Wimbi jipya la kumtaka aondoke madarakani linahusiana na matukio mawili yaliyotokea hivi karibuni yanayomhusu. Tarehe 8 mwezi Desemba Bw. Rumsfeld alipokwenda Kuwait kukagua jeshi la Marekani lililoko huko, wakati alipojibu suala kuhusu upungufu wa zana za majeshi, alisema kuwa askari wa Marekani wanaweza tu kwenda vitani kwa zana zilizoko hivi sasa wala siyo zana wanazotaka au wanazotarajia kuwa nazo siku za baadaye. Watu wengi walimkosa kuwa hajali usalama wa askari wa Marekani. Muda si mrefu baada ya hapo, Rumsfeld alilalamikiwa na jamaa wa askari waliofariki vitani kutokana na kuwa hakusaini yeye mwenyewe barua ilizoandika wizara ya ulinzi kwa jamaa wa askari waliofariki katika mapigano. Aidha, hali ya usalama nchini Iraq haikuboreshwa kwa udhahiri, ambayo inasababisha uchaguzi mkuu wa Iraq unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Januari mwaka kesho kukabiliwa na shinikizo kubwa la suala la usalama, jambo ambalo linamwajibisha Rumsfeld.
Shinikizo linalomkabili Rumsfeld hivi karibuni siyo kutoka kwa chama cha Democrat na vyombo vya habari peke yake, baadhi ya wabunge wa chama cha Republican pia wamepoteza imani yao juu yake, wanamkosoa kwa kuwa kazi zake zinakosa ufanisi na kutosikiliza maoni ya watu wengine. Watu wa kundi jipya la wahafidhina pia wanamkosoa Rumsfeld kwa kutokuwa na mpango kamili kuhusu kuikalia Iraq kwa muda mrefu wala hakupeleka idadi kubwa ya askari kutokomeza harakati za wapinzani na kuendeleza vizuri na ujenzi mpya nchini humo, na kumtaka ajiuzulu. Wakati huo huo, kiwango cha uungaji mkono wa wamarekani kwa Rumsfeld pia kimeshuka. Uchunguzi wa kura za maoni ya raia unaonesha kuwa 52% ya watu walioulizwa wanaona kuwa Rumsfeld angeondoka madarakani, wakati 56% ya watu wanaona kuwa hakuna faida kwa kuanzisha vita vya Iraq.
Ingawa Rumsfeld anakabiliwa na shinikizo kutoka pande mbalimbali, lakini Ikulu ya Marekani siku zote inamwunga mkono. Mkurugenzi wa ofisi ya Ikulu Bw. Andrew Card tarehe 19 alisifu kazi za Rumsfeld, na kusema kuwa rais Bush ana imani kubwa juu yake. Katika mkutano uliofanyika na waandishi wa habari tarehe 20, rais Bush alieleza kwa mara nyingine kuwa anamwunga mkono Rumsfeld kwa nguvu zake zote. Katika mazingira ya namna hiyo, baadhi ya wanachama muhimu wa chama cha Republican ingawa hawafurahishwi na Rumsfeld, lakini wanaona kuwa si busara kumbadilisha katika wakati muhimu. Mwenyekiti wa kamati ya kijeshi ya bunge la Juu la Marekani Bw John Warner amesema kuwa uchaguzi mkuu wa Iraq utafanyika hivi karibuni na kutakuwa na shida nyingi katika muda mrefu baada ya uchaguzi mkuu, hivyo haifai kumbadilisha waziri wa ulinzi katika wakati muhimu. Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa kidiplomasia ya baraza la juu la bunge la Marekani Bw Richard Lugar pia amesema kuwa si vizuri kumbadilisha waziri wa ulinzi wakati wa vita, Rumsfeld anapaswa kuwajibika kuhusu makosa hayo, lakini angeruhusiwa kuendelea na wadhifa wake.
Rumsfel mwenyewe pia amechukua baadhi ya hatua ambazo ni pamoja na kutoa taarifa katika gazeti la Stars and Stripes la jeshini kuwa katika siku za usoni yeye atasaini barua zote kwa wafiwa wa askari wote waliofariki katika uwanja wa vita..
Wachambuzi wanasema kuwa hadhi ya Rumsfeld bado ni salama kwa hivi sasa, ukipita muda wa uchaguzi mkuu wa Iraq unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka kesho na shughuli za majeshi ya ulinzi katika mwaka mpya na tathimini ya wizara ya ulinzi wa Marekani kuhusu nguvu za kijeshi inayofanyika kila baada ya miaka minne. Lakini hayo hayamaanishi kuwa Rumsfeld ataweza kupita kwa salama miaka yote minne ya kipindi chake.
Idhaa ya kiswahili 2004-12-22
|