Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-06 22:31:34    
Rais mteule wa Afghanistan Hamid Karzai akabiliana na changamoto kubwa

cri
Rais mteule wa Afghanistan Hamid Karzai akabiliana na changamoto kubwa

Tarehe 7 mwezi huu, Bwana Hamid Karzai, ambaye ni rais wa kwanza aliyechaguliwa na raia katika historia ya Afghanistan ataapishwa kushika wadhifa wa urais. Vyombo vya habari vimeona kuwa, japokuwa Bwana Karzai alishinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa urahisi, lakini kutokana na matatizo yaliyosababishwa na mgogoro wa kivita wa miongo kadhaa, ukarabati wa Afghanistan unakabiliwa na changamoto kubwa, hivyo Bwana Karzai pia ana jukumu kubwa na njia ndefu.

Kwanza kabisa, kutokomeza kundi la Taliban na kundi la Al-Qaeda, na kulinda usalama na utulivu wa nchi hiyo ni changamoto kubwa kabisa inayomkabili Bw. Karzai. Utawala la Taliban uliangushwa miaka mitatu iliyopita, lakini Taliban bado ina nguvu kubwa katika sehemu ya kusini na kusini mashariki, na mara kwa mara wafuasi wa Taliban wamekuwa wanafanya mashambulizi nchini Afghanistan, na hii ni sababu kubwa ya kuhatarisha usalama wa nchi hiyo. Hivyo, hali ya usalama nchini Afghanistan bado si ya kufurahisha.

Pili, kuimarisha madaraka ya serikali kuu na kunyang'anya silaha kutoka kwa mabwana wa kivita wa kisehemu ni suala lingine gumu linalomkabili Bw. Karzai. Mgogoro wa kivita uliokuwepo kwa miongo kadhaa nchini Afghanistan umesababisha hali ya mgawanyo nchini humo. Mabwana wa vita wenye silaha nzuri wamedhibiti madaraka ya kisiasa, kifedha na kodi za sehemu mbalimbali. Serikali ya Afghanistan ilianza kutekeleza mpango wa kunyang'anya silaha za kisehemu tokea Oktoba mwaka jana, lakini kuna kipingamizi kikubwa. Kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, watu elfu 20 tu wamenyang'anywa silaha, bado kuna watu laki moja ambao wanatakiwa kunyang'anywa silaha. Wachambuzi wameona kuwa, japokuwa Bwana Karzai ana uhuru wa kuunda baraza la serikali yeye mwenyewe, na hana haja ya kufanya mashauriano na mabwana wa vita, lakini mabwana wa vita hawazezi kukaa kimya, hivyo si rahisi kwa Karzai kuunda serikali mpya yenye uwiano.

Tatu, kufufua uchumi na kuondokana na umaskini pia ni jukumu kubwa kwa Bw. Karzai. Afghanistan inakabiliwa na jukumu kubwa ya ukarabati, kwenye mikutano miwili ya kimataifa kuhusu suala la Afghanistan iliyofanyika mjini Tokyo na Berlin, Bw. Karzai alipata ahadi ya msaada wenye dola za kimarekani zaidi ya bilioni 11. Lakini inakadiriwa kuwa, ukarabati wa Afghanistan katika miaka 7 ijayo utahitaji dola za kimarekani bilioni 28.

Isitoshe, Afghanistan pia inakabiliwa na suala la kutokomeza kilimo na biashara ya dawa za kulevya. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa, kilimo cha dawa za kulevya kimeongezeka haraka, hivi sasa Afghanistan imekuwa nchi kubwa kabisa duniani inayozalisha dawa za kulevya. Afghanistan ina ukosefu wa raslimali, ardhi yake haina rutuba na hali yake ya kimaumbile ni mbaya. Hivyo kilimo haramu cha dawa za kulevya kimekuwa chanzo muhimu cha mapato. Kama ikitaka kuacha kabisa kilimo hicho, lazima kwanza ipate zao lingine la kiuchumi linaloweza kulibadili zao linalotumika kutengeneza dawa za kulevya, ili kutatua tatizo la njaa na umaskini, lakini hili si jambo rahisi.

Wachambuzi wanaona kuwa, ukarabati na maafikiano ya Afghanistan yatakuwa mchakato wa kipindi kirefu. Akiwa rais mteule wa kwanza wa kiraia, Bwana Karzai anakabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali.