|
Hivi karibuni, jumuiya ya kimataifa imefuatilia sana shughuli za kidiplomasia katika mashariki ya kati, mabadiliko mazuri yaliyotokea kati ya pande mbili za Palestina na Israel kuhusu mchakato wa amani. Juhudi zilizofanywa na Marekani na nchi nyinginezo zimeonesha kuwa, mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel unaelekea katika hali nzuri ya kufufuka. Lakini kuzindua upya mchakato wa amani kunahitaji zaidi vitendo madhubuti.
Baada ya kiongozi wa Palestina Yasser Arafat kufariki dunia, tatizo kubwa linalowakumba watu wa Palestina ni kuwa, mgogoro ulioendelea kwa miaka minne utaelekea wapi? Mwanzoni mwenyekiti wa sasa wa kamati ya utendaji ya ukombozi wa Palestina Bwana Mahmoud Abbas anayepinga matumizi ya nguvu na kushikilia mazungumzo ya amani alipata asilimia 4 tu ya waungaji mkono, lakini uchunguzi umeonesha kuwa, hivi sasa watu wa Palestina wanaomwunga mkono wameongezeka sana. Wakati huohuo, watu wanaounga mkono kundi la FATAH wameongezeka, wakati watu wanaoliunga mkono kundi la HAMAS lenye siasa kali wamepungua. Bwana Abbas alisisitiza kuwa, Palestina lazima itumie vizuri fursa hiyo mpya. Hivi karibuni, kwa upande mmoja, Bwana Abbas amefanya mazungumzo na vikundi mbalimbali nchini Palestina ili kutuliza hali ya kisiasa ya ndani na kujaribu kuhimiza kusimamisha mapambano dhidi ya Israel. Kwa upande mwingine, alijaribu kuihimiza Israel kukaa kwenye meza ya mazungumzo, na kuzitembelea nchi jirani za kiarabu ili kujipatia uungaji mkono zaidi.
Mgogoro wa miaka minne pia umebadilisha msimamo wa watu wa Israel. Dhana iliyotolewa na chama cha wafanyakazi cha Israel kuhusu kuondoka kutoka sehemu ya Gaza sasa imeanza kupata uungaji mkono wa watu wengi wa Israel.
Kufariki kwa Arafat, kushika madaraka ya urais kwa mfululizo kwa rais Bush, na hali ngumu ya Marekani nchini Iraq kumeilazimisha Marekani kurekebisha sera yake kwa Palestina na Israel. Wachambuzi wanaona kuwa, nia ya Marekani kuunga mkono uchaguzi mkuu wa Palestina ni kujaribu kuifanya Palestina kama ngome yake nyingine ya kidemokrasia katika sehemu ya mashariki ya kati baada ya Iraq.
Jambo linalostahili kufuatiliwa ni kuwa, Umoja wa Ulaya unajaribu kuimarisha ushawishi wake katika suala la Palestina na Israel. Baada ya kufariki kwa Arafat, Umoja wa Ulaya ulikuwa umeonesha juhudi kubwa katika kusuluhisha uhusiano kati ya Palestina na Israel, nchi kadhaa kubwa za Ulaya kwa nyakati tofauti zilituma mawaziri wao wa mambo ya nje kwenda Palestina na Israel kueleza nia yao. Waziri mkuu wa Uingereza Bw Tony Blair ameufanya utatuzi wa suala la Palestina na Israel kuwa suala la dharura la kimataifa kutokana na matakwa yake ya kisiasa. Japokuwa umuhimu wa nchi za Ulaya hauwezi kulingana na ule wa Marekani, lakini msimamo wao wenye uwiano zaidi katika mchakato wa amani wa mashariki ya kati, bila shaka utasaidia utatuzi wa mgogoro wa Palestina na Israel.
Nchi za kiarabu pia zimeimarisha nguvu katika kusukuma mbele mchakato wa amani wa Palestina na Israel. Rais Hosni Mubarak wa Misri anawaunga mkono viongozi wapya wa Palestina kufanya upya mazungumzo na Israel.
Tukiangalia historia ya Palestina na Israel, tumaini la amani liliwahi kuonekana mara nyingi, lakini lilipotea mara moja baada ya lingine. Palestina na Israel zikitaka kutimiza amani, zinapaswa kusonga mbele kwenye njia ya kufanya mazungumzo, kuacha mgogoro zikiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-08
|