Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-15 20:26:41    
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zakubaliana kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji katika maeneo yao

cri
    Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zimehakikishiana kulinda, kutunza na kuheshimu haki za wafanyakazi wahamiaji katika maeneo yao.

    Maafikiano hayo yalifikiwa jana na wawakilishi kutoka nchi hizo za Tanzania, Kenya na Uganda, wakati wa uzinduzi wa mradi wa Shirika la Kazi Duniani ILO wa uhuru wa uhamaji wa wafanyakazi kutoka nchi moja hadi nyingine katika Afrika Mashariki bila vikwazo.

    Azma ya lengo hilo ni kufanikisha majukumu yao hasa ya kiuchumi kwa faida ya nchi zote husika.

    Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana na Michezo wa Tanzania, Profesa Juma Kapuya ndiye aliyezindua mradi huo, unaofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).

    Wawakilishi hao, pamoja na Profesa Kapuya ni Waziri wa nchi anayeshughulikia masuala ya Kazi na Viwanda wa Uganda, Bw. Henry Obbo na Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Wafanyakazi wa Kenya, Bw. Newton Kulundu.

    Mawaziri hao, kila moja kwa wakati wake walisisitiza suala la kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji katika maeneo hayo kama njia ya kutekeleza mradi huo.

    Waziri Kulundu alisema serikali husika hazina budi kushirikiana ipasavyo na kuhakikisha wafanyakazi hao hawanyonywi katika nchi wanazofanyia kazi, kubaguliwa na wala kuonewa.

    Alisema, kwa kufanya hivyo, wataweza kutekeleza majukumu yao kwa faida ya nchi wanazotoka wanakofanyia kazi.

    Alisisitiza kuwa ni kwa kufanya kazi katika mazingira ya amani, mfanyakazi mhamiaji anaweza kujenga uhusiano mzuri kati ya nchi yake na ile aliyopo na hivyo kuufanya mradi huo ufanyekazi kama ulivyokusudiwa.

    Pia, alizungumzia suala la wafanyakazi wakimbizi na kusema ni lazima serikali zote tatu zihakikishe wanafuata sheria, kanuni na taratibu katika nchi wanazokuwapo.

    Lengo ni kuhakikisha mradi huu hautumiwi kama mwanya wakutenda maovu, hili ni kwa wote hata wasio wakimbizi.

    "Pamoja na uhuru huu wa kuhama wafanyakazi, ulinzi na usalama wa nchi zote lazima udumishwe,"alisema waziri huyo wa Kenya.

    Naye waziri wa Uganda, Bw. Obbo alisema nchi husika hazina budi kuhakikisha zinaweka na kutekeleza mikakati itakayosaidia uchumi wa nchi zao kukua hasa kupitia mpango huu.

    Alisema, kama ilivyo katika nchi yake, suala la umasikini limetanda sehemu zote kiasi cha kuhitaji ufumbuzi wa kina ambao kwa upande wake aliona kuwa kazi hiyo ni moja wapo.

    Alisema, kwakuwa wameafiki mradi huo kwa kuona unamanufaa, nchi yake itahakikisha wafanyakazi watakao hamia Uganda wanapata haki zote wanazo stahili kama njia ya kuwawezesha kufanya kazi kwa uhuru na haki, na hivyo kushinda vita dhidi ya umasikini.

    Kwa mujibu wa ILO, mradi huu utanufaisha nchi watokazo wafanyakazi wahamiaji na zile wanazo hamia kiuchumi na kimaendeleo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-15