Msemaji wa Ikulu ya Marekani Bw. Scott McClellan juzi alitangaza kuwa, rais Bush ameamua kumteua tena waziri wa fedha wa sasa Bw. John Snow kuwa waziri wa fedha katika baraza jipya la mawaziri, na Bw. Snow pia amekubali. Hivi karibuni rais Bush amekuwa akijishughulisha na kuunda kundi la kiuchumi kwa kipindi chake cha pili cha urais. Maofisa wa Ikulu na vyombo vya habari vya Marekani vyote vinakisia kuwa mtu mwingine atashika nafasi ya Bw. Snow. Hivyo, uamuzi huo wa Ikulu ya Marekani kweli umewashangaza watu wengi. Kwa nini rais Bush anataka Bw. Snow aendelee na kazi yake?
Mwezi Februari mwaka 2003 Bw. Snow alichukua cheo cha waziri wa fedha wa Marekani badala ya Bw. Paul H. O'Neill. Lakini tangu Bush achaguliwe tena kuwa rais, maisha ya kisiasa ya Bw. Snow hayaonekani wazi. Wiki mbili zilizopita, ofisa wa Ikulu ya Marekani alidokeza kuwa, Bw. Snow huenda ataendelea na kazi yake, lakini muda hautakuwa mrefu. Baada ya hapo, maofisa wa Ikulu ya Marekani walikuwa wakidokeza kuwa mtu mwingine anaweza kuchukua nafasi ya Bw. Snow. Vyombo vya habari vilikuwa na mazungumzo mengi. Baadhi ya vyombo vya habari vilikisia kuwa, mkurugenzi wa ofisi ya Ikulu Bw. Andrew Card atakuwa waziri wa fedha, na watu kadhaa walipendekeza kumteua mbunge wa jimbo la Texas Bw. Phil Gramm kuwa waziri wa fedha. Maofisa wa Ikulu walijibu kuwa, mtu atakayekuwa waziri wa fedha hatakuwa mtu anayepingwa na watu wengine. Maneno hayo yaliwafanya watu kuamini kuwa, Bw. Snow hatashika cheo chake kwa muda mrefu.
Lakini inaonekana kuwa Ikulu ya Marekani haikutaka kutoa uamuzi haraka. Maofisa wengi waandamizi hawakujua kwa nini Bw. Bush hakutangaza uamuzi wake. Maofisa kadhaa walisema kuwa, hali ya sasa ya uchumi nchini Marekani haikubali ishara isiyo wazi, kutangaza mapema mteuzi wa waziri wa fedha kutatuliza hali ya Wall Street na bunge.
Labda kutokana na sababu hiyo, Ikulu ya Marekani mwishoni iliamua kumteua Bw. Snow. Uamuzi huo unawashangza watu. Wachambuzi wanaona kuwa, si vigumu kuelewa kwa nini rais Bush amechukua uamuzi huo.
Kwanza, rais Bush anataka kuhakikisha mfululizo wa sera za kiuchumi. Wabunge kadhaa wa chama cha Republican wanaona kuwa, kutokana na baadhi ya wabunge kuwa na mashaka kuhusu mageuzi ya sera za kodi na ubinafsishaji wa sehemu fulani ya bima ya jamii, rais Bush anahitaji mtu anayeweza kuwashawishi watu hao ili kutekeleza sera yake. Na Bw. Snow ndiye mtu huyo, kwani anajulikana kuwa ni mtu anayeunga mkono kithabiti sera za kiuchumi za rais Bush.
Pili, watu wengine kadhaa walioteuliwa na rais Bush si watu wanaofaa. Hivi karibuni, thamani ya dola za kimarekani zimepungua kwa kiasi kikubwa, na soko limekuwa na wasiwasi wa msukosuko wa kifedha. Katika hali hiyo, mbunge wa zamani wa jimbo la Texas Bw. Phil Gramm ambaye anajulikana kuwa husema "kinaganaga", si chaguo linalofaa kutuliza hali ya soko la fedha za kigeni. Ingawa pia wataalamu wa usimamizi wa Wall Street wangeweza kuteuliwa, lakini wachambuzi wanaona kuwa, wengi wao wana mashaka kuhusu pengo kubwa la fedha linaloongezeka la serikali ya Bush. Bila shaka maoni hayo yanakwenda kinyume na mapendekezo ya kiuchumi ya rais Bush. Hivyo Bw. Snow akawa chaguo zuri zaidi.
Aidha, rais Bush hahitaji waziri wa fedha awe na maoni mapya na kujitegemea wakati anapobuni sera ya kiuchumi, anataka waziri wa fedha aendelee kuwa "msemaji wa uchumi wa Ikulu ya Marekani". Wataalmu wa uchumi wa Wall Street wanaona kuwa, Bw. Snow anafaa zaidi na msemaji wa mambo ya kiuchumi wa Ikulu ya Marekani kuliko waziri wa fedha anayebuni sera ya kiuchumi. Kutokana na sababu hiyo, Bw. Snow ni chaguo zuri.
Ikulu ya Marekani inapotangaza uamuzi huo haikusema wazi kuwa Bw. Snow ataendelea kufanya kazi kwa muda gani. Bw. Snow pia alisema kupitia msemaji wake kuwa, anaona fahari kubwa kufanya kazi na rais Bush na kumsaidia kutekeleza sera ya kiuchumi.
Wachambuzi wanaona kuwa, Bw. Snow ni mtiifu wa serikali ya Bush kutokana na vitendo vyake alipokuwa waziri wa fedha. Kwa sababu ya kutokuwa na uwezo mkubwa wa kubuni sera ya kiuchumi, uwezo wake wa kuendesha soko pia si mkubwa, na athari yake katika siasa ya kiuchumi itakuwa ndogo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-10
|