Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-16 19:06:07    
Mtibet anayeendesha hoteli karibu na hekalu la Laboleng

cri

    Katika wilaya ya Xiahe ya mkoa wa Gansu, kaskazini magharibi mwa China, kuna hekalu maarufu sana la dini ya buddha ya kitibet?Hekalu la Laboleng. Mandhari nzuri ya kimaumbile na utamaduni wa buddha wa kitibet wa sehemu hiyo unawavutia watalii wengi kutoka nchi za nje. Na watalii wa ng'ambo huwa wanachagua kukaa katika hoteli ya Huaqiao kutokana na matangazo yaliyopo kwenye kitabu kiitwacho "Safari Nchini China" kilichoandikwa na mgeni.

    Mwendeshaji wa hoteli ya Huaqiao mwenye umri wa miaka 40 hivi mwaka huu anaitwa Zirenrosan, ni wa kabila la watibet mwenye uraia wa Nepal. Hoteli ya Huaqiao iliyoendeshwa na Zirenrosan iko kwenye mtaa uliostawi sana katika wilaya ya Xiahe, umbali wa mita 500 tu kutoka Hekalu la Laboleng. Hoteli hiyo inawafaa sana watalii wageni wanaotoka nchi za nje, hasa watalii wanaojitegemea. Kwenye ubao wa hoteli hiyo kuna maelekezo kwa lugha ya Kiingereza na Kichina kuhusu huduma za aina mbalimbali zinazotolewa na hoteli hiyo, kama vile kukodisha baiskeli, kufua nguo, kutumia mtandao wa internet, na kulipia huduma ya waongozaji wa utalii.

    Mwandishi wa habari alipoingia katika hoteli hiyo aliwakuta watalii wengi wa ng'ambo wakiwa wanapata kifungua kinywa, ambao wanatoka sehemu mbalimbali duniani.

    "'Mimi natoka Australia', 'Natoka Marekani', 'Mimi natoka Ubelgiji'. Tunaifahamu hoteli hii kupitia kitabu cha 'Safari Nchini China'. Kwa kweli hoteli hiyo inatoa huduma nzuri sana, na chakula pia ni kizuri."

    Jambo linalowavutia zaidi watalii wageni ni kwamba, watumishi wa hoteli hiyo wote wanajua lugha tatu za Kichina, Kiingereza na Kitibet, hivyo hakuna kipingamizi chochote cha mawasiliano.

    Mwendeshaji wa hoteli hiyo Bwana Zirenrosan alisema kuwa, hoteli hiyo ilianzishwa na baba yake Bwana Ganjiarosan aliyerudi nchini China kutoka Nepal. Ganjiarosan alizaliwa katika wilaya ya Xiahe na kuishi Nepal, alikuwa anafanya biashara ya vitambaa kati ya mji wa Chengdu, mji wa Lhasa na India. Baada ya kukusanya mtaji wa kutosha, aliamua kurudi kwenye maskani yake ili kutoa mchango wake kwa maendeleo ya maskani yake.

    "Baba yangu alikuwa mtu wa kwanza wa kabila la watibet aliyerudi kutoka nje katika wilaya ya Xiahe. Kwa kuwa serikali ya wilaya ilimpa ardhi nzuri, hivyo baba yangu aliamua kuanzisha hoteli ili kuwapokea wageni waliotoka nchi za nje."

    Bwana Ganjiarosan alianzisha hoteli ya Huaqiao karibu na Hekalu la Laboleng mwaka 1981. Wakati ule, sekta ya utalii nchini China ilikuwa bado iko nyuma, hivyo biashara ya hoteli ya Huaqiao haikuweza kuwa nzuri, lakini Bwana Ganjiarosan hakukata tamaa, akaacha maisha yake ya huko Nepal, na kupata uraia wa China.

    Mwaka 1993, mzee Ganjiarosan alifariki dunia, Zirenrosan alirithi biashara ya baba yake na kuendelea na shughuli za hoteli. Chini ya juhudi zake, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa nchi za nje wanaokuja kuitembelea Hekalu la Laboleng, biashara yake pia imekuwa ikistawi siku hadi siku, na hivi sasa hoteli hiyo inajulikana duniani.

    Bibi Zijiarosan ni Mke wa Zirenrosan, yeye ni mnepal, anajua lugha nne za Kiingereza, Kichina, Kitibet, na Kinepal na lahaja mbili za kihindi. Mwandishi wa habari alipomkuta Bi. Zijiarosan aliyevaa nguo za kimila za Nepal, alikuwa anazungumza na wageni wake kwa Kiingereza. Alisema anamwunga mkono mume wake kuendeleza biashara yake nchini China, yeye mwenyewe pia anapenda kuishi nchini China. Alisema:

    "Nafikiri mume wangu amefanya vizuri, hoteli yetu ni tofauti na nyingine, tumejitahidi sana katika kuwahudumia vizuri wageni wetu, hivyo tunapata faida. Serikali ya mkoa imetusaidia sana, kila tukikumbwa na tatizo huwa tunapewa misaada."

    Zirenrosan ana watoto wawili, msichana mmoja na mvulana mmoja, wote wanasoma kwenye shule ya kimataifa mjini Chengdu ili wapate elimu ya kichina kuanzia utotoni.

    Familia ya Zirenrosan inafuata maisha rahisi. Kama wakazi wengine wa kabila la watibet, Zirenrosan pia ni mwumini wa dini ya buddha ya Kitibet, kila asubuhi anaamka saa kumi na kufanya sala katika Hekalu la Laboleng. Alisema kuwa, anaishi vizuri na ana uhuru katika mambo ya kidini na kibiashara.

    Mkuu wa idara inayoshughulikia shughuli za wachina wanaorudi kutoka nchi za nje ya wilaya ya Xiahe bwana Sanjieka alisema kuwa, serikali imetoa misaada mingi na sera za kipaumbele kwa wachina wanaorudi kutoka ng'ambo. Chini ya msaada na uungaji mkono wa serikali ya mkoa, Zirenrosan anazingatia kupanua zaidi biashara yake. Siku za usoni, yeye ataendesha hoteli nyingine, na shule ya kiingereza. Anatumai kuwa, kutokana na juhudi zake kazi ya utalii katika wilaya ya Xiahe itapata maendeleo zaidi. Wakati huohuo yeye pia ametoa msaada kwa nyumba ya kuwahudumia wazee, na kila mwaka anatoa kiasi fulani cha fedha kwa Hekalu la Laboleng.

    Kutokana na maendeleo makubwa nchini China, hivi sasa kila mwaka watu wengi wa kabila la watibet waishio nchi za nje wanarudi nchini China ili kutafuta fursa ya kujiendeleza. Bwana Zirenrosan alisema kuwa, hivi sasa matakwa yake makubwa ni kupata uraia wa China, na kuwa mkazi mmoja wa kabila la watibet.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-16