Bei ya mafuta ya asili ya petroli duniani imekuwa ikipanda kutoka mwanzoni mwa mwaka huu. Hebu tuchukue mfano wa bei ya mafuta ya asili ya petroli katika soko la mafuta ya asili ya Petroli la New York, bei ya mafuta ilifikia dola za kimarekani 48.9 kwa pipa mwezi Novemba kutoka kiasi cha dola 30 kwa pipa mwanzoni mwa mwaka huu, na hata iliwahi kuzidi dola 55 kwa pipa wakati fulani, kiasi ambacho ni cha juu kabisa tangu kuanzishwa kwa soko hilo katika miaka 21 iliyopita, hali hiyo imefuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa.
Wachambuzi wamesema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta, kushindwa kutosheleza mahitaji ya mafuta kwa nyakati zote na ulanguzi wa mafuta. Kwanza, maendeleo ya uchumi wa dunia yanahitaji mafuta ya petroli mengi zaidi, hii ni sababu muhimu inayoifanya bei ya mafuta ipande. Mwaka huu Shirika la Utoaji Mikopo Duniani lilikadiria kwa kiwango cha juu kuhusu ongezeko la uchumi wa nchi mbalimbali, jambo ambalo lilifanya wachambuzi na taasisi nyingi za utafiti wa hali ya mafuta ya asili ya petroli nao walirekebishe kwa kiwango cha juu makadirio waliyofanya kuhusu mahitaji ya mafuta ya petroli ya mwaka 2004, yaani kutoka mapipa milioni 1 hadi milioni 1.2 kwa siku hadi zaidi ya mapipa milioni 2 kwa siku.
Pili, hali yenye wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya nchi muhimu zinazozalisha mafuta, ambayo ilisababisha hali ya kushindwa kutosheleza mahitaji ya mafuta ya petroli duniani kwa nyakati zote, pia ni sababu iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli. Toka mwanzoni mwa mwaka huu, uzalishaji wa mafuta wa jumuiya ya nchi zinazosafirisha nje mafuta ya petroli, OPEC ulitikia kikomo cha uwezo wake na ilishindwa kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta kwa kuongeza utoaji wa mafuta. Saudi Arabia, ambayo ni nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa mafuta, ilitishiwa vibaya na mashambulizi ya kigaidi; wafanyakazi wa mafuta nchini Norway, ambayo ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa utoaji wa mafuta duniani, walifanya mgomo wakidai nyongeza ya mshahara; wafanyakazi wa mafuta nchini Nigeria, ambayo ni ya tano kwa uzalisjaji wa utoaji wa mafuta, walifanya migomo mara nyingi toka mwaka 2002 kutokana na migogoro kati yao na matajiri; mgongano kati ya rais Hugo Chaves wa Venezuela pamoja na wapinzani na Marekani ulikuwa mkali katika baadhi ya nyakati, ambao uliathiri utoaji na usafirishaji nje wa mafuta ya asili ya petroli. Kampuni ya mafuta ya Yokos nchini Russia, ambayo uzalishaji wake wa mafuta unachukua 20% ya utoaji wa mafuta duniani, ilikaribia kufilisika kutokana na kudaiwa kodi ya dola za kimarekani bilioni 3.4; hali mbaya ya usalama nchini Iraq iliathiri sana usafirishaji wa mafuta kwa nchi za nje. Mambo hayo pia yaliharibu utulivu wa bei ya mafuta duniani.
Tatu, shughuli za ulanguzi wa mafuta ya petroli pia zilichangia kupanda kwa bei ya mafuta ya asili ya petroli. Baada ya kuingia mwaka 2004, mashirika ya uwekezaji yenye tabia ya kubahatisha yaliingia kwenye soko la mafuta ya asili ya petroli duniani; isitoshe, kiasi cha ubadilishaji kati ya dola za kimarekani na Euro kilishuka kwa mfululizo na kuzidisha shughuli za ulanguzi.
Nne, ni kutokana na sera za Marekani kuhusu mafuta ya asili ya petroli. Marekani ni nchi ya kwanza kwa wingi wa matumizi ya petroli duniani, ambayo karibu kila siku inatumia mafuta ya asili zaidi ya mapipa milioni 20 yakiwa ni robo ya matumizi ya mafuta ya dunia nzima. Aidha, Marekani inaongeza akiba yake ya mafuta ya asili kwa tahadhari ya vita. Katika mwaka uliopita, akiba ya mafuta ya asili ya Marekani iliongezaka na kuzidi mapipa milioni 660 kutoka milioni 580, jambo ambalo lilizidisha mahitaji ya mafuta ya asili duniani. Mbali na hayo, ukoo wa Bush una uhusiano mkubwa na kampuni za petroli nchini Marekani, serikali ya Bush haikuchukua hatua wala kudhibiti upandaji wa bei ya mafuta kwa kutumia akiba ya mafuta ya asili ya nchi hiyo kwa ajili ya kulinda maslahi ya matajiri wakubwa wa petroli wa Marekani. Bei kubwa ya mafuta ya asili ya petroli iliyoendelea kwa muda mrefu bila shaka imeathari vibaya uchumi wa dunia.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-17
|