Waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq Bw. Allawi jana alimaliza ziara yake ya siku 3 nchini Russia. Hii ni mara ya pili kwa viongozi wapya wa Iraq kufanya ziara nchini Russia baada ya utawala wa Saddam kuangushwa mwaka jana. Mwezi Desemba mwaka jana, mwenyekiti wa zamu wa kamati ya usimamizi ya muda ya Iraq Bw. Hakimu alitembelea Moscow. Ingawa safari hii nchi hizi mbili Russia na Iraq hazijasaini waraka wowote halisi wa ushirikiano, lakini rais Putin wa Russia kumwalika kiongozi wa Iraq kuizuru Russia kumeonesha kuwa nchi hizo mbili zinatumai kuendelea na kukuza ushirikiano wa jadi wa kirafiki.
Uhusiano wa ushirikiano kati ya Russia na Iraq umekuwepo kwa miaka mingi. Katika zama ya Urusi ya zamani, Baghdad ilikuwa rafiki muhimu wa Moscow katika eneo la Mashariki ya Kati, na nchi hizo mbili zilikuwa zinashirikiana sana katika nyanja za siasa, uchumi na biashara na teknolojia ya kijeshi. Wakati ule, Iraq ilikuwa ni soko muhimu kwa silaha za Urusi ya zamani. Asilimia 80 ya zana za kijeshi za jeshi la Iraq zilinunuliwa kutoka Urusi ya zamani.
Baada ya Umoja wa Mataifa kuiweka vikwazo Iraq, Russia iliendelea kushirikiana na Iraq katika msingi wa mpango wa "mafuta kwa chakula" uliowekwa na Umoja wa Mataifa. Kabla ya vita ya Iraq kuzuka, kampuni zaidi ya 200 za Russia zilikuwa zinafanya biashara nchini Iraq. Maslahi ya uchumi ni sababu moja muhimu iliyofanya Russia iipinge Marekani kuanzisha vita nchini Iraq. Baada ya utawala wa Saddam kuangushwa, Russia inatumai kujenga tena uhusiano mzuri na serikali mpya ya Iraq. Rais Putin alipokutana na Bw. Hakimu mjini Moscow mwezi Desemba, mwaka jana alisema kuwa, Russia inazingatia sana ushirikiano mzuri kati ya wananchi wa nchi hizo mbili, na baadhi ya kampuni za Russia zimejiandaa kushiriki katika ukarabati wa Iraq baada ya vita. Iraq inatumai kuwa Russia itafanya kazi katika kuisaidia kukabidhi madaraka na pia inazikaribisha kampuni za Russia kushiriki katika kazi ya ukarabati wa Iraq baada ya vita.
Suala la deni ni suala muhimu la hivi sasa linalozikabili nchi hizo mbili. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Russia, hivi karibuni Russia iliamua kuisamehe Iraq asilimia 90 ya deni lake. Waziri wa fedha wa Russia alisema kuwa, kazi hii itamalizika mwaka 2008. Rais Putin juzi alipozungumza na Bw. Allawi alisema kuwa, Russia ni nchi ambayo inaisamehe Iraq deni kubwa kabisa katika Klabu ya Paris. Alisema anatumai kuwa viongozi wa sasa wa Iraq na serikali mpya ya Iraq itazingatia maslahi ya kampuni za Russia nchini Iraq. Bw. Allawi aliishukuru Russia kusamehe deni lake na kusema kuwa hii itasaidia Russia kufanya kazi muhimu katika ukarabati wa uchumi na viwanda vya Iraq.
Rais Putin na Bw. Allawi pia walijadiliana kuhusu kufanya ushirikiano katika nyanja za nishati na uwekezaji. Wamekubaliana kikanuni kujenga mfumo kati ya serikali za nchi hizo mbili ili kujadili uwezekano wa kutekeleza makubaliano husika yaliyosainiwa wakati wa utawala wa Saddam. Waziri wa viwanda na nishati wa Russia juzi alidokeza kwa vyombo vya habari kuwa, kamati kati ya serikali ya nchi hizo mbili inaweza kufanya mkutano mwezi Februari, 2005 ili kujadili makubaliano yaliyosainiwa zamani. Bw. Allawi jana alipohojiwa na vyombo vya habari vya Russia nchini Moscow alisema kuwa, Iraq itashirikiana na Russia na kusaini nayo mapatano yoyote, na kampuni za Russia zinapaswa kushiriki katika ukarabati wa Iraq.
Russia ikishirikiana na Iraq haitapata tu maslahi ya uchumi, pia itaongeza athari yake katika suala la Mashariki ya Kati. Kwa upande wa Iraq, Russia ikiwa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama itafanya kazi kubwa katika ukarabati wa kisiasa na uchumi wa Iraq baada ya vita. Hususan mara hii Russia kuamua kuisamehe Iraq deni kwa kiasi kikubwa, kumeweka msingi wa ushirikiano wa siku za usoni. Kutokana na maslahi ya nchi zao, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaimarishwa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-09
|