Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-07 21:01:06    
Tishio kubwa linaloikabili jumuiya ya kimataifa na tishio la silaha za viumbe

cri

   Mkutano wa kimataifa wa nchi wanachama wa "Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Viumbe" mwaka 2004 ulifanyika huko Geneva kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 10 mwezi Desemba. Jumuiya ya kimataifa inaona umuhimu wa kuimarisha mkataba huo kutokana na kuongezeka kwa matishio ya silaha za viumbe na maambukizi ya maradhi duniani. Mkataba huo umekuwa silaha muhimu ya nchi mbalimbali duniani ya kukabiliana na matishio ya silaha za viumbe.

    "Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Viumbe" ukiwa wa mfumo wa mikataba ya kudhibiti zana za kisilaha duniani na ni sehemu muhimu ya mpango wa usalama wa pamoja hususan wa Umoja wa Mataifa, tangu ulipoanza kutekelezwa mwaka 1975, umetoa mchango mkubwa katika kupiga marufuku na kuteketeza silaha za viumbe na kuzuia kuenea kwa silaha za aina hiyo. Baada ya kuingia karne mpya, hali ya usalama duniani imekumbwa na mabadiliko makubwa. Usalama wa kimataifa unakabiliwa na changamoto kali kutokana na kuongezeka kwa vyanzo vya aina nyingi vikiwemo vya kijadi, ugaidi, maambukizi ya magonjwa na kuenea kwa silaha za kuhikilisha umma. Hususan ni kuwa pindi vijidudu na virusi vinapobadilika kuwa silaha za magaidi, usalama wa dunia utakabiliwa na hatari kubwa, hivyo kutekeleza kwa ukamilifu "Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Viumbe" ni muhimu zaidi kwa hivi sasa.

    Katika miaka ya karibuni, nchi zilizosaini "Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Viumbe" ziliitisha mkutano wa wataalamu na mkutano mkuu wa nchi wanachama, ambayo imetoa nafasi muhimu kwa nchi mbalimbali kujadili na kubadilishana uzoefu wao katika kuimarisha nguvu na kutekeleza mkataba huo. Katika mkutano wa wataalamu uliofanyika mwezi Julai mwaka huu, washiriki walikuwa na majadiliano kuhusu mada mbili za kuimarisha usimamizi juu ya maambukizi ya maradhi na uwezo wa jumuiya ya kimataifa wa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matumizi ya silaha za viumbe. Mkutano mkuu wa mwaka huu wa nchi wanachama utatoa maoni na mapendekezo juu ya msingi wa mkutano wa wataalamu wa mwaka huu ili kuwa na maoni ya namna moja na kuchukua hatua nzuri zaidi za kutekeleza mkataba huo. Balozi wa China kuhusu upunguzaji wa zana za kijeshi Bw. Hu Xiaodi tarehe 6 alipotoa hotuba kwenye mkutano huo, alitoa wito wa kutaka nchi mbalimbali ziwe na mtazamo mpya wa usalama wenye msingi wa kuaminiana, kunufaishana, usawa na ushirikiano, na kuzitaka ziimarishe mazungumzo na ushirikiano, kuhifadhi utaratibu wa kimataifa wa kudhibiti, kupunguza na kuzuia kueneza zana za kisilaha ili kukabiliana kwa pamoja na matishio ya magaidi yakiwemo matumizi ya silaha za viumbe.

    Wataalamu wanaona kuwa kuimarisha usimamizi kuhusu maambukizi ya magonjwa na kugundua mapema mashambulizi ya silaha za viumbe ya magaidi ni muhimu sana. Katika upande huo, serikali za nchi mbalimbali zinapaswa kubeba majukumu na kujenga na kuboresha mfumo wa sheria kuambatana na hali halisi ya nchi yake na kuimarisha uwezo wa nchi wa kusimamia na kukabiliana na maambukizi ya magonjwa. Jumuiya zinazohusika duniani pia zinatakiwa kufanya ushirikiano. Nchi zilizosaini mkataba huo zinatakiwa kutoa misaada ya fedha, teknolojia na zana kwa nchi wanachama zinazohitaji msaada. Aidha nchi wanachama zinatakiwa kuimarisha upashanaji habari kuhusu maambukizi ya magonjwa na kuchukua hatua za kukabiliana nayo, hatua ambazo zinafaa sana kwa kuimarisha uwezo wa dunia wa kukabiliana na maambukizi ya magonjwa na kuchukua tahadhari dhidi mashambulizi ya silaha za viumbe ya magaidi.

    China siku zote inapendekeza kupiga marufuku na kuteketeza kabisa silaha za viumbe, na inaunga mkono kuimarisha nguvu ya mkataba huo katika kanuni za nchi nyingi. Balozi wa China kuhusu upunguzaji wa zana za kijeshi Bw. Hu Xiaodi katika mkutano mkuu wa nchi wanachama alisema kuwa serikali ya China inatoa kipaumbele kwa usalama na afya za wananchi, imebuni sheria husika kadha wa kadha, imejenga mfumo wa dhamana wa usimamizi, utoaji wa taarifa na kufanya uchunguzi kuhusu maambukizi ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea. Pia amesema China inazingatia mawasiliano na ushirikiano pamoja na nchi na jumuiya husika, itajitahidi kupunguza na kudhibiti maambukizi ya magonjwa, kuimarisha ufanisi wa "Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Viumbe" na kutokomeza kabisa matishio ya silaha za viumbe.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-07