Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-13 15:00:31    
Huanglong

cri
Wiki iliyopita tuliwaelezea mandhari nzuri ya sehemu ya Jiuzhaigou ambayo jina hilo Jiuzhai linatokana na vijiji 9 vya kabila la watibet kwenye bonde la mlima. Sehemu hiyo ina mandhari ya kiasili inayowavutia sana watu, hasa maji ya maziwa yenye rangi mbalimbali. Wakati fulani maji hayo huwa ni ya buluu sana, wakati mwingine yanakuwa ya kijani, na baadhi ya wakati rangi ya maji inachanganyika na ya kijamanjano. Rangi za maji zinabadilikabadilika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na majira.

    Msichana wa kabila la watibet Yan Feng ambaye ameishi katika sehemu ya Jiuzhaigou tokea alipozaliwa alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, maji ya sehemu ya Jiuzhaigou ni ya ajabu sana, na rangi mbalimbali zinatokana na sababu mbalimbali.

    Sababu ya kwanza ni kuwa, ndani ya maziwa kuna aina tofauti zaidi ya 200 za mimea. Rangi za mimea hiyo zinatofautiana, hivyo maji ya ziwa huonekana kuwa na rangi tofauti; pili ni kutokana na mionzi ya jua. Jua linapochomoza, ukisimama kwenye pembe tofauti kwa wakati tofauti katika sehemu tofauti, unaweza kuona rangi ya maji ikibalikabalika. Zaidi ya hayo, kutokana na vitu mbalimbali vya kikemikali ndani ya maji ya sehemu ya Jiuzhaigou, hivyo maji yanaweza kubadilika kikemikali.

    Msichana Yan Feng alisema kuwa, watu wakifanya utalii katika sehemu ya Jiuzhaigou siku zenye jua, wanatazama maji, siku zisizo na jua wanatazama milima, na baada ya mvua wanatazama mawingu na ukungu. Kweli milima mirefu yenye vilele ambavyo vimefunikwa kwa theluji majira yote inapendeza sana. Katika ya milima na mabonde kuna miti mbalimbali yenye rangi nyekundu, manjano na kijani. Kama siku zisizo na jua, mawingu na ukungu vinaelea kwenye milima na kuonekana kama picha nzuri. Wakati fulani, baada ya mvua, jua likitokea tena, upinde wa rangi mbalimbali unaweza kuonekana katikati ya milima, na ndani ya maji, ambapo watu wakitembea bondeni, wataona kama wako kwenye ndoto wakitembea peponi.

    Ukipanda gari kutoka sehemu ya Jiuazhaigou kuelekea kusini utafika sehemu ya Huanglong baada ya saa tatu. Sehemu hiyo pia ni urithi wa maumbile ya ajabu. Katika bonde hilo lenye misitu ya kiasili, bonde la mteremko lenye urefu wa mita zaidi ya 300 linaonekana kama dragon mmoja mwenye rangi ya dhahabu anayetambaa ndani ya misitu na milima ya mawe na vilele vyenye theluji. Kwenye ardhi ya bonde, maji ya theluji ya milima mirefu inatiririka kutoka juu na kuunda kuwa mabwawa mengi ya rangi.

    Mtalii mmoja wa Shanghai Bibi Xu Xiaowei alisema kuwa, mabwawa zaidi ya elfu moja ya sehemu ya Huanglong yana rangi ya kimanjano, kijani, na kibuluu, na yanapendeza sana.

    Baada ya kutembelea sehemu za Jiuazhaigou na Huanglong, watalii wanaweza kuishi kwa siku mbili hivi katika mji mdogo wa Wilaya ya Sonpan ambapo upo uwanja wa ndege wa Jiuhuang. Mji huo mdogo una historia ya miaka zaidi ya 1300. Kwenye mji huo nyumba nyingi ni zenye kimo kifupi, kuna vichochoro vingi na madaraja mengi ya kale. Mitaani watu wa makabila mbalimbali wanafanya biashara ndogo za kuuza mazao ya misituni, chai, chumvi na vitambaa. Ingawa miaka mingi imepita, mji huo mdogo bado unaonekana na hali ya kiasili yenye mtindo pekee ambayo inawafanya watu wang'ang'anie huko hata hawataki kuondoka.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-13