Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair jana alifanya ziara ya muda mfupi nchini Palestina na Israel. Bw. Blair akiwa kiongozi wa kwanza wa kigeni anayezuru Palestina na Israel baada ya kufariki dunia kwa kiongozi wa zamani wa Palestina Yasser Arafat, anataka kuonesha kuwa Uingereza inazingatia sana masuala ya kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel na kuhimiza mchakato wa amani. Pia kwa kupitia njia hiyo, Bw. Blair anataka kusuluhisha misimamo ya Palestina na Israel ili kufanya matayarisho kwa mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati utakaofanyika huko London mwanzoni mwa mwaka kesho.
Jana kwa nyakati tofauti Bw. Blair alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon na mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya chama cha ukombozi wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas kuhusu hali ya Palestina na Israel na mkutano wa kimataifa wa London kuhusu suala la Mashariki ya Kati. Kabla ya hapo, Israel ilikuwa na wasiwasi kuwa mkutano huo utasababisha kuanzisha tena mazungumzo kati yake na Palestina, hivyo ilieleza wazi kuwa haitashiriki kwenye mkutano huo. Ili kupata uungaji mkono wa Israel, Uingereza inabainisha kuwa, mkutano huo utajadili namna ya kutoa misaada kwa Palestina.
Lakini ni wazi kuwa Palestina inasikitishwa na maelezo ya Uingereza. Waziri mkuu wa serikali ya Palestina Bw. Ahmod Qurei alisema kuwa, licha ya kujadili mageuzi ya ndani ya Palestina, Palestina pia inatumai kuwa mkutano huo utafanya mashauriano kuhusu utatuzi wa mgogoro kati yake na Israel.
Katika ziara yake Bw. Blair alisisitiza kuwa, mkutano wa London utazingatia kuisaidia Palestina kufanya mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na mfumo wa usalama ili kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza mpango wa amani ya Mashariki ya Kati, lakini hautajadili mgogoro kati ya Palestina na Israel, hivyo Uingereza haikutarajia Israel kushiriki katika mkutano huo. Pia alisisitiza kuwa, ugaidi ni kikwazo cha mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel kupata mafanikio, hivyo Palestina lazima ichukue hatua kwanza kusimamisha mashambulizi kwa Israel. Aidha, Bw. Blair alitoa maoni yake kuhusu msingi wa kuanzisha tena mpango wa amani ya Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Palestina kufanya uchaguzi wa kidemokrasia na kufanya mageuzi ya siasa, uchumi na jeshi la usalama ili kuanzisha mfumo wa usalama unaoaminika; jumuiya ya kimataifa kuweka mpango ili kutoa misaada kwa Palestina; na Israel kutekeleza mpango wa upande mmoja wa kuondoka kutoka eneo la Gaza na eneo la kando ya magharibi ya Mto Jordan. Alisema kuwa baada ya kutekeleza hayo, ndiyo Palestina na Israel zinaweza kurudisha mpango wa amani na ndiyo Palestina inaweza kuanzisha nchi yake. Bw. Blair alisisitiza kuwa mkutano wa kimataifa wa London utazisaidia Palestina na Israel kurudisha mpango wa amani, lakini hautakuwa mkutano wa kujadili na kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel. Habari zinasema kuwa, Palestina iliwahi kuwa na matumaini kuwa Bw. Blair ataweka shada la maua kwenye kaburi la Arafat alipozuru Ramallah ili kuonesha uungaji mkono kwa Palestina, lakini Bw. Blair alikataa.
Maoni ya raia yanaona kuwa, hivi sasa kuna tofauti kubwa kati ya Palestina na Israel katika suala la kuanzisha tena mazungumzo ya amani. Palestina inatumai sana kuanzisha mazungumzo mapema ili kurudisha mpango wa amani, lakini Israel inasisitiza kuwa kabla ya kuanzisha tena mazungumzo ya amani, Palestina lazima ipambane kwa halisi na watu wenye siasa kali ili kusimamisha mashambulizi dhidi ya Israel. Msimamo huo wa Israel katika suala hilo unaungwa mkono na Marekani. Kutokana na hali hiyo, ingawa Bw. Blair anataka kusuluhisha mgogoro, lakini anapaswa kukabiliana na hali hiyo, kwa kuwa udhibiti wa Marekani kwa mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel hauwezi kubadilika katika muda mfupi.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-23
|