Mkutano wa 5 wa mwaka wa Shirikisho la amani la mabunge ya Asia ulifungwa jana huko Islamabad, mji mkuu wa Pakistan. Wakati wa mkutano huo wajumbe wa nchi mbalimballi walijadili masuala mengi makubwa yanayofuatiliwa kuhusu siasa, usalama, uchumi na jamii chini ya kauli mbiu ya kutimiza amani na maendeleo kwa kupitia mazungumzo kati ya mabunge, na wamepata maoni mengi ya pamoja.
Mkutano huo wa mwaka umethibitisha malengo mengi ya mbali kwa kutimiza amani na maendeleo ya sehemu ya Asia, malengo hayo yanafuata hali halisi na yana umuhimu mkubwa.
Wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo wanaona kuwa, katika dunia ya hivi sasa, amani na maendeleo yamekuwa mkondo usiozuilika wa zama, Bara la Asia linakabiliwa na fursa nyingi mpya za maendeleo. Hali ya jumla ya amani katika dunia imeweka mazingira mwafaka kwa maendeleo ya Asia; maendeleo ya kina ya utandawazi wa uchumi duniani, na marekebisho ya haraka ya miundo ya uzalishaji duniani yanasaidia nchi za Asia kutumia mitaji ya kimataifa kwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazogawanyika na kufanya ushirikiano ; na maendeleo makubwa sana ya mapinduzi ya kisayansi na kiteknolojia pamoja na kazi mbalimbali za ushirikiano mzuri duniani zimeziwezesha nchi za Asia kupata fursa ya kujifunza na kuingiza sayansi na teknolojia za hali ya juu na uzoefu mzuri wa uzalishaji ili kutumia ipasavyo nguvu zao zenyewe kwa kujipatia maendeleo makubwa.
Wakati huohuo watu wameanza kuona kuwa, amani ya kudumu na maendeleo endelevu ya Bara la Asia bado yanakabiliwa na changamoto nyingi: matishio ya jadi na yasiyo ya jadi yanachanganyika, ushindani wa kimataifa unazidi kuwa mkali siku hadi siku, pengo kati ya kusini na kaskazini linaendelea kupanuka, utaratibu mkongwe wa kisiasa na kiuchumi usio wa haki na halali duniani bado haujaweza kubadilika. Ili kutumia vizuri zaidi fursa na kukabiliana na changamoto, wajumbe wa nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano walitoa maoni na mapendekezo mengi ya kiujenzi yanayohusika na sekta mbalimbali, maoni na mapendekezo hayo yameoneshwa vilivyo kwenye "Taarifa ya Islamabad" iliyopitishwa kwenye mkutano huo wa mwaka.
Hadhi na mchango wa China katika Shirikisho la amani la mabunge ya Asia inavutia zaidi. Naibu spika wa bunge la umma la China Bibi Uyunqimuge alipotoa hotuba isemayo "Mabunge ya nchi za Asia kuimarisha ushirikiano na mazungumzo na kusukuma mbele amani na maendeleo", alitoa mapendekezo manne yaani kushikilia kanuni tano za kuishi maisha kwa pamoja, kuondoa migogoro kwa kupitia mazungumzo, kufanya ushirikiano kwa kutafuta usalama, kujenga kwa pamoja mazingira ya amani na utulivu ya kikanda; kuheshimu hali tofauti mbalimbali barani Asia, kuimarisha mazungumzo na maingiliano kati ya nchi zenye tofauti za imani ya dini na mfumo wa kisiasa ili kuongeza maelewano na uaminifu; kuimarisha usawazishaji na ushirikiano katika mambo ya kimataifa na kikanda, kusukuma mbele mazungumzo kati ya kusini na kaskazini, ili kuhimiza demokrasia na uhusiano wa kimataifa, na kuweka utaratibu mpya wa kisiasa na kiuchumi ulio wa haki na usawa duniani; kuzidisha ushirikiano wa kikanda, kusukuma mbele mchakato wa utandawazi wa uchumi, kusukuma mbele maingiliano na ushirikiano kati ya nchi mbalimbali kwenye nyanja za sayansi na teknolojia, jamii na utamaduni, ili kuongeza uwezo wa kukabiliana kwa pamoja migogoro na kutimiza usitawishaji kwa pamoja. Bibi Uyunqimuge alisisitiza kuwa, China inayoendelea siku hadi siku inasaidia kuimarisha amani na maendeleo ya Bara la Asia, na hayo yamekuwa ni maoni ya pamoja ya nchi nyingi za Bara la Asia.
Miaka mitano iliyopita tangu kuanzishwa kwa shirikisho la amani la mabunge ya Asia, wajumbe wa nchi mbalimbali wametambua wazi zaidi kuwa, mustakbali wa amani na maendeleo ya Bara la Asia ni wenye mwangaza, lakini pia utakabiliana na njia yenye vikwazo vingi. Kutimiza amani na maendeleo hakutaweza kufanikiwa mara moja tu, kunatakiwa juhudi za pamoja za nchi mbalimbali za Asia kwa muda mrefu. Kama alivyoainisha naibu spika wa bunge la umma la China Bibi Uyunqimuge kuwa, katika hali mpya, nchi za Asia zinapaswa kuwa na mshikamano na ushirikiano na kufanya juhudi za pamoja ili kujitegemea na kujikakamua, ndipo zitakapoweza kutumia fursa, kushinda taabu na kusukuma mbele amani na maendeleo ya pamoja .
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-03
|