Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-21 18:26:44    
Barua za Wasikilizaji 1221

cri

    Msikilizaji wetu Mbarak Mohammed Abucheri, wa sanduku la posta 792 Kakamega Kenya, ametuletea barua akianza kwa salamu na kutoa shukurani kwa watangazaji na wasimamizi wa Radio China Kimataifa kwa kuwaletea wasikilizaji matangazo na vipindi maridhawa moja kwa moja toka Beijing. Anasema hakika Radio China ni mwangaza ung'arao duniani. Kwani radio hii inawaelimisha watu wengi sana duniani hususan kwa kuwapa habari sahihi na za kuaminika, na kuwaburudisha kwa vipindi vyake maarufu.

    Anasema Radio China Kimataifa inaweza kufananishwa na ndege aina ya tausi, kwani maumbile yake ni ya kupendeza, rangi zake ni maridadi, mwendo wake ni safi na anapotaga mayai, anataga mayai ya dhahabu, na anapototoa vifaranga wake wanapototolewa ni fedha, na wanapokuwa wakubwa ni shaba na wanapokomaa ni chuma kisichoweza kuvunjwa kwa kutumia mikono.

    Anasema yeye akiwa msikilizaji mgeni na pia mwanachama mpya wa Radio China kimataifa amefurahishwa na namna watangazaji wa Radio hii wanavyoendesha shughuli za kila siku, hasa kwa kuzungumza kiswahili fasaha chenye mtiririko mzuri wenye kuvutia wasikilizaji, ambao unawapa wasikilizaji matumaini na matarajio ya moja baada ya nyingine. Haswa amefurahishwa na kupendezwa na namna watangazaji wanavyoendesha na kusikika vizuri katika kusoma taarifa ya habari, salamu zenu, Tazama China, Jifunze kichina, Ijue China, Chemsha bongo, ambapo ameweza kujua ukweli halisi kuhusu nchi ya jadi ya China na uhusiano wake na mataifa mbalimbali duniani ambayo ni washirika wake wakubwa kimaendeleo na kifalsafa. Pia anafurahi kwa kuwa Radio China inaendelea kuwajulisha mambo mbalimbali hasa kuhusu sayansi asilia, historia, siasa, kilimo na ufugaji, michezo na mambo mengine.

    Anasema angependa kutuambia tuendelee na juhudi zetu za kuwaelimisha, kuwafahamisha, kuwaburudisha na mwisho kuwashauri bila kuchoka au kuhofu kwani wao wako pamoja nasi. Pia anasema anawasilisha ombi la orodha ya wasikilizaji na wanachama wetu, tumtumie nambari yake ya wanachama, majarida au magazeti na vitabu vinavyoelezea historia pana kuhusu Radio China na taifa la China kwa jumla, nembo ya uanachama, fulana, kalenda au hata tai.

    Pia anasema angependa kupendekeza kubuniwa kwa kipindi cha maoni ya wasikilizaji, ukumbi wa mashairi, mashujaa wa Radio China na vijana na maendeleo. Anaongeza kusema kama kuna uwezekano pia viwepo vipindi kama tabasamu na tafakari, ili kupokea visa vya kufurahisha na kuchekesha, haki za watoto, haki za kina mama na haki za kina baba. Pia anasema anapendekeza viwepo vipindi kuhusu haki za wanyama, afya na maisha ya jamii. Anamaliza kwa kusema kuwa atafurahi kama tutayazingatia mapendekezo yake.

    Tunamshukuru msikilizaji wetu kwa Mbarak Mohamed Abucheri kwa mapendekezo yake. Tunapenda kumuarifu kuwa baadhi ya mapendekezo aliyotoa tayari yapo kwenye matangazo yetu, na wasikilizaji wetu wote wako huru kutuletea maoni yao wakati wowote. Labda kwa kuwa yeye ni msikilizaji mpya kama alivyosema, bado hajapata kuyasikia kwa kuwa yeye ni msikilizaji mpya. Hata hivyo maombi na mapendekezo mengine tutayazingatia.

    Msikilizaji wetu George Simiyu Wandabwa wa sanduku la posta 2287 Bungoma Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu, na kusema kuwa anatuandikia barua hii kwa furaha na kutupongeza kutokana na mawasiliano yetu kupitia kwa barua ambazo huzipokea vizuri sana tena kwa wakati unaofaa, kupitia kwa sanduku langu la barua. Anasema pia huvutiwa na vipindi ambavyo hupeperushwa hewani kila siku saa kumi na moja kamili hadi saa kumi na moja na nusu jioni kwa saa za Afrika mashariki, vipindi ambavyo husikika vizuri sana. Sasa watu wengi wameanza kuvutwa katika kijiji cha Nalondo na hata mlima Elgon kusikiliza matangazo ya Radio China. Pia anasema wanaelezwa na baadhi ya marafiki zao kuwa wanafurahia sauti zetu nyororo wakati wa matangazo na wanapenda sana kipindi cha salamu zenu.

    Na kuhusu mashindano ya chemsha bongo ya mwaka jana anasema angependa kuwapongeza wasikilizaji wenzake wote walioshiriki kwa juhudi ipasavyo. Pia anatoa pongezi za pekee kwa wasikilizaji Franz Manko Ngogo wa Tarime Tanzania na Xavier-Telly-Wambwa wa Bungoma Kenya kwa bidii yao . Anawaambia jaribuni "jaribu zaidi" ili mufikie tuzo maalum. Ombi lake kwa idhaa hii ni kwamba anapenda tuwatumie majibu sahihi baada ya matokeo ili waweze kusahihisha makosa yao.

    Anasema ombi lingine ni kuwa tujaribu kuandaa mikutano kama ule uliofanyika kisii Kenya, ili wajifunze mbinu mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kuifanya idhaa hii iweze kushindana na idhaa nyingine. Hii ni kwa kuwa mara nyingi hawajaweza kupata tuzo maalum. Njia hii pia itaweza kupunguza sababu za kushindwa kwa idhaa yetu kupata nafasi maalum kwenye mashindano ya chemsha bongo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-17