Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-17 15:13:30    
Umoja wa Ulaya waamua kuanzisha mazungumzo na Uturuki kuhusu nchi hiyo kujiunga nao

cri

    Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya uliofanyika jana huko Brussels jana usiku uliamua kuanzisha mazungumzo na Uturuki kuhusu nchi hiyo kujiunga na umoja huo kuanzia tarehe 3 Oktoba mwaka kesho. Wachambuzi wanaona kuwa, uamuzi huo umeonesha kuwa juhudi za Uturuki za kujiunga na Umoja wa Ulaya zimepata matokeo ya kipindi, lakini bado haijaweza kuthibitisha kama imepata ushindi hakika kuhusu suala hilo.

    Waziri mkuu wa Uholanzi ambayo ni nchi mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya Bwana Jan Peter Balkenende alipotangaza uamuzi huo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema kuwa, madhumuni ya mazungumzo hayo ni kuiwezesha Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, lakini kuanzisha mazungumzo hakuwezi kuhakikisha kuwa hatimaye Uturuki inaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya. Mazungumzo ni mchakato unaoweza kusimamishwa wakati wowote.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Ulaya Bwana Jose Manuel Barroso alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa, Umoja wa Ulaya umeifungulia mlango Uturuki, huu ni uamuzi wa kulinganisha maslahi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Uturuki. Anaona kuwa Uturuki ingefurahia kupokea uamuzi huo.

    Ingawa uamuzi huo wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya unamaanisha kuwa juhudi za Uturuki za kujiunga na Umoja wa Ulaya zimepata matokeo ya kipindi, lakini uamuzi huo bado uko mbali na matarajio ya Uturuki. Kwani ingawa kiongozi wa Umoja wa Ulaya amebainisha kuwa madhumuni ya mazungumzo hayo ni hatimaye kuiwezesha Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, lakini Umoja wa Ulaya umesisitiza pia kuwa mazungumzo hayo yataweza kusimamishwa wakati wowote, na kuanzisha mazungumzo hakumaanishi kuwa Uturuki hakika itaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya. Na Uturuki siku zote inapinga maoni hayo. Aidha Umoja wa Ulaya umeamua kuanzisha mazungumzo, lakini umethibitisha mazungumzo hayo yataanzishwa tarehe 3 Oktoba mwakani, na siyo tarehe ya nusu ya kwanza ya mwaka kesho iliyotarajiwa na Uturuki, hii imefuata dhahiri matakwa ya Ufaransa na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya.

    Hivi sasa bado kuna masuala makubwa mawili kwa kuanzisha mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya. La kwanza ni suala la Cyprus. Kutokana na sababu za kihistoria, Cyprus ilifarakanishwa kuwa sehemu mbili za kusini na kaskazini. Kabla ya kupanuliwa kwa Umoja wa Ulaya mwezi Mei mwaka huu, Cyprus ilipiga kura za maoni ya raia kuhusu Cyprus kujiunga na Umoja wa Ulaya ikiwa nchi nzima moja au la. Baada ya kushindwa kwa upigaji kura huo, sehemu ya kusini ya Cyprus imejiunga na Umoja wa Ulaya, lakini sehemu ya kaskazini bado inajitenga. Nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya zimeeleza kuwa, kabla ya kuanzisha mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, Uturuki inapaswa kutambua Jamhuri ya Cyprus ya kusini. Suala la pili ni kuwa, kutokana na kuhofia kuwa idadi kubwa ya watu wa Uturuki huenda italeta shinikizo kubwa kwenye soko la ajira la Umoja wa Ulaya, nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya zimeeleza kuwa, kama Uturuki itajiunga na Umoja wa Ulaya, wafanyakazi wa Uturuki hawataruhusiwa kuingia kwa uhuru kwenye nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kama walivyo raia wa nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya, na lazima kuwazuia daima kwa kuingia kwa wafanyakazi hayo. Namna ya kutatua masuala hayo mawili bado itategemea matokeo ya mashauriano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki.

    Mazungumzo kuhusu Uturuki kuingia Umoja wa Ulaya ni mchakato wa muda mrefu wenye vipengele vinavyobadilikabadilika. Viongozi wa nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaona kuwa, mchakato huo utaendelea kwa muda usiopungua miaka 10.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-17