Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-02 21:22:06    
Wachina wanapenda michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje siku hadi siku

cri

    Hivi sasa wachina wanaofanya kazi ofisini wanapenda sana michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje. Huwa wanasafiri kwa kuendesha magari yao wenyewe, au kupanda majabali, kupanda mlima, au kutembea kwa miguu nje ili kujionea uzuri wa mazingira ya kimaumbile.

    Bwana Zhang Yuan ni karani wa kampuni, muda si mrefu uliopita alimaliza kazi yake ya mwaka huu, hivyo akaamua kusafiri kwenda sehemu ya magharibi kwa kuendesha gari mwenyewe pamoja na marafiki zake. Bwana Zhang alisema kuwa, amechagua njia hiyo ya kujiburudisha kutokana na kuwa na gari yeye mwenyewe na kutaka kubadili mazingira ya kimaisha.

    "Baada ya kuishi mjini kwa kipindi kirefu, nimechoka kuona vitu vya aina moja, hivyo natamani sana kubadili mazingira angalau kwa muda tu."

    Bwana Zhang alisema kuwa, tofauti na kupanda ndege au gari moshi, kusafiri kwa kuendesha gari mwenyewe ni rahisi sana, anaweza kusafiri kama anavyopenda. Alisema kuwa, akiwa na wakati wa kutosha, huwa anakwenda safari kwa mara kadhaa kwa mwaka, safari fupi au ndefu.

    Tofauti na Bwana Zhang, Bibi Zeng Yu anapenda sana kupanda mlima. Kwa kuwa mji anaoishi uko katika mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China. Huko kuna milima mingi maarufu, kila ifikapo likizo ndefu au sikukuu ya taifa, mashabiki wa kupanda mlima kutoka sehemu mbalimbali nchini China humiminikia mkoani Sichuan. Bi. Zeng alisema kuwa, zamani yeye alikuwa akifanya mazoezi katika jumba la mazoezi ya kujenga afya, lakini sasa ameacha kufanya mazoezi ya nyumbani na kuanza kupanda majabali na mlima.

    "Zamani watu wengi walipendelea kufanya mazoezi kwenye majumba ya mazoezi ya kujenga afya, kwanza kwa kukimbia kwenye mashine ya kukimbilia, halafu kufanya mazoezi kwenye chombo cha kufanyia mazoezi kutokana na mwongozo wa kocha, hakuna raha hata kidogo. Siku moja nilipata nafasi ya kupanda majabali na niliupenda sana mchezo huo mara moja. Najisikia kuwa, kupanda majabali ni bora zaidi kuliko kufanya mazoezi nyumbani ."

    Kwa wanafunzi wasiokuwa na pesa za kutosha, huwa wanapenda kufanya safari kwa miguu kwenye sehemu ambazo hazina watalii wengi, na wanaita njia hiyo kuwa "utalii wa kujitesa". Yaani wanapaswa kubeba mzigo mzito, na kuishi na kula chakula katika nyumba za wakulima. Au kulala kwenye hema na kula chakula kikavu .

    Msichana Lin Weijing ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha ualimu cha Nanjing, kuanzia mwaka jana alianza kupenda safari ya kwenda mlimani. Akiwa na wakati, msichana Lin huenda kusafiri pamoja na wenzake, na mara kwa mara wakakumbwa na matatizo wasiyowahi kuyafikira, lakini hata hivyo anaona amepata faida kubwa kutokana na safari hizo za kujitegemea.

    "Japokuwa safari ya kujitegemea ni safari ya kuchosha, kila mara mimi hutokwa na jasho jingi, na wakati mwingine huwa nakutana na hatari, lakini najisikia vizuri sana, si kama tu naweza kufanya mazoezi, bali pia naweza kukaribia maumbile. Maisha ya shuleni ni ya anasa, safari ya kujitegemea inaweza kuinua uwezo wangu wa kujimudu katika hali ngumu, pia itaniwezesha kushiriki kwa ushindani jamii baada ya kuhitimu masomo."

    Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaopenda michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje, maduka yanayouza bidhaa maalum za michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje yameanza kuongezeka na yanauza vitu kama vile mikoba ya safari, mahema, fumba, makoti ya kuzuia upepo na majiko.

    Katika miaka ya hivi karibuni, klabu za michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje zimeanzishwa katika miji kadhaa nchini China. Klabu hizo huwaandikisha watu wanaopenda kufanya michezo nje. Klabu ya michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje ya wafugaji ya Shanghai ni klabu kubwa kabisa ya aina hiyo nchini China. Katika miaka miwili iliyopita tangu ianzishwe, imekuwa na wanachama zaidi ya 10,000. Klabu hiyo kila wiki inapanga safari ya kwenda nje mara mbili au tatu, kama vile kufanya pikiniki na kupanda mlima. Mhusika wa klabu hiyo Bwana Li Chungang alisema kuwa, wanachama wa klabu hiyo wanatoka kwenye fani mbalimbali, lakini wote wanajiunga na klabu hiyo kwa ajili ya kujipatia maisha yenye furaha zaidi. Alisema :

    "Wanachama wana lengo tofauti, baadhi yao ni wapya katika mji huo, hivyo nia yao hasa ni kukutana na watu, wengine wanajiunga nasi kwa ajili ya kujenga afya. Lakini jambo muhimu zaidi ni kuwa, watu wote wanatafuta maisha mazuri zaidi."

    Bibi Liu Xiaoyi alijiunga na klabu moja ya michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje mwaka mmoja uliopita, sasa amekuwa kiongozi wa klabu hiyo. Alisema kuwa, michezo ya kujiburudisha inayofanyika nje inamsaidia kuondoa hisia za shinikizo la maisha ya mjini na kufurahia mandhari ya nje. Anapotembea mlimani huwa anasahau usumbufu wote wa kimaisha, hivyo anapenda sana kupanda mlima. Japokuwa kupanda mlima ni kama kazi ya sulubu, lakini kunamsaidia sana katika maisha yake. Tofauti na zamani, sasa Bi. Liu amekuwa ni mtu mchangamfu na mkakamavu anayekaribishwa zaidi na watu walio karibu naye.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-02