Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-16 15:50:49    
India na Pakistan zaanzisha "namba ya simu maalum kuhusu nyuklia"

cri

    Mazungumzo ya siku mbili kuhusu hatua za kujenga uaminifu wa nyuklia kati ya India na Pakistan jana yalimalizika huko Islamabad, mji mkuu wa Pakistan. Nchi hizo mbili zimekubali kuanzisha "namba ya simu maalum kuhusu suala la nyuklia" kati ya wizara za mambo ya nje za nchi hizo mapema iwezekanavyo.

    Baada ya mazungumzo kumalizika, nchi hizo mbili zilitoa taarifa ya pamoja zikisema kuwa, mazungumzo hayo ni yenye maana ya kiujenzi. Taarifa hiyo pia inasema kuwa pande hizi mbili zimejadiliana na kushauriana kwa kina na zimepata maendeleo kuhusu hatua za kupunguza hatari ya nyuklia. Pande hizo mbili zimekubali kuanzisha "namba ya simu maalum kuhusu suala la nyuklia" kati ya wizara za mambo ya nje za nchi hizo mbili, ambayo itawaunganisha moja kwa moja makatibu wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili. Aidha, pande hizo mbili zimepata maendeleo kuhusu makubaliano ya "kuarifiana majaribio ya makombora".

    Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mazungumzo hayo, mwakilishi wa Pakistan Bw. Tariq Osman Hyder alisema kuwa kwa kweli India na Pakistan ziliarifiana kabla ya kuanza majaribio ya makombora, sasa jambo ambalo pande hizo mbili zinahitaji kulifanya ni kuhakikisha kitendo hicho kwa njia ya makubaliano. Alisema kwamba India na Pakistan zitaendelea kufanya mazungumzo ili kufikia makubaliano mapema iwezekanavyo. Mwakilishi wa India Bw. Meera Shankar alisema kuwa, kusaini makubaliano kama hayo kunahusika na masuala mengi, hivyo pande hizo mbili lazima zifikiri zaidi.

    Wakati wa kufanya mazungumzo hayo, jana nchi hizo mbili pia zilifanya mazungumzo kuhusu silaha za kawaida mjini Islamabad ili kujenga mfumo wa kuaminiana katika nyanja za silaha za kawaida na kuepusha kuongezeka kwa hatari mapambano ya kijeshi kutokana na kutoelewana. Bw. Hyder alisema kuwa, pande hizo mbili zinatumai kutimiza amani na usalama na kujenga uhusiano wenye utulivu kati ya nchi zao mapema.

    Baada ya mazungumzo kuhusu silaha za kawaida, wawakilishi wa India na Pakistan walieleza kuwa wataendelea kufanya mazungumzo kuhusu hatua za kujenga uaminifu katika nyanja za silaha za nyuklia na silaha za kawaida ili kuepusha kuzuka vita kutokana na kutoelewana.

    Katika mwezi Mei, mwaka 1998, India na Pakistan zilifanya majaribio ya makombora ya nyuklia na kupata mafanikio, hivyo kwa kweli zimekuwa "nchi zenye nyuklia". Jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi kwamba, hali hiyo inaweza kusababisha balaa kubwa.

    Mazungumzo hayo ni ya pili kwa nchi hizo mbili kuzungumza kuhusu suala la nyuklia baada ya kuanzisha mchakato wa mazungumzo mwezi Februari mwaka huu. Mwezi Juni, mwaka huu, wawakilishi wa nchi hizo mbili walibadilishana maoni kuhusu usalama na sera za nyuklia na kutoa taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo kumalizika. Taarifa hiyo inasema kuwa, nchi hizo mbili zinakubali kusimamisha kwa muda majaribio ya nyuklia isipokuwa kama likitokea "tukio maalum" linalohatarisha mamlaka ya nchi. Pande hizo mbili pia zimekubali kuendelea kuboresha njia ya mawasiliano kati ya makamanda wa nchi hizo mbili na mfumo wa kukutana kwa wakati unaopangwa.

    Kufuatana na mpango, tarehe 27 na 28, mwezi huu, makatibu wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili watafanya mazungumzo mjini Islamabad ili kukumbusha maendeleo yatakayopata kutokana na mazungumzo hayo na kuthibitisha wakati na mahala pa kufanya mazungumzo yajayo.

    Wachambuzi wanaona kwamba, ingawa safari hii India na Pakistan hazijasaini makubaliano ya "kuarifiana majaribio ya makombora", lakini dhati iliyooneshwa na pande hizo mbili katika mazungumzo itasaidia kuongeza uaminifu kati ya nchi hizo mbili, pia itasaidia kulinda usalama wa eneo la Asia ya kusini. Hususan mawasiliano yaliyofanywa na pande hizo mbili kuhusu suala la usalama wa nyuklia yatasaidia nchi hizo mbili "zenye nyuklia" kuepusha kwa uhalisi vita ya nyuklia.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-16