Wakati unapokaribia mwisho wa mwaka, vyombo vya habari vya Ulaya vimechambua uchumi wa dunia wa mwaka 2004 na kuona kuwa, uchumi wa dunia mwaka huu umeshika njia ya ongezeko la haraka, ongezeko hilo limesaidia umoja wa uchumi wa aina zote, hali hii ilikuwa nadra kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Lakini wakati huo huo, bei ya mafuta imeongezeka sana, na thamani ya dola ya kimarekani imeshushwa, hayo yote yameleta athari mbaya kwa uchumi wa duniani, na huenda yakaathiri vibaya maendeleo mazuri ya uchumi wa dunia.
Shirika la fedha duniani linakadiria kuwa, ongezeko la uchumi wa dunia litafikia karibu asilimia 5, ongezeko hilo litakuwa la haraka zaidi kuliko miaka iliyopita tokea mwaka 1973. Mwaka huu uchumi wa Marekani, sehemu zinazotumia Euro na Japan unafufuka kwa wakati mmoja, ongezeko la uchumi wa Marekani limefikia 4.3 %, la sehemu zinazotumia Euro ni 2.2 % na la Japan ni 4.4 %, na ongezeko la uchumi wa nchi zinazoendelea linatazamiwa kufikia 6.6 %. Toleo la mwezi Novemba la Jarida la wiki la "Wataalamu wa uchumi" la Uingereza lilisema kuwa, mashirikisho muhimu ya uchumi yapatayo 55 duniani yanayofuatiliwa na jarida hilo yote yanadumisha ongezeko lao la uchumi. Hali hiyo nzuri imetokea kwa mara ya kwanza tokea mwaka 1980, na imeonesha kuwa nchi na sehemu nyingi zaidi zimefaidika na ongezeko la uchumi.
Hali inayostahiki kutajwa ni kuwa, mwaka huu uchumi wa nchi zinazoendelea umekuwa na hali nzuri katika mabara ya Latin Amerika, Afrika, sehemu ya mashariki ya kati au nchi za madola huru. Hasa nchi zinazoendelea za bara la Asia, ongezeko la thamani ya jumla ya uzalishaji mali linakadiriwa kufikia 7.6 % mwaka huu. Na ongezeko la uchumi wa China linachangia siku hadi siku ongezeko la uchumi wa dunia. Maongezeko ya haraka la China, India na mashirikisho mengine ya uchumi yanabadilisha hali ya ongezeko la uchumi wa dunia, pia yanaharakisha marekebisho ya miundo ya uchumi wa dunia.
Vyombo vingi vya habari vya Ulaya vinachukua tahadhari wakati wa kutarajia mustakbali wa uchumi wa dunia wa mwaka 2005. Baadhi ya wataalamu wa uchumi wa Ulaya wanakadiria kuwa ongezeko la uchumi wa dunia mwaka kesho litakuwa 3.5 %-4 %, ambalo ni chini ya lile la mwaka huu. Hata lengo hilo likitaka kutimizwa, lazima kuchukua tahadhari kukwepa matatizo kadhaa yaliyojificha ambayo huenda yatasababisha uendeshaji wa uchumi wa dunia uende mrama.
Tatizo la kwanza ni pengo kubwa la matumizi na mapato na pengo la biashara la Marekani linaloongezeka siku hadi siku, huenda litasababisha kiasi cha ubadilishaji wa dola za kimarekani kiendelee kuwa chini zaidi, hii ni changamoto kubwa itakayoukabili uchumi wa duniani. Kuanzia mwanzo wa mwaka 2002, serikali ya Marekani ilijaribu kupitia kushusha thamani ya dola za kimarekani kuiacha dunia ibebe kwa pamoja hatari ya "mapengo yake mawili". Rais Bush hivi karibuni alitoa taarifa kuhusu kudumisha nguvu ya dola za kimarekani, lakini taarifa hiyo haiwezi kuliwezesha soko liamini kuwa Marekani itabadilisha sera yake ya kudhoofisha dola ya kimarekani. Baadhi ya watu wanaona kuwa, kama wawekezaji vitega uchumi wakikata tamaa juu ya uchumi wa Marekani, watauza dola za kimarekani kwa kiasi kikubwa, basi uchumi wa Marekani utapata hasara kubwa, na uchumi wa dunia hakika utaathiriwa vibaya.
Tatizo la pili ni bei ya mafuta. Tokea mwanzoni mwa mwaka huu, bei ya mafuta imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, ongezeko la bei ya mafuta kwa mwaka mzima limefikia 30 %, na bei ya kila pipa la mafuta imepanda juu na kufikia dola za kimarekani 40. Athari mbaya ya bei kubwa ya mafuta kwa uchumi wa dunia imeonekana, ambapo ongezeko la uchumi wa dunia limekuwa likienda taratibu katika nusu ya pili ya mwaka huu, hali hiyo pia imeongeza shinikizo la mfumuko wa bei.
Aidha, mashambulizi makubwa ya kigaidi yanayoweza kutokea wakati wowote pamoja na ongezeko la akiba la mabenki ya nchi zilizoendelea, na mwelekeo wa hifadhi ya kibiashara, yote hayo yanaweza kuzuia maendeleo ya uchumi wa dunia.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-17
|