Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-14 15:36:57    
Barua 1214

cri
    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyang Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema anapenda kutuma fursa hii kutushukuru sana kwa juhudi kubwa tunazozifanya kwa ajili ya kuwahudumia vyema wasikilizaji wetu kwa kuwatangazia vipindi maalum na habari motomoto katika idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema vipindi kama vile Sanduku la barua, Daraja la urafiki kati ya China na Afrika, Klabu ya utamaduni, Tazama China, Elimu na afya, Wapenzi wa michezo, kwa kweli vipindi hivyo ambavyo siku zote hutanguliwa na taarifa ya habari na maelezo baada ya habari vinawapatia ujuzi na maarifa mengi kuhusu taifa la China na ulimwengu mzima.

    Anasema anapenda kutuambia kuwa katika kipindi cha sanduku la barua cha tarehe 12 mwezi Septemba mwaka huu wa 2004, pamoja na mambo mengine mtangazaji aliweza kunukuu barua yake aliyokuwa ametutumia siku za nyuma. Hakika alifurahi sana kwa kuwa hii inawatia moyo sana wasikilizaji wetu na kuzidi kuwa tayari kutoa michango mbalimbali ya maoni na ushauri na kuiwasilisha kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema yeye akiwa ni msikilizaji wa siku nyingi wa Radio China kimataifa, anaahidi kuendelea kuwa msikilizaji mwaminifu na kushiriki kikamilifu kusikiliza na kushiriki katika chemsha bongo ya mashindano ya ujuzi yanayotolewa na kuandaliwa na Radio China kimataifa takribani kila mwaka.

    Anasema katika mwaka huu wa 2004 ambapo Radio China kimataifa imeandaa mashindano ya ujuzi kuhusu miaka 55 ya kuasisiwa kwa China mpya. Anasema, yeye na wasikilizaji wengine wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, wataiunga mkono sana Radio China kimataifa, serikali ya China na wananchi wote wa Jamhuri ya watu wa China na hivyo taifa kuzidi kuwa na umoja na mshikamano.

    Bwana Kulwa pia anasema anapenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zake za dhati kwa ajili ya vipindi vya jumapili ya tarehe 26 mwezi Septemba mwaka huu wa 2004 ambapo siku hiyo katika kipindi cha "Sanduku la barua" kabla ya kurudia kutangaza makala ya kwanza ya mashindano ya chemsha bongo kuhusu miaka 55 ya China mpya, na katika kipindi hicho tulinukuu na kutangaza barua yake aliyokuwa ametuandikia akiwa huko Dar es Salaam, barua hiyo ilikuwa na mapendekezo kadhaa yanayohusu kuboresha zaidi vipindi vyetu, na hasa juu ya mashindano ya ujuzi ambayo yamekuwa yakiandaliwa na Radio China kimataifa karibu kila mwaka.

    Anasema amefurahishwa sana na majibu yaliyotolewa na mtangazaji wa kipindi hicho mama Chen ambapo akishirikiana na ndugu Fadhili Mpunji kutoa ufafanuzi mzuri kuhusu mashindano hayo. Siku hiyo Mama Chen alisistiza kuwa siku zote wapo tayari na wako mstari wa mbele kabisa katika kutetea na kusaidia wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa wapate ushindi mkubwa.

    Anasema, hakika kauli na maelezo hayo yamewatia moyo sana na wataendelea na juhudi kubwa kushiriki katika mashindano hayo ya chemsha bongo kila yanapoandaliwa. Yeye angependa sana kuona na kusikia kuwa kila mwaka au walau kila baada ya miaka miwili msikilizaji mmoja kutoka idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa anapata ushindi mkubwa na kualikwa kuitembelea China. Hii ni kutokana na ukweli kwamba lugha ya Kiswahili ni lugha kubwa kabisa inayozungumzwa na watu zaidi ya milioni 100 katika nchi za Afrika mashariki na eneo la maziwa makuu kwa ujumla.

    Anasema kuwa kuna vyuo vikuu zaidi ya 20 duniani vyenye vitivo vinavyofundisha lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu vyao. Kuna marais wa nchi zaidi ya 25 barani Afrika wanaoweza kuzungumza na kuongea Kiswahili safi na sanifu, baadhi ya marais hao ni Joachim Chissano wa msumbiji Rais Levy Mwanawasa wa Zambia, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Benjamin Mkapa wa Tanzania, Rais Amani Karume wa serikali ya mapinduzi Zanzibar, rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Rais Paul Kagame wa Rwanda, na rais Olunsegun Obasanjo wa Nigeria kwa kutaja wachache tu.

   Pia anasema kuna stesheni za Radio na televisheni nyingi duniani zinazotumia Kiswahili kwa mfano, Radio China kimataifa CRI, Radio ya Japan NHK, Radio India, , Pakistan-Radio Pakistan, Radio Iran, Saudi Arabia-Radio Jeddah, German-DW, Uingereza-BBC, Italia-Vatican Radio ambapo pia mkuu wa Vatican-Papa John Paul wa pili alipoitembelea Tanzania alitumia Kiswahili katika mahubiri na hotuba zake mwaka 1990.

    Stesheni nyingine ni kama vile Sauti ya Amerika-VOA, Channel Afrika, Radio Comoro, Kenya-KBC, Radio Uganda, Radio Cairo, Radio Rwanda, Radio Tanzania Dar es Salaam, Sauti ya Tanzania-Zanzibar na baadhi ya vituo vya televisheni vinatumia lugha ya kiswahili. Hivi sana Kiswahili ni lugha rasmi inayotumika katika vikao mbalimbali vya muungano wa mataifa ya Afrika. Hivyo ni lugha ya kimataifa.

    Anasema siku za baadaye atatuletea mchanganuo ulio mzuri zaidi ili kutusaidia wakuu wa CRI kuelewa kuwa Kiswahili ni lugha inayostawi na kukua kwa kasi na kina hadhi ya kimataifa.