Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-14 21:24:30    
Sekta ya uzalishaji wa magari imejiandaa vizuri dhidi ya usafirishaji wa magari wa nchi za nje

cri

    Mwaka 2005 hautakuwa wa kawaida kwa sekta ya uzalishaji wa magari ya China. Kwani, kutokea tarehe 1 mwezi Januari mwaka kesho, China itaondoa kiwango cha usafirishaji wa magari wa nchi za nje, usimamizi wa leseni na kupunguza zaidi ushuru wa forodha wa magari. Hatua hiyo inamaanisha kuwa magari na vipuri vya magari kutoka nchi za nje vitaingia nchini China kwa urahisi zaidi. Kutokana na kukabiliwa na hali hiyo, sekta ya uzalishaji wa magari ya China itafanya nini? Basi leo nimekuandalia hayo katika kipindi hiki cha nchi yetu mbioni.

    Machoni pa watu wengi, sekta ya uzalishaji wa magari ya China ni dhaifu, lakini mtaalamu mmoja wa sekta ya magari ya China, ambaye ni naibu mkuu wa shiriikisho na viwanda vya uzalishaji wa magari la China, Bw. Zhang Xiaoyu alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa sekta ya magari ya China siyo dhaifu kama watu wengi wanavyofikiria, wala haitadidimia baada ya makampuni makubwa ya kimataifa ya magari kuingia nchini. Alisema,

    "Katika miaka mitatu iliyopita haikutokea hali ya kusambaratika kwa sekta ya uzalishaji wa magari ya China , baada ya China kujiunga na Shirika la Biashara Duniani WTO, bali kinyume chake ni kuwa pamoja na kuimarika kwa nguvu ya ushindani ya China, bei za magari, hususan za magari madogo zimekaribia kwa haraka bei za magari za soko la kimataifa, tena bei zake zitapungua zaidi."

    Bwana Zhang anaona kuwa maendeleo ya mfululizo ya uchumi na uwezo mkubwa wa soko la magari la China ni nguvu inayohimiza maendeleo ya sekta ya magari ya China. Pamoja na kuongezeka kwa mapato ya wakazi wa mijini na vijijini, watu wa China wamekuwa na shauku kubwa ya kununua magari.

    Dada Dai Zhenzhen amefanya kazi kwa miaka miwili katika kampuni moja ya matangazo ya biashara baada ya kumaliza masomo yake. Hivi karibuni alinunua gari lenye thamani ya Yuan za Renminbi laki moja. Dada huyu alisema kuwa baada ya kununua gari, anaona ni rahisi sana katika kufanya shugnuli zake, na anaona watu wengi anaowafahamu wamenunua magari pia.

    Sasa inakaribia miaka 50 tangu China itengeneze gari la kwanza mwaka 1956, ambapo sekta ya uzalishaji wa magari ya China imeimarika mwaka hadi mwaka. Hivi sasa baadhi ya viwanda vya uzalishaji wa magari vya China vimeimarika na vimesimama imara katika masoko ya magari yenye ushindani mkali. Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003, idadi ya magari nchini China ilifikia zaidi ya milioni 24, na karibu nafasi zote za soko la magari la China zimechukuliwa na viwanda vya magari vya China.

    Kutokana na msingi mzuri kama huu, viwanda vingi vya magari vya China havina wasiwasi juu ya mwaka 2005. Katika miji muhimu inayozalisha magari ikiwemo Shanghai na Changchun, viwanda vya magari vinaendelea kuzalisha magari na kufanya utafiti wa magari ya aina mpya, isipokuwa vinaharakisha hatua zake za kuzalisha aina mpya za magari. Kampuni ya magari ya Geely ni kampuni binafsi, hivi karibuni ilianza kuzalisha aina ya gari linalopendwa na familia yenye pato la chini ya kiwango cha wastani, ambalo bei yake ni pungufu ya Yuan elfu 30. Magari ya aina mpya ya Chery na Changan pia yameanza kuzalishwa katika viwanda. Kampuni ya magari ya Shanghai sasa inaharakisha hatua zake katika kufanya utafiti wa kuzalisha magari yanayotumia aina mpya ya nishati, muda mfupi baada ya kampuni ya magari ya Shanghai kutangaza kuonesha magari yanayotumia betri, kampuni ya magari ya Changchu ilitangaza kuwa itazalisha magari yanayotumia nishati za aina mbili za betri na petroli mwaka kesho kwa kushirikiana na kampuni ya magari ya Toyota. Meneja mkuu wa kampuni ya magari ya "Changchun Bw. Zhu Yanfeng alisema,

    "Kuhusu magari yanayoweza kutumia nishati za aina mbili, hivi sasa tunafanya uchunguzi kuhusu mahitaji ya soko la magari hayo, na matayarisho ya kiteknolojia, magari yatazalishwa kwa wingi katika mwaka 2006, na yatazalishwa kwa majaribio katika mwaka 2004.

    Kutokana na mambo hayo, tunaweza kuona pia matatizo yaliyoko katika sekta ya uzalishaji wa magari ya China, ambayo ni pamoja na nguvu dhaifu ya kiteknolojia, aina za chache za magari yanayosanifiwa na China peke, na magari yaliyosanifiwa na China yenyewe na yanayochukua nafasi kubwa katika soko la magari la nchini ni ya kiwando cha wastani au cha chini. Kwa hiyo viwanda vingi vya China vinachagua njia ya kufanya ushirikiano na kampuni kubwa za magari za nchi za nje vikitaka kuimarisha nguvu zake kwa kujifunza teknolojia na uzoefu wa kisasa.

    Wataalamu wanachambua kuwa moja ya mabadiliko mapya katika seta ya magari ya China katika siku za baadaye ni kufanya ubia na ushirikiano na kampuni za nchi za nje. Hivi karibuni kampuni ya magari ya Daimler Chrysler ya Ujerumani iliamua kujenga kiwanda kipya kwa ubia na kampuni ya magari ya Beijing na kuzalisha magari ya Benz katika kipindi cha ushirikiano cha miaka 30. Naibu kiongozi wa taasisi ya nchini inayofanya utafiti kuhusu kampuni za kimataifa, Bw. Zhang Xiaoyu alisema kuwa baadhi ya kampuni za kimataifa zimegundua kuwa katika siku za usoni soko la magari la China litahitaji malori makubwa na magari ya kilimo. Alisema,

    "Kadiri uchumi wa China unavyokuzwa, mahitaji ya magari hususan magari ya kilimo yatakuwa makubwa, na yatachukua nafasi kubwa katika soko la magari. Ninajua, hivi sasa kampuni za kimataifa zimelenga shabaha ya soko hilo na zinajiandaa kuingia katika soko hilo hatua kwa hatua."

    Naibu mkurugenzi wa kamati ya wataalamu wa shirikisho la viwanda vya magari la China Bw. Rong Huikang anaona kuwa licha ya kufanya ubia, kampuni za magari za nchi za nje pia zinataka kuinua kiwango cha usafirishaji wa magari yao kwa China kwa kutumia nafasi ya China kuondoa leseni za uagizaji wa magari ya nchi za nje, hali ambayo italeta pigo kwa sekta ya uzalishaji wa magari ya China..

    Hivi sasa baadhi ya viwanda vya magari vya China vinaharakisha kufanya ubia na ushirikiano na kampuni kubwa za magari ya nchi za nje, wakati vinapoimarisha nguvu ya ushindani, vinalenga shabaha masoko mapya ya magari ya nchi za Ulaya ya Mashariki.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-14