
Baada ya kashfa ya ufisadi wa mpango wa mafuta-kwa-chakula kuanza kujulikana na watu, hasa kuwepo kwa ushahidi unaoonesha kuwa mtoto wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan pia anahusika na kashifa hiyo, baadhi ya watu nchini Marekani wamemtaka Bw. Annan ajiuzuru kwa mara nyingi. Lakini nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimesema kuwa zinamwunga mkono Bw. Annan. Maoni ya umma yamefafanua kuwa Wamarekani hao wanaotaka Bw. Annan ajiuzuru bila shaka wana lengo lao.
Tarehe 10 mwezi Desemba mwaka 1996, Umoja wa Mataifa ulianza mpango wa mafuta-kwa-chakula ambao uliruhusu kampuni za nchi kadhaa kununua mafuta ya Iraq, na Iraq kutumia mapato hayo kununua bidhaa kwa matumizi ya raia. Mpango huo ulimalizika mwezi Novemba mwaka jana. Kashfa ya ufisadi wa mpango huo ilianza kujulikana mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu. Gazeti moja la Iraq lilifunua kuwa, ili kupata uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa, rais wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein alitumia mapato hayo kuwapa rushwa maofisa wa serikali, waandishi wa habari na watu wengine zaidi ya 270 kutoka nchi 46, pamoja na mkuu wa ofisi ya usimamizi wa mpango wa mafuta-kwa-chakula ya Umoja wa Mataifa Bw. Benon Sevan. Mwezi Aprili mwaka huu, Bw. Kofi Annan aliwateua watu watatu kuunda kikundi cha kuchunguza jambo hilo. Kikundi hicho kitatoa ripoti ya kwanza katika majira ya spring mwakani.
Lakini mwezi uliopita, kamati ya uchunguzi ya baraza la juu la bunge la Marekani inayoongozwa na Bw. Norm Coleman ilisema kuwa imepata ushahidi kuwa utawala wa Saddam ulikiuka kisirisiri vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa, na kukusanya dola za kimarekani bilioni 21.3 kupitia njia haramu ikiwemo mpango wa mafuta-kwa-chakula. Katika makala ya Bw. Coleman iliyotolewa katika gazeti la Wallstreet Journal, alisema kuwa kashifa mkubwa kabisa katika historia ya Umoja wa Mataifa ilitokea wakati Bw. Kofi Annan akiwa katibu mkuu, kujiuzuru kwake hakukwepeki. magazeti mengi kadhaa ya Marekani likiwemo gazeti la New York Times pia yametoa makala kadhaa zinazotaka Bw. Annan ajiuzuru.
Msemaji wa Bw. Annan Bw. Fred Eckhard juzi alisema kuwa, hivi sasa hakuna nchi mwanachama yoyote wa Umoja wa Mataifa inayotaka Bw. Annan ajiuzuru. Bw. Annan ataendelea kutekeleza wajibu wake katika kipindi cha miaka miwili na mwezi mmoja kijacho. Aidha, wafanyakazi zaidi 2700 wa umoja huo wameonesha uungaji mkono wao kwa kumwandikia barua pamoja wakisema kuwa, wanaziunga mkono kazi za Bw. Annan zenye uwiano, haki na uhuru wakati sifa ya umoja huo inapotiliwa shaka.
Kwa nini watu kadhaa wakiwemo Bw. Coleman wamekuwa wakimtaka Bw. Annan ajiuzuru? Kuna sababu mbili:
Kwanza, siku zote Marekani haipendi kitendo cha Umoja wa Mataifa cha kutoifuata, bila shaka itachochea mambo. Tunaweza kugundua hii katika maneno ya Bw. Coleman. Alitishia kuwa, kama Bw. Annan ataendelea kushika cheo chake, atahimiza Marekani kupunguza ada ya uanachama ya umoja huo. Kama inavyojulikana, Marekani ilichelewesha ada yake ya uanachama kwa miaka mingi, mpaka mwaka jana ililipa kimsingi ada hiyo iliyochelewesha. Katibu mkuu wa zamani wa umoja huo Bw. Boutros Boutros-Ghali aliwahi kusema kuwa, kutokana na Marekani kuchelewesha ada nyingi, miaka ya karibuni Umoja wa Mataifa ulikabiliwa na tatizo kubwa la kifedha, kutokuwa na fedha kumesababisha umoja huo kusitasita mara kwa mara unapotekeleza mpango wa mageuzi. Alisema kuwa, alipokuwa katibu mkuu, ilimbidi aiombe Marekani mara nyingi kulipa ada yake iliyocheleweshwa. Inaonekana kuwa watu kadhaa wakiwemo Bw. Coleman wanataka kuutishia Umoja wa Mataifa tena kwa ada ya uanachama.
Pili, hii ni alama nyingine ya siasa ya upande mmoja wa Marekani. Katika miaka ya karibuni, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa ya upande mmoja, na kusababisha hadhi, mchango na athari ya Umoja wa Mataifa kuathirika kwa kiasi fulani. Kama naibu waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Yuri Fedotov alivyosema jana, lawama ya Wamarekani kadhaa haina msingi, na kitendo chao kinalenga kupunguza mchango wa Umoja wa Mataifa katika mambo ya kimataifa na kuharibu kanuni ya pande nyingi katika maingiliano ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-03
|