Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-29 17:32:41    
Maabara ya kompyuta iliyojengwa kwa msaada wa China yatoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu ya kompyuta nchini Tanzania

cri

    Maabara ya kompyuta ya chuo cha ufundi cha Dar es Salaam ni moja ya miradi iliyoafikiwa kati ya serikali ya China na ya Tanzania kwenye baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lililofanyika mwaka 2000. Maabara hiyo yenye kompyuta 50 ilijengwa na kuzinduliwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2001. Hadi leo imeshafanya kazi kwa miaka mitatu hivi, na imetoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu ya kompyuta kwa watanzania.

    Bwana Liu Yong ni mwalimu wa kompyuta aliyetumwa na serikali ya China. Alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

    "Jukumu kuu la maabara hiyo ya kompyuta ni kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa idara ya kompyuta ya chuo hicho. Pia kuna wanafunzi wa kozi fupifupi baada ya ratiba za kawaida za madarasa ya wanafunzi wa hapa FDC na ADEs. Muda uliobaki ni kuwasaidia watu wa nje kama vile kufanya semina za mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na shule za sekondari, wanafunzi kutoka jumuiya ya wanawake ya Tanzania na kadhalika."

    Maabara hiyo inafunguliwa kwa siku tano na nusu kila wiki, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tatu usiku. Kwa kuwa hapo ni sehemu inayoweza kutumia mtandao wa internet, hivyo kila siku wanafunzi wengi wanakwenda kufanya mazoezi na kutafuta data kwenye mtandao wa internet.

    Bwana Dennis Shija ni mwalimu wa kompyuta wa maabara hiyo, alipotaja umuhimu wa maabara hiyo alisema:

    "Maabara hiyo imetusaidia sana, ingawaje bado haijampa kila mwanafunzi fursa ya kutumia kompyuta, na internet. Kwa sababu wanafunzi ni wengi na wote wanahitaji. Hivyo bado tunahitaji maabara zaidi ili kila mwanafunzi aweze kuitumia kompyuta."

    "Tunaishukuru sana serikali ya China kwa kutuletea wataalamu ambao wanatusaidia kwenye mambo mengine mengi, ambayo sisi tulikuwa hatuyafahamu. Vile vile tunashukuru kwamba, baadhi ya wenzetu wanapata nafasi ya kusoma katika nchi zilizoendelea kama China, ambao wanakuja na ujuzi na kutuongezea sisi ambao bado tuko hapa. Kwa hiyo kidogo kwa elimu ya kompyuta tumeweza kusogea kidogo mbele, ikilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kwanza walimu walikuwa ni wachache lakini sasa hivi tumekuwa na walimu wengi."

    Bwana Dennis alisema kuwa, sasa hali ya maendeleo ya kompyuta na mtandao wa internet nchini Tanzania imesogea mbele kidogo, alisema:

    "Tukizungumzia internet na kompyuta kwa ujumla, kwa mimi mwenyewe binafsi, naona kama tumeendelea. Kwa upande wa internet wanafunzi wetu wengi wametokea kufahamu internet na kujua jinsi ya kuitumia katika masomo yao. Kutafuta data, na vitu vingine. Ilikuwa ni kama tofauti na zamani ambapo wanafunzi walikuwa wanategemea tu vitabu ambavyo vilikuwa haviwezi kuwatosheleza. Kwa upande mwingine, kwa sasa hivi utaona kuna vifaa vya internet pamoja na kompyuta ambazo zinasaidia kwa kiasi kikubwa sana kwa wanafunzi na walimu kupata data kwa ajili ya kujiendeleza. Hivyo tunaweza kusema kuwa kuna maendeleo, tumeweza kusogea mbele upande wa internet na kompyuta."

    Bwana Frank Mbano mwenye umri wa miaka 50 mwaka huu ni mwalimu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, sasa yeye pia ni mwanafunzi anayesomea shahada ya pili, alikuja kujifunza na kufanya mazoezi katika maabara hiyo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-29