Kiongozi wa Fatah Bw. Marwan Barghouti, ambaye hivi sasa amefungwa na Israel, juzi alitangaza ghafla kuwa atashiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Januari mwaka kesho kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mamalaka ya utawala wa Palestina. Habari hii inafuatiliwa na pande zote.
Mnamo tarehe 26, mwezi uliopita, Bw. Barghouti kupitia msaidizi wake alitangaza kuwa, ili kulinda mshikamano wa Fatah, hatashiriki kwenye uchaguzi mkuu. Pia aliwasihi Wapalestina kumwunga mkono Bw. Abbas kuwa mgombea wa Fatah kushiriki katika uchaguzi huo. Kutokana na kubadili msimamo wake wa mwanzo na kuamua kushiriki katika uchaguzi, msaidizi wa Bw. Barghouti alisema kuwa, Bw. Barghouti ameamua kufanya hivyo ili kulinda mapinduzi ya Palestina yanayoendelea kwa miaka minne. Bw. Barghouti aliwalaani viongozi wa Fatah kujaribu kuyaaibisha mapinduzi ya Palestina na alisema kuwa wamekwenda kinyume cha njia ya marehemu Arafat. Habari nyingine za Palestina zinasema kuwa, Bw. Barghouti alitangaza ghafla kushiriki kwenye uchaguzi ili kutoa shinikizo kwa wakuu wa Fatah. Aidha, kwa mujibu wa gazeti la Haaretz la Israel, sababu nyingine iliyomfanya Bw. Barghouti kubadili maoni yake ni kwamba, baadhi ya wanasiasa wa Palestina siku hizi wanasema kuwa hawatamwunga mkono Bw. Abbas kushiriki katika uchaguzi. Pia inakadiriwa kwamba, wakala wa Bw. Barghouti anamshawishi sana kushiriki uchaguzi ili kutoa shinikizo kwa Israel na kumwachia huru mapema.
Habari kuhusu Bw. Barghouti kutangaza ghafla kushiriki kwenye uchaguzi imeleta mshangao mkubwa ndani ya Fatah. Kwa sababu Bw. Barghouti anapata uungaji mkono wa watu wengi wa kawaida, hivyo kushiriki kwake bila shaka kutamnyang'anya kura nyingi kutoka Bw. Abbas. Aidha, jambo hili litaifanya Fatah kuzidi kufarakana na huenda kuzinufaisha jumuiya nyingine kama Hamas na hivyo kuifanya hali ya siasa ya Palestina kuwa vigumu zaidi kutabiriwa. Katibu mkuu wa ikulu ya Palestina Bw. Tayeb Abdul Rahim usiku wa tarehe 1 alitoa taarifa akisema kuwa uamuzi wa Bw. Barghouti kushiriki kwenye uchaguzi "hauwezi kupokewa". Alisema kitendo chake kimekiuka sheria husika za Fatah. Pia alisema kuwa Bw. Barghouti alipoamua kushiriki kwenye uchaguzi amejiondoa uanachama wa Fatah. Habari zinasema kuwa, hivi sasa baadhi ya viongozi wa Fatah wanawasiliana na Bw. Barghouti na kumshawishi aachane na uamuzi wake.
Habari hiyo kuhusu Bw. Barghouti kushiriki kwenye uchaguzi pia inafuatiliwa na Marekani na Misri. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Colin Powell alisema kuwa, uamuzi wa Bw. Barghouti utasababisha matatizo mengi. Rais wa Misri Bw. Hosni Mubarak alisema anatumai kuwa, Wapalestina "watasema kwa sauti moja", kuacha tofauti kati ya pande mbalimbali na kufanya juhudi ili kulinda mshikamano wa Palestina.
Baada ya kusikia uamuzi wa Bw. Barghouti, waziri mkuu wa Israel Bw. Sharon alisema wazi kwamba Israel haitamwachia huru Bw. Barghouti.
Kwanza, hivi sasa maoni ya raia nchini Israel hayaungi mkono kumwachia huru Bw. Barghouti. Pili, kumwachia huru Bw. Barghouti kutaongeza mabadiliko mengi kwa mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel. Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Marekani haipendi kuona hali hiyo. Hivi sasa lengo la Marekani ni kumhakikisha Bw. Abbas anachaguliwa na kuendesha madaraka bila matatizo.
Kwa mujibu wa maoni ya kiraia yaliyokusanywa na idara moja chini ya mamlaka ya utawala wa Palestina, uungaji mkono wa Bw. Abbas ni asilimia 41. Al Aksa Martyrs Brigades iliyokuwa "kambi" ya Bw. Barghouti baada ya kusikia habari ya Bw. Barghouti kushiriki uchaguzi pia ilieleza wazi kuwa, ili kulinda mshikamano wa Fatah itaendelea kumwunga mkono Bw. Abbas.
|