Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-20 15:15:21    
Mgogoro kati ya Palestina na Israel yaleta wasiwasi wa kufanyika uchaguzi mkuu wa Palestina

cri
    Hivi karibuni, jeshi la Israel na wanamgambo wa Palestina walipambana kwa mfululizo katika sehemu ya kusini mwa Gaza, na tofauti kati ya viongozi wa Palestina na Israel katika masuala makubwa pia zimeonekana wazi, hali hiyo si kama tu imetoa pigo kwa hali ya kufurahisha iliyotokea hivi karibuni, bali pia imeleta hali ya wasiwasi kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina.

    Ili kulipiza kisasi kwa mashambulizi yaliyoanzishwa na wanamgambo wa Palestina, tarehe 16 jeshi la Israel lilianzisha harakati ya kijeshi ya siku mbili katika sehemu ya kusini mwa Gaza, likiwaua wapalestina wasiopungua 11, na kubomoa nyumba 39. Jeshi la Israel lilisema kuwa, lengo lake ni kuwazuia wanamgambo wa Palestina wasiendelee kushambulia shabaha za Israel. Pia lilionya kuwa, ikiwa wanamgambo wa Palestina wataendelea kushambulia vituo vya makazi vya wayahudi, basi jeshi la Israel huenda litaanzisha operesheni kubwa zaidi ya kijeshi dhidi ya wapalestina.

    Vitendo vya jeshi vya Israel vimelaumiwa na serikali ya utawala wa Palestina na kuona kuwa, vitendo vya kijeshi vilivyoanzishwa na jeshi la Israel vimeathiri vibaya maandalizi yaliyofanywa kwa ajili ya uchaguzi wa mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina. Kama uchaguzi mkuu wa Palestina utapaswa kuahirishwa kutokana na vitendo vya Israel, basi serikali ya Israel inapaswa kubeba lawama zote. Ili kuweka mazingira mazuri kwa uchaguzi mkuu, mamlaka ya Palestina hivi karibuni inafanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya wanamgambo ili kuyahimiza yafikie makubaliano ya kusimamisha vita na Israel. Kuzusha tena migogoro ya kijeshi kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Palestina katika sehemu ya kusini mwa Gaza, bila shaka kumeleta changamoto kubwa kwa juhudi zilizofanywa na mamlaka ya Palestina ya kusimamisha vita.

    Isitoshe, msimamo mkali wa waziri mkuu wa Israel Bwana Ariel Sharon kuhusu mswada wa kuanzisha taifa kwa Palestina umeongeza utatanishi katika utatuzi wa tatizo kati ya pande hizo mbili, na sauti ya Palestina ya kushikilia mapambano ya kisilaha dhidi ya Israel imeongezeka. Bwana Sharon tarehe 16 alisema kuwa, ili kuleta amani ya kisehemu, Israel lazima ifuate mpango wa kuchukua vitendo kwa upande mmoja, na kuondoka kutoka sehemu ya Gaza. Lakini alikataa kutambua kuwa, wakimbizi wa Palestina wana haki ya kurudi makwao, pia hakubali kulirudisha jeshi la Israel kwenye mstari wa mpakani uliowekwa kabla ya vita ya tatu vya mashariki ya kati ilivyotokea mwaka 1967. Maneno hayo ya Bw. Sharon yamepingwa na wapalestina. Mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya ukombozi wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas alisema kuwa, watu wa Palestina hawawezi kukubali kushurutishwa na Israel kuhusu hadhi yao ya mwisho, wapalestina kamwe hawataacha msimamo wao katika masuala ya wakimbizi kurudi makwao, hadhi ya Jerusalem, na jeshi la Israel kuondoka kutoka kwenye ardhi zinazokaliwa. Mjumbe mkuu wa mazungumzo wa Palestina Bwana Erakat alisema kuwa, maneno ya Sharon yameonesha kuwa, yeye hana moyo wa dhati kuhusu amani. Vyombo vya habari vya Palestina vinaona kuwa, litakuwa kosa kubwa la kimkakati kwa viongozi wapya wa Palestina kuacha kabisa mapambano ya kisilaha dhidi ya Israel, Palestina haina njia nyingine ila tu kushikilia mapambano ya kimabavu na kufanya mazungumzo ya amani sambamba.

    Vyombo vya habari vinaona kuwa, wakati siku ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Palestina inapokaribia, migogoro ya mfululizo si kama tu imeharibu utulivu wa hali ya Palestina, kuweka kipingamizi kipya kwa uchaguzi mkuu, bali pia itachochea hisia za watu wa Palestina dhidi ya Israel, kuathiri kiasi cha waungaji mkono wa Bw. Abbas, na kuongeza matatizo kwa juhudi za kuanzisha upya mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-20