Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-07 10:48:19    
Mapambano dhidi ya ugaidi kuendelea nchini Saudi Arabia

cri
    Ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah, Saudi Arabia tarehe 6 ulishambuliwa na watu wenye silaha na kusababisha vifo vya watu 12. Wachambuzi wanaona kuwa ingawa wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia siku hiyo ilitangaza kuwa tukio hilo limemalizika, lakini matukio mfululizo yaliyozushwa na magaidi miaka ya karibuni nchini humo yanaonesha kuwa mapambano kati ya Saudi Arabia na magaidi yataendelea.

    Habari zinasema kuwa kundi la watu wenye silaha asubuhi ya siku hiyo walitumia baruti kali na silaha kuushambulia ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah. Magaidi hao waliwaua walinzi wanne na kuingia kwenye ubalozi huo na kuwateka wafanyakazi wenyeji 18 waliokuwa kwenye ubalozi huo.

    Mara tu baada ya kutokea kwa tukio hilo, Saudi Arabia ilituma askari wa kikosi cha ulinzi na polisi wapatao 200 kuingia kwenye ubalozi huo na kupambana vikali na magaidi hao. Waliwaua magaidi watatu na kuwakamata wengine wawili. Katika mapambano hayo, wafanyakazi wenyeji watano waliuawa.

    Wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia ilitoa taarifa baadaye ikisema kuwa kikosi cha usalama cha nchi hiyo kimedhibiti hali ya ubalozi huo na tukio hilo limemalizika. Lakini taarifa hiyo haikudokeza hali kuhusu wafanyakazi wa ubalozi huo waliotekwa nyara na magaidi hao.

    Mpaka hivi sasa uraia na madhumuni ya magaidi hao bado havijulikani. Kutokana na uchambuzi wa watu wenye taarifa za kuaminika, ni dhahiri kuwa tukio hilo lilifanywa na kundi la Al-Qaeda nchini Saudi Arabia. Msemaji wa ubalozi wa Marekani nchini humo alisema kuwa wafanyakazi wa Marekani walioko katika ubalozi mdogo wa Jeddah hawakudhuriwa.

    Tangu mwezi Mei mwaka 2003, matukio mfululizo ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wageni wanaoishi nchini humo na serikali ya Saudi Arabia, yamekuwa yakitokea nchini humo na kusababisha vifo vya watu 170. Ingawa serikali ya nchi hiyo ilichukua hatua nyingi za ulinzi, lakini mashambulizi ya kigaidi yalitokea mara kwa mara.

    Wachambuzi wanaona kuwa sababu kubwa ya kuifanya Saudi Arabia ishindwe kuzuia mashambulizi ya kigaidi nchini humo ni kuwa, msingi wa magaidi upo nchini humo. Saudi Arabia ni nchi ya kiislam iliyofungwa sana, bila shaka kuna waislamu wenye msimamo mkali. Pia kuna Wasaudi katika kundi la Al-Qaeda linaloongozwa na Osama Bin Laden. Magaidi hao wanauchukia sana utamaduni wa magharibi na kulenga shabaha lao kwa nchi za magharibi.

    Zaidi ya hayo, serikali ya Saudi Arabia siku zote imekuwa na uhusiano mwema na nchi za magharibi ikiwemo Marekani. Baada ya kutokea kwa tukio la tarehe 11 Septemba, magaidi hao waliona kuwa wametafuta njia ya kupambana na nchi na ustaarabu wa magharibi, yaani kutumia ugaidi kupambana na maslahi ya Marekani na nchi nyingine za magharibi duniani.

    Kwa hiyo tukio hilo la kushambuliwa kwa ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah linaonesha tena kuwa magaidi hao hawataishia hapa, na mapambano dhidi ya ugaidi nchini Saudi Arabia yataendelea.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-07