Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair tarehe 21 alibadili ziara yake na kuitembelea Iraq kwa ghafla katika safari ya kwenda Israel na Palestina kufanya ziara. Wakati uchaguzi mkuu wa Iraq unapokaribia siku hadi siku na mashambulizi makali yanapofanyika huku na huko nchini Iraq, kwa nini Tony Blair aliamua kuitembelea Iraq ghafla, jambo hilo limefuatiliwa na watu.
Katika hali ya kutotangazwa, Tony Blair jana asubuhi aliondoka nchini Jordan na kuelekea Baghdad. Halafu alikuwa na mazungumzo na makamanda wa jeshi la muungano, maofisa waandamizi wa Iraq na maofisa wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Baada ya mazungumzo, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Tony Blair na waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq Bw. Iyad Allawi, Tony Blair alieleza kuunga mkono kwa uthabiti uchaguzi mkuu wa Iraq. Alisema kuwa ingawa hali ya usalama nchini Iraq ni mbaya na mashambulizi yanalenga kuharibu uchaguzi mkuu yanatokea huku na huko, lakini uchaguzi mkuu unapaswa kufanyika katika tarehe iliyowekwa na kuwashirikisha watu wa sekta mbalimbali wa Iraq.
Wachambuzi wanaona kuwa ziara hiyo ya Tony Blair nchini Iraq ina malengo mawili. Kwanza ni kuwasalimia wanajeshi elfu nane na mia tano wa Uingereza walioko nchini Iraq kabla ya sikukuu ya Krismas ili kuwatia moyo, na wakati huo huo kuboresha sura yake nchini Uingereza iliyoathiriwa na vita vya Iraq.
Jambo muhimu zaidi ni kufanya kampeni za kuunga mkono uchaguzi mkuu wa Iraq. Sasa ni wiki sita tu zimebaki kabla ya kufika tarehe ya uchaguzi mkuu wa Iraq iliyopangwa, lakini mashambulizi makali yanaongezeka nchini Iraq. Milipuko miwili tu iliyotokea tarehe 19 katika miji miwili mitakatifu iliwaua watu 67 na wengine 175 kujeruhiwa. Ndipo wakati Tony Blair alipoitembelea Iraq, mkahawa wa kituo cha kijeshi cha Marekani kilichoko mjini Mosul ulishambuliwa kwa mizinga, wizara ya ulinzi ya Marekani ilithibitisha kuwa watu wasiopungua 22 waliuawa na wengine 55 kujeruhiwa. Zaidi ya hayo, maofisa 9 wanaoshughulikia uchaguzi huo pia waliuawa. Kama kuongezeka kwa mashambulizi makali kutauwezesha uchaguzi mkuu ufanyike kwa tarehe iliyopangwa au la, ni suala ambalo linalofuatiliwa tena na watu. Katika wakati huo muhimu, lengo kuu la ziara ya Blair nchini Iraq ni kuonesha uungaji mkono thabiti kwa uchaguzi mkuu na kuzishawishi pande mbalimbali zishikilie kufanya uchaguzi huo katika tarehe iliyopangwa.
Kwa Bw Tony Blair na rais Bush wa Marekani, vita vya Iraq vimewavuruga siku zote. Hao wawili wote wanatarajia kutuliza hali ya Iraq kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika kwa tarehe iliyopangwa. Kwa hiyo wanatetea kwa uthabiti kutobadili tarehe ya uchaguzi mkuu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan tarehe 21 alieleza kuwa uchaguzi mkuu wa Iraq kufanyika kwa tarehe iliyopangwa au la, suala hilo linapaswa kuamuliwa na wairaq, lakini kama mashambulizi yataendelea, hakika yataleta athari kwa uchaguzi mkuu. Kadiri tarehe ya uchaguzi mkuu wa Iraq inavyokaribia, ndivyo mabadiliko ya hali ya Iraq yatafuatiliwa zaidi na watu wengi zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2004-12-22
|