Mkutano wa nane wa viongozi wa China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki umemalizika huko Vientian, mji mkuu wa Laos. Wakati wa mkutano huo, China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki zilitiliana saini mikataba muhimu, ambayo imesukuma kuanzishwa kwa eneo la biashara huru kati ya pande hizo mbili katika hatua halisi. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya utafiti wa uchumi wa dunia wa taasisi ya utafiti wa masuala ya kimataifa ya China Bibi Wei Min leo alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa hatua hiyo itaharakisha mchakato wa utandawazi wa uchumi wa kikanda wa Asia.
Kutiwa saini kwa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na biashara ya bidhaa wa eneo la biashara huria la China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki na mkataba wa utaratibu wa utatuzi wa migogoro kati ya China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki, ni moja ya mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo.
Mikataba hiyo miwili inaagiza kuwa China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki zitaanza kupunguza ushuru wa forodha kwa biashara la eneo hilo kuanzia mwaka kesho, ambao utafikia kiwango cha asilimia 5 au chini zaidi kabla ya mwaka 2010; na nchi za Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki zimetambua hadhi ya uchumi wa soko ya China. Kuhusu mikataba hiyo miwili, bibi Wei Min alisema,
"Mikataba hiyo miwili ni yenye umuhimu wa kihistoria. Kisiasa, inaonesha kuwa uhusiano kati ya China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki umeingia kipindi kipya cha ushirikiano wa pande zote. Kiuchumi, inaonesha kuwa kuanzishwa kwa eneo la biashara huru la China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki kumeingia katika hatua halisi. Kutiwa saini kwa mikataba hiyo kumeondoa vikwazo kwa uanzishaji wa eneo la biashara huria kwa pande hizo mbili, na uhusiano wao wa kiuchumi utaendelezwa kwenye msingi wa mikataba hiyo na hatimaye kutimiza lengo la kuanzisha eneo la biashara huria, kunufaishana na kustawi kwa pamoja."
Katika miaka ya karibuni, ushirikiano kati ya China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki ulipata maendeleo makubwa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande hizo mbili umekuwa mkubwa na kutegemeana zaidi mwaka hadi mwaka. Katika miaka 10 iliyopita, biashara kati ya pande hizo mbili ilikuwa na wastani wa ongezeko la asilimia 20 kwa mwaka. Katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka huu, thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili inakaribia dola za kimarekani bilioni 85.
Mwanzoni mwa mwaka huu, China ilitangulia wakati kufungua mlango wa soko la mazao ya kilimo, ambapo nchi nyingi za umoja wa Asia ya Kusini Mashariki, ambazo zinategemea kilimo, zimenufaika kutokana na eneo la biashara huria la pande hizo mbili. Licha ya hayo, China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki ziliandaa maonesho ya biashara na mkutano wa viongozi wa nchi kuhusu uwekezaji, hatua ambayo imefungua uwanja kwa ushirikiano wa pande hizo mbili.
Aidha, pande mbili zimekuwa na ushirikiano mkubwa katika kustawisha kilimo, mawasiliano na sehemu unayopita mto wa Meikong. Bibi Wei Min, ambaye amefanya utafiti kwa miaka mingi kuhusu uchumi wa Asia ya mashariki, anaona kuwa ushirikiano mkubwa wa kiuchumi kati ya pande hizo mbili unatokana na uhusiano wao mzuri wa kisiasa. Alisema,
"Naona uhusiano mzuri wa kisiasa kati ya pande hizo mbili unatoa mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati yao, vilevile ushirikiano mkubwa wa kiuchumi unahimiza maendeleo ya uhusiano wa kisiasa, naona uhusiano kati ya vitu hivyo viwili ni wa kuhimizana."
China na Umoja wa Nchi za Asia ya Kusini Mashariki zote zimefanya juhudi kubwa, ili kuhakikisha eneo la biashara huru kati ya nchi hizo linaanzishwa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-02
|