Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair anatarajia kufanya ziara ya siku mbili katika sehemu ya Palestina na Israel. Akiwa kiongozi wa nchi ya kigeni anayetembalea sehemu ya Palestina na Israel baada ya kiongozi wa Palestina Yaser Arafat kufariki dunia, lengo lake ni kusuluhisha misimamo ya pande mbili za Palestina na Israel na kufanya maandalizi kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Palestina a Israel uliopangwa kufanyika mwezi Februari mwaka kesho. Lakini kabla ya kiongozi huyo kufunga safari, waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon jana alisema kuwa Israel haitashiriki mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Palestina na Israel uliopendekezwa na Uingereza. Kauli hiyo ya Sharon inafanya jitihada za Blair za kuhimiza mchakato wa amani kugonga mwamba.
Ili kupunguza mgogoro wa kisiasa uliotokea nchini Uingereza kutokana na vita vya Iraq na kuboresha sura ya Uingereza duniani, Tony Blair anachukulia kuhimiza mchakato wa amani ya Palestina ya Israel kuwa moja ya madhumuni ya sera ya kidiplomasia ya serikali ya Uingereza. Muda si mrefu baada ya Arafat kufariki dunia, Blair alitoa haraka pendekezo la kufanya mkutano wa kimataifa mjini London akijaribu kuzindua upya mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel. Palestina, ambayo inataka kuanzisha nchi yake haraka, inajaribu kutumia fursa hiyo na nguvu za jumuiya ya kimataifa kuilazimisha Israel kurudi kwenye meza ya mazungumzo. Habari zinasema kuwa Palestina ina matumaini makubwa na mkutano wa kimataifa wa London kujadili suala la hadhi ya mwisho ya Palestina na Israel. Lakini Israel haina shauku na pendekezo la Blair, bali ni kinyume chake kuwa ina mashaka mengi. Maofisa wa ngazi ya juu wa Israel akiwemo waziri mkuu Sharon wamesema mara nyingi kuwa kabla ya Palestina kuchukua hatua halisi za kupambana na vikundi vyenye siasa kali, Israel haitaweza kuanzisha upya mazungumzo ya amani na Palestina, ama mazungumzo kuhusu suala la hadhi ya mwisho ya Palestina na Israel yanachukuliwa ni suala lililoko nje ya ajenda ya mazungumzo ya pande hizo mbili.
Ili kufanya Israel iunge mkono mkutano huo wa kimataifa wa London, Uingereza ililazimika kurekebisha ajenda za mkutano huo na kuieleza Israel mara nyingi kuwa lengo la kuitisha mkutano huo siyo kuupeleka mchakato wa amani ya Palestina na Israel katika "njia ya kasi", bali ni kutoa uungaji wa hali na mali kwa viongozi wapya wa Palestina na kuwasaidia kufanya mageuzi katika mambo ya siasa na usalama na kukuza uwezo wake wa kutekeleza majukumu yote yaliyowekwa katika mpango wa "ramani ya njia" ya amani ya mashariki ya kati. Hata hivyo, Israel bado ina mashaka. Tarehe 20 waziri mkuu Sharon huko Jerusalen alipokuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Czech alisema kuwa Israel inatambua umuhimu wa mkutano huo, lakini haitapeleka mwakilishi. Naibu waziri mkuu Ehud Olmert siku hiyo alisema kuwa jukumu muhimu la Israel kwa hivi sasa ni kutekeleza mpango uliobuniwa na Israel, aliongeza kuwa mkutano wa London utavuruga utekelezaji wa mpango huo. Kukataa kushiriki mkutano wa kimataifa wa London kwa Israel kunaonesha msimamo wake wa siku zote wa kutopenda kulifanya suala la Palestina na Israel kuwa la kimataifa. Toka muda mrefu uliopita, kutokana na kuhofia kushinikizwa na jumuia ya kimataifa kuitaka ilegeze masharti yake kwa Palestina, Israel inatarajia rafiki yake mkubwa Marekani kuongoza mchakato wa amani ya Palestina na Israel. Baada ya Arafat kufariki, Israel imekabiliwa na shinikizo kubwa duniani la kuanzisha upya mazungumzo ya amani na Palestina. Blair alifika hadi kutaka pande mbili za Palestina na Israel kuruka kipindi cha kwanza cha mpango wa "ramani ya njia" ya amani ya mashariki ya kati na kuingia moja kwa moja katika kipindi cha pili, yaani kuwa na mazungumzo kuhusu suala la lianzisha nchi ya Palestina, jambo ambalo linaifanya Israel kunung'unika.
Kutokana na msimamo wa Israel wa kutokuwa na ushirikiano, Blair anayetaka sana kuonesha umuhimu wake katika suala la Palestina na Israel, hana njia nyingine ila tu kurekebisha msimamo wake. Habari zinasema kuwa katika ziara yake katika sehemu ya Palestina na Israel, Blair atajitahidi kuondoa wasiwasi wa Israel na kuonesha kuwa mkutano wa London siyo "mkutano wa amani", wala hautagusia hadhi ya Jarusalen na kurejea kwa wakimbizi wa Palestina, tena atasihi maofisa wa Palestina wasiwe na matumaini makubwa na mkutano huo. Vyombo vya habari vinaona kuwa mafanikio na umuhimu wa mkutano wa kimatiafa wa London utapungua sana kutokana na Israel kukataa kushiriki kwenye mkutano huo na kurekebisha ajenda muhimu za mkutano huo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-17
|