Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-30 21:47:28    
Kuwafuatilia kina mama na kupambana na ugonjwa wa ukimwi

cri

    Mwaka 1988 Shirika la afya duniani WHO liliamua kuwa tarehe mosi Desemba ya kila mwaka ni siku ya dunia nzima kutoa elimu kuhusu kinga na tiba ya ukimwi, ili kuwahamasisha watu wa dunia nzima washirikiane katika kupambana na ugonjwa wa ukimwi. Tarehe mosi Desemba mwaka huu ni siku ya 17 ya ugonjwa ukimwi ya kimataifa, kauli mbiu yake ni "Kuwafuatilia kina mama na kupambana na ugonjwa wa ukimwi".

    Tangu kugunduliwa kwa mgonjwa wa kwanza wa ukimwi mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, ugonjwa wa ukimwi umekuwa ukienea kwa haraka sana kote duniani. Shirika la afya duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi yalitoa Taarifa ya uchunguzi kuhusu ugonjwa wa ukimwi tarehe 23 Novemba ikikadiria kuwa, mwaka 2004 wagonjwa wa ukimwi na watu walioambukizwa virusi vya ukimwi wamefikia milioni 39.4, na milioni 4.9 miongoni mwao ni watu walioambukizwa ukimwi mwaka huu, na mwaka huu watu milioni 3.1 kote duniani wamekufa kwa ugonjwa wa ukimwi.

    Taarifa hiyo pia imedhihirisha mwelekeo wa kasi wa maambukizi ya virusi vya ukimwi miongoni mwa kina mama. Nusu ya wagonjwa wa ukimwi na walioambukizwa virusi vya ukimwi ni kina mama. Nafasi za kuambukizwa virusi vya ukimwi kwa wanawake vijana na watoto wa kike ni mara 2.5 kuliko wanaume vijana na watoto wa kiume kote duniani. Katika sehemu ya Afrika kusini mwa Sahara, wanawake walioambukizwa virusi vya ukimwi ni asilimia 60 ya idadi ya jumla ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi. Na katika sehemu mbalimbali duniani, wanawake walioambukizwa virusi vya ukimwi na wagonjwa wanawake wa ukimwi wameongezeka kwa kiasi kubwa mwaka huu kuliko miaka miwili iliyopita, ndiyo maana kauli mbiu ya siku ya ukimwi ya kimataifa ya mwaka huu imethibitishwa kuwa "kuwafuatilia kina mama na kupambana na ukimwi".

    Wataalamu wameainisha kuwa, kutokana na umaalum wa afya ya wanawake na tofauti za kijinsia, wanawake huwa ni wadhaifu kuliko wanaume katika jamii na uchumi, hivyo tishio la ukimwi kwa wanawake ni kubwa sana kuliko lile kwa wanaume. Hivyo kusisitiza kuwafuatilia kina mama na watoto wa kike ni kwa ajili ya kuihimiza jamii nzima ichukue hatua zaidi ya kinga na tiba ya ukimwi, kuwahamasisha kina mama wajifunze ujuzi kuhusu kinga na tiba ya ukimwi, kupata matibabu kwa usawa, kuongeza mawazo na uwezo wa kujilinda ili kujiepusha na ugonjwa wa ukimwi.

    Shirika la afya duniani na Shirika la kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa yamedhihirisha kuwa, hali ya ubaguzi dhidi ya wagonjwa wa ukimwi na watu walioambukizwa virusi vya ukimwi inaonekana katika nchi mbalimbali duniani. Wagonjwa wa ukimwi wanapoteseka na ugonjwa, pia wanabaguliwa na kudhalilishwa na watu wa pembeni mwao ama kutengwa na jamii. Ubaguzi huo unatokana na sababu nyingi mbalimbali kama vile kutokuwa na ujuzi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, kuwa na uzushi mbalimbali au maoni yasiyo sahihi kuhusu maambukizi ya ukimwi, kutoweza kupata matibabu mwafaka ama kusikia habari zisizo sahihi zinazotolewa na vyombo vya habari. Hayo yote yamewafanya wagonjwa wa ukimwi wasikitishwe sana moyoni. Ili kukwepa ubaguzi au udhalilishaji, wagonjwa hao hufanya chini juu kuficha hali yao ya ugonjwa. Matokeo yake ni kuwa, hospitali haziwezi kupata hali halisi ya maambukizi ya ukimwi, hivyo maambukizi ya ukimwi yanaendelea zaidi katika jamii. Mashirika hayo mawili yameona kuwa wakati wa kutokomeza ubaguzi huo umewadia.

    Mwezi Desemba mwaka 2003 shirika la afya duniani lilianzisha kampeni moja ya kuwapatia dawa na matibabu mwafaka ifikapo mwaka 2005 watu walioambukizwa virusi vya ukimwi wapatao milioni 3. Lakini hii bado iko mbali sana na lengo la binadamu la kudhibiti ukimwi, hivyo shirika la WHO linaona kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za dharura ili kuzuia kwa pamoja ugonjwa wa ukimwi usienee zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-30