizwa kutoka nchi za nje Bwana Li Yuanping alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema.

    "Njia nzuri ya kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuendeleza ujenzi wa mashambani kwa ajili ya kudhibiti uchafuzi kwa mazao ya kilimo, ni kufanya kampuni hizo kuwa na mashamba yake na kushirikiana na idara husika za serikali ili kuongeza ubora wa mazao ya kilimo yanayosafirishwa kwa nchi za nje kutoka mwanzoni."

   

    Hivi sasa karibu kampuni zote za China zinazosafirisha mazao ya kilimo nchi za nje, zimekuwa na mashamba na usimamizi mmoja kutoka mwanzoni ukiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa uzalishaji, kutumia mbegu, miche, mbolea na dawa za kuua wadudu bora, kukagua malighafi za mazao ya kilimo na kuyasindika kwa utaratibu mzuri ili kuhakikisha ubora na usalama wa chakula.

    Kampuni ya Anqiu tunayoizungumzia hivi sasa imekuwa na mashamba zaidi ya 1,500. Malighafi ya mazao ya kilimo inakaguliwa kwa makini kabla ya kupelekwa katika karakana ya usindikaji, na ubora wa mazao unakaguliwa kila baada ya kumalizika kwa kazi moja.

    Uzalishaji wa mazao ya kilimo na teknolojia ya usindikaji ya kampuni ya Anqiu imemvutia sana Konsela wa kilimo wa ofisi ya ubalozi wa Korea ya Kusini nchini China, ambaye alikuwa mmoja wa wageni walioalikwa kutembelea kampuni ya Anqiu. Ofisa huyo baada ya matembezi alisema kuwa, mazao ya kilimo yanasindikwa katika mazingira safi, na aliongeza kuwa mazao hayo yatakuwa na nguvu kubwa ya ushindani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-23