Mazungumzo hayo ya siku mbili ni sehemu ya mchakato wa mazungumzo unaoanzishwa mwaka huu kati ya India na Pakistan. Ingawa nchi hizi mbili hazijaafikiana kuhusu hatua zitakazochukuliwa ili kupambana pamoja na biashara ya dawa za kulevya, lakini maofisa wa idara za kupambana na dawa za kulevya wa nchi hizo mbili wamebadilishana miswada ya kumbukumbu kuhusu kukubaliana suala hilo. Baada ya mkutano, pande hizo mbili zilitoa taarifa ya pamoja zikisema kuwa, nchi hizo mbili zitashirikiana ili kukabiliana pamoja na suala la biashara ya dawa za kulevya na zitaimarisha mawasiliano na ushirikiano.
Taarifa inaona kuwa mazungumzo hayo ni "ya dhati na yenye maana ya ujenzi". Vyombo vya habari vya India vilinukuu habari kutoka serikali vikisema kuwa, hakuna tofauti kubwa kati ya pande hizo mbili, hivyo nchi hizo mbili zinaweza kufikia makubaliano kuhusu kuimarisha ushirikiano katika kupambana na dawa za kulevya na njia ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, katika taarifa hiyo pande hizo mbili zinaeleza kuwa, zinakubali kufanya mazungumzo ya ngazi ya wakuu ya idara za kupambana na dawa za kulevya za nchi hizo mbili mwezi Juni, mwakani nchini Pakistan na kuendelea kufanya mashauriano kuhusu suala la dawa za kulevya.
India na Pakistan zinakabiliana na suala la biashara ya dawa za kulevya, na nchi hizo mbili zinachukuliwa kuwa ni nchi muhimu za kupitishia dawa za kulevya ya kimataifa. Afghanistan, ambayo ni nchi muhimu inayozalisha dawa za kulevya aina ya kasumba, inazichukulia India na Pakistan kuwa "vituo vya kupitishia" dawa za kulevya kwenda Ulaya na Marekani. Jiografia ya mipaka kati ya Pakistan na Afghanistan ni ya utatanishi, hali ambayo inatoa mwanya kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Kwa mujibu ya ripoti iliyotolewa mwezi Agosti mwaka huu na idara kuu ya upelelezi ya India, kuanzia mwezi Januari hadi Julai, polisi wa New Delhi wa India waligundua kwa mfululizo matukio makubwa ya biashara ya dawa za kulevya. Katika dawa za kulevya zilizokamatwa, thamani ya heroin imefikia rupia zaidi ya bilioni moja.
Mazungumzo ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya kati ya India na Pakistan yalisimamishwa mwaka 1999 kutokana na uhusiano wa mvutano kati ya nchi hizo mbili. Mwanzoni mwa mwaka huu, nchi hizo mbili zilianzisha mchakato wa mazungumzo na kuanza kufanya mazungumzo kuhusu masuala ambayo bado hayajatatuliwa, likiwemo suala la kupambana pamoja na biashara ya dawa za kulevya. Mwezi Juni mwaka huu, maofisa wanaoshughulikia usimamizi wa dawa za kulevya wa nchi hizo mbili walifanya mazungumzo ya kwanza kuhusu suala hilo na kukubali kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika kupambana na dawa za kulevya na biashara, pia walikubali kuchukua hatua ili kuzuia biashara ya heroin kati ya nchi hizo mbili.
Kuanzia mwezi Desemba India na Pakistan zitaanza kufanya mazungumzo ya kipindi cha pili kuhusu masuala yaliyopo kati ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo kuhusu kupambana na dawa za kulevya ni sehemu ya mchakato wa duru la pili la mazungumzo. Wachambuzi wanaona kuwa, nchi hizo mbili zimeelewa kwamba ni lazima zishirikiane ili ziweze kukomesha biashara ya dawa za kulevya kati ya nchi zao. Inaaminika kuwa kutokana na mazungumzo kati ya nchi hizo mbili kuendelea, na pande hizo mbili kuzidisha kuelewana na kuaminiana, ushirikiano kati yao utaimarishwa.
Idhaa ya kiswahili 2004-12-15
|