Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-08 22:38:25    
Umoja wa Afrika watoa mchango mkubwa wa kuelekeza kushughulikia mambo ya kikanda

cri

    Katika mwaka 2004 utakaomalizika hivi karibuni, maendeleo na ukuaji wa Umoja wa Afrika umekuwa tukio moja linalovutia kabisa kwenye jukwaa la siasa za Afrika. Kazi ya uongozi wa Umoja wa Afrika katika utatuzi wa mambo ya kikanda umefuatiliwa na nchi mbalimbali duniani.

    Umoja wa Afrika ulianzishwa mwaka 2002 badala ya Umoja wa nchi huru za kiafrika. Katika zaidi ya miaka miwili tu iliyopita, ujenzi wa Umoja wa Afrika unabadilika siku hadi siku. Hasa mwaka huu, Umoja wa Afrika umeingia katika kipindi cha ujenzi wa pande zote, na maendeleo makubwa yamepatikana katika ujenzi wa vyombo mbalimbali vya umoja huo, na umepiga hatua kubwa katika mchakato wa utandawazi.

    Umoja wa Afrika unapopevuka siku hadi siku, unaimarisha kwa kiasi fulani kazi na hadhi yake katika kutatua mambo ya kikanda. Mwaka 2004, hali ya ujumla barani Afrika inaelekea kuwa tulivu, maafikiano na maendeleo, na ongezeko la mfululizo la uchumi pia limedumishwa. Lakini sehemu hiyo bado ina sababu kadhaa zisizo za utulivu, kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea katika nchi kadhaa za Afrika ya magharibi pamoja na suala la Darfur la Sudan. Kutokana na kukabiliwa na hali ya utatanishi ya kikanda, Umoja wa Afrika umejitahidi kufanya kazi ya uelekezaji katika kushughulikia mambo ya kikanda.

    Kuhusu suala la Darfur, Umoja wa Afrika unafanya juhudi kuihimiza serikali ya Sudan na jeshi la upinzani kufanya mazungumzo ili kuondoa mgogoro, na kusisitiza kuwa suala hilo linapaswa kutatuliwa kwenye eneo la bara la Afrika. Hivyo mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Nigeria Olusengun Obasanjo kwa mara tatu alizialika pande mbili zinazopambana za Darfur zifanye mazungumzo huko Abuja, na mwisho kuzifanya pande hizo mbili zifikie makubaliano kuhusu suala la ubinadamu na suala la usalama. Umoja wa Afrika pia ulipeleka askari mara mbili katika sehemu ya Darfur. Hatua hizo za Umoja wa Afrika zimefanya kazi muhimu katika kutuliza hali ya Darfur na kuzuia hali ya sehemu hiyo isizidi kuwa mbaya.

    Aidha Umoja wa Afrika umefanya kazi kubwa sana katika kulinda amani ya sehemu ya maziwa makuu. Toka mwezi Mei hadi Juni mwaka huu, hali ya sehemu ya mpaka wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Rwanda ilikuwa ya wasiwasi kutokana na tukio la sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lililozushwa na askari kadhaa wa jeshi la upinzani la Rwanda wanaong'ang'ania nchini humo. Katika wakati wa hatari, rais Obasanjo aliwaalika viongozi wa nchi hizo mbili kufanya mashauriano uso kwa uso huko Abuja, mwishowe hali ya wasiwasi ya sehemu hiyo ilipungua. Mwezi Novemba mwaka huu, mkutano wa kwanza wa wakuu wa sehemu ya maziwa makuu ya Afrika kuhusu amani na maendeleo ulifunguliwa huko Dar es Salaam, mkutano huo ulioendeshwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ulipitisha "Taarifa ya Dar es Salaam". Rais Obasanjo alisifu sana taarifa hiyo, alisema kuwa taarifa hiyo ina umuhimu wa kihistoria, na itaielekeza sehemu ya maziwa makuu na bara zima la Afrika kuingia kipindi kipya cha maendeleo.

    Zaidi ya hayo, Umoja wa Afrika umefanya kazi muhimu kwa kupunguza mgogoro wa Cote D'ivoire ulioibuka mwezi Novemba. Kwanza rais Thabo Mbeki wa Afrika ya kusini alikabidhiwa jukumu na Umoja wa Afrika kwenda Cote D'ivoire kufanya usuluhishi wa kidiplomasia. Halafu kutokana na mwaliko wa rais Obasanjo, viongozi wa nchi au wajumbe wa serikali kutoka nchi 7 za Afrika walifanya mkutano wa dharura huko Abuja, kuzihimiza pande mbalimbali zinazopambana kuacha vitendo vyote vya kijeshi, na kutekeleza kwa makini makubaliano mbalimbali ya amani yaliyosainiwa. Rais Obasanjo alitangaza pia kuwa Umoja wa Afrika unaunga mkono azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kuviwekea vikwazo vikundi mbalimbali vya Cote D'ivoire pamoja na vikwazo vya silaha. Chini ya usuluhishi wa Umoja wa Afrika, mgogoro wa Cote D'ivoire umepungua kwa kiasi fulani.

    Wakati huo huo, Umoja wa Afrika unajitahidi kusukuma mbele maendeleo ya mkutano wa maafikiano ya kitaifa na amani ya Somalia uliofanyika nchini Kenya.

    Ni dhahiri kuwa, Umoja wa Afrika umekuwa nguvu kubwa ya uongozi barani Afrika. Kutokana na juhudi zake, bara la Afrika linafuata njia ya amani na maendeleo siku hadi siku.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-08