Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-30 14:30:51    
China yaendeleza uzalishaji wa chai isiyo na vitu vyenye madhara kwa afya ya binadamu

cri
Mama Han Ping mwenye umri wa miaka 71 mwaka huu ni mzaliwa wa mji wa Jinan, siku chache zilizopita mwandishi wetu wa habari alipomwona kwenye maonesho ya kimataifa ya China yaliyofanyika nchini China, alikuwa akinyanyua kikombe na kuonja chai. Mama Han alisema kuwa ameishi miaka mingi, na kitu anachopenda zaidi ni kunywa chai. Alisema,

    "Mimi ninapenda sana kunywa chai ya rangi ya kijani. Chai ya rangi ya kijani inaweza kuondoa mafuta yaliyoganda kwenye mishipa ya damu, cholesterol na kupunguza nguvu ya msukumo wa damu. Mimi nina matatizo ya mafuta mengi kwenye mishipa ya damu na nguvu kubwa ya msukumo wa damu, hivyo licha ya kutumia chai ya rangi ya kijani, mimi na mume wangu tunatumia chai ya Wulong. Kila siku alasiri saa tisa hivi, mimi na mume wangu tunatengeneza chai nyumbani. Tunakunywa kila siku, inatufaa sana kwa afya zetu!"

    Hapa nchini kuna idadi kubwa sana ya watu wanaopenda kunywa chai kama mzee Hao Ping. China ni nchi ya chanzo cha chai, na chai nchini China ilianza kutumika kabla ya miaka elfu 4 au 5 iliyopita, na inapendwa na wachina tangu zamani za kale. Katika miaka ya karibuni pamoja na kuinuka kwa kiwango cha maisha, watu wanazingatia sana afya zao, chai isiyo na mabaki ya dawa za kilimo na vitu vingine vyenye madhara inapendwa na watu wengi. Hivi sasa karibu miji yote nchini China ina maduka na migahawa ya chai. Tunachukua mfano wa mji wa Beijing, biashara ya chai ni nzuri sana. Katika duka maarufu la chai linalojulikana kwa WU Yutai, meneja wa duka hilo bibi Guo Ling alimwambia mwandishi wetu wa habari,

    "Katika miaka ya karibuni, mahitaji ya chai kwa wakazi yanaongezeka kwa mfululizo. Mauzo ya chai ya duka letu yanaongezeka kwa wastani wa 10% kwa mwaka, biashara ya chai ni nzuri sana."

    Kuongezeka kwa wapenzi wa chai kumehamasisha uzalishaji wa chai nchini. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2003 mashamba ya chai nchini China yalifikia hekta milioni 1.2, ikichukua nafasi ya kwanza duniani, uzalishaji wa chai umezidi tani laki 7 kwa mwaka na pato la sekta ya uzalishaji wa chai limefikia Yuan za Renminbi bilioni 34 kwa mwaka.

    Nchini China chai pia inatumiwa katika usindikaji wa chakula na vinywaji, hata inatumiwa kutengeneza vipodozi. Kwa mfano maji ya chai yanatumiwa katika kukaanga mbegu za matikiti-maji ambazo ni moja ya vitafunwa.

    Pamoja na kuhitaji chai nyingi, wachina pia wanapenda kununua chai bora na kuzingatia mazingira ya utengenezaji wa chai na sehemu za uzalishaji wa chai. Matakwa hayo ya wanunuzi yameihimiza sekta ya uzalishaji wa chai kuzalisha chai isiyo na vitu vyenye mabaki ya dawa za kilimo na vitu vingine vya kikemikali, ambavyo vinaathiri afya ya binadamu.

    Kiongozi wa kampuni ya uzalishaji wa chai maarufu ya Puer kutoka mkoa wa Yunnan, sehemu ya kusini magharibi ya China, bibi Wang Xia alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa ili kuwapatia wateja chai bora, wameanzisha mashamba yao ya chai katika sehemu za juu za milima ambazo hazijachafuliwa na vitu vya kikemikali. Bibi wang Xia alisema,

    "Chai ya Puer inatengenezwa kutokana na majani ya michai ya Puer inayoota katika milima mikubwa ya mkoani Yunnan, ambayo haikuchafuliwa na uchafuzi wa kikemikali. Bidhaa zetu za chai ya Puer hivi sasa zinauzwa sana, hata baadhi yake zinasafirishwa katika nchi za Ulaya."

    Hivi sasa kampuni nyingi za chai zina mashamba yake zenyewe ya chai, ambapo wafanyakazi wa mashamba ya chai wanaruhusiwa kutumia mbolea ya samadi kidogo tu, kwenye michai ya mashambani ili kuepusha uchafuzi wa vitu vya kikemikali.

    Ili kujenga utaratibu mzuri wa uzalishaji wa chai, serikali ya China pia imechukua hatua nyingi zikiwa ni pamoja na kuweka kanuni za kupiga marufuku kwa matumizi ovyo ya mbolea ya chumvichumvi na dawa za kilimo. Idara husika za China zimebuni kiwango kwa upimaji wa vitu vya mabaki ya mbolea na dawa za kilimo, na ni chai inayolingana na kiwango kilichowekwa, ndiyo inaruhusiwa kuuzwa. Ili kuhakikisha ubora wa chai, hivi sasa, kampuni nyingi za chai za China zinatumia teknolojia ya kisasa za kukausha chai, kuhifadhi chai katika halijoto baridi na katika mifuko isiyo na hewa ndani.

    Aidha, kwa baadhi ya chai maarufu, China inatekeleza sera za kuhifadhi sehemu asilia za uzalishaji. Kwa mfano, sehemu ya Longjing ya ziwa la magharibi mkoani Zejiang ni moja ya sehemu iliyohifadhiwa na serikali. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya chai ya Longjing, Bw. Qi Guo-wei alipoeleza mambo hayo alisema, "Sera za hifadhi ni pamoja na ya kwanza, kuweka eneo la Longjing ni kilomita za mraba 168, na chai inayozalishwa katika eneo hilo inachukuliwa kuwa ni chai ya Longjing. Pili, kila hekta inaruhusiwa kuzalisha kilo 375 tu za chai. Na tatu ni kuanzisha maduka maalumu ya chai ya Longjing ili kuwawezesha wateja kupata chai ya Longjing ya kweli."

    Katika miaka ya karibuni, chai bora inayosafirishwa kwa nchi za nje imekuwa ikiongezeka kwa haraka. Naibu mkurugenzi wa jumuiya ya kusafirisha mazao ya kijadi ya kilimo na mifugo ya China, bwana Yang Shengjun alisema kuwa mwaka jana chai iliyosafirishwa nje ilifikia tani laki 2.6 ikichukua nafasi ya tatu duniani. Kati ya chai iliyosafirishwa kwa nchi za nje, chai ya Puer inapendwa sana na wateja wa nchi za Asia ya kusini mashariki na Ulaya. Libya na Morocco zinapenda chai ya rangi ya kijani ya China. Na chai ya Wulong inapendwa na wateja wa nchi ya Japan. Ili kukidhi mahitaji ya nchi hizo, idara husika za China zinajitahidi kutekeleza wazo la kuzalisha chai isiyo na vitu vinavyoathiri afya za binadamu.

    Bwana Yang Shengjun anasema kuwa ubora wa chai ya China unasifiwa na watu wengi duniani hivi sasa idara za serikali zinashirikiana na kampuni zinazohusika kuchukua hatua ili kuongeza ubora wa chai ya China na kuifanya ilingane na kiwango kilichowekwa duniani kuhusu chakula cha usalama na cha teknolojia. Aliongeza kuwa katika siku za usoni, China itatumia ubora wa rasilimali zake, kuongeza thamani ya mazao ya chai ya China, kuendelea kuzalisha chai isiyo na vitu vinavyoathiri afya za watu.

Idhaa ya kiswahili 2004/11/30