Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-15 14:53:08    
Kwa nini serikali ya Bush inapinga Baradei asichaguliwe tena kuwa katibu mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani?

cri
    Hivi karibuni serikali ya Bush imeeleza waziwazi mara kwa mara kuwa inapinga Bw Mohamed el Baradei kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa Shirika la nishati ya atomiki duniani IAEA mwaka kesho atakapomaliza muda wa madaraka yake ya awamu ya pili, na tena serikali ya Marekani imechukua hatua mbalimbali. Ni kwa nini Marekani inapinga kuchaguliwa tena kwa Bw Baradei?

    Kutokana na ufafanuzi wa msemaji wa Ikulu ya Marekani Bwana McClellan, sababu ya serikali ya Bush kupinga Bw Baradei kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa shirika la ni kuwa, nchi mbalimbali zinazohusika zimefikia kauli moja kuhusu muda wa madaraka ya kiongozi wa shirika hilo, yaani kiongozi wa shirika hilo anaweza tu kushika wadhifa huo kwa awamu mbili mfululizo. Na hali kadhalika kwa wakuu wa Umoja wa Mataifa au mashirika mengine makubwa ya kimataifa. Lakini wachambuzi wanaona kuwa, hiki ni kisingizio tu, sababu ya kikweli ya Marekani kupinga Bw Baradei kuchaguliwa tena kuwa katibu mkuu wa IAEA ni kutokana na kuwa Baradei hakufuata matakwa ya Marekani aliposhughulikia masuala ya Iraq, nyuklia nchini Iran na mengine kadhaa.

    Kabla ya kuanzisha vita dhidi ya Iraq mwaka 2003, Marekani siku zote ilidai kuwa Iraq ilikuwa na silaha za viumbe na kemikali na ilianzisha tena mpango wake wa silaha za nyuklia. Lakini Shirika la IAEA linaloongozwa na Baradei lilipinga maoni hayo ya Marekani, shirika hilo lilikwenda Iraq kufanya ukaguzi mara kwa mara, baadaye lilitangaza kuwa halikugundua ushahidi kuhusu Iraq kurudisha mpango wake wa silaha za nyuklia. Bwana Baradei pia alieleza mashaka yake kuhusu Marekani na Uingereza kuilaani Iraq kununua uranium kutoka Niger, alisema kuwa uchunguzi umeonesha kuwa nyaraka husika ni za uwongo. Baada ya vita vya Iraq Marekani haikuweza kupata ushahidi wowote kuhusu Iraq kufufua mpango wake wa silaha za nyuklia, na Bw Baradei aliwahi kueleza kuwa ukweli wa mambo umeonesha kuwa aliyosema ni ya sahihi. Serikali ya Bush ilikasirishwa sana na kitendo hicho.

       Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Marekani siku zote inaona kuwa Iran ni kikwazo kwa Marekani kutembeza mikakati yake katika eneo la mashariki ya kati, hivyo Marekani inashikilia kuichukulia hatua kithabiti. Lakini Bwana Baradei anashikilia kanuni za kufuata hali halisi na alishirikiana na nchi muhimu za Ulaya na nyingine duniani kutetea kutatua suala la nyuklia la Iraq kwa kupitia mazungumzo, na mwishowe kufikia makubaliano na Iran, na Marekani ikashindwa kulifikisha suala hilo kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Maofisa wa Marekani mara kwa mara walimkosoa mara kwa mara Bw Baradei kwa kutoweza kuchukua hatua imara dhidi ya Iran, na kumlaani kwa kuficha "ushahidi wa uhalifu" wa Iran kwa shirika la IAEA, na kuharibu juhudi za Marekani za kulifikisha suala hilo kwenye baraza la usalama. Gazeti la Washington Post la Marekani lilidokeza kuwa, maofisa wa serikali ya Bush walisikiliza kwa siri mazungumzo ya mara kumi kadhaa kwenye simu kati ya Baradei na maofisa wa kidiplomasia wa Iran, kwa lengo la kutafuta ushahidi wa kumwondoa Bw Baradei.

    Aidha, Marekani haifurahii hatua za Baradei kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-15