Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-23 20:50:26    
Uhusiano kati ya Saudi Arabia na Libya wawa mbaya ghafla

cri

    Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Bw. Saud Al-Faisal jana alitangaza ghafla kuwa, Saudi Arabia imeamua kumfukuza balozi wa Libya nchini humo na kumwita balozi wa Saudi Arabia kutoka nchini Libya. Bw. Faisal alisema kuwa, Saudi Arabia imechukua uamuzi huo kutokana na Libya kupanga kisirisiri kumwua mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Bw. Abdullah Ibn Abdul-Aziz. Wachambuzi wanaona kuwa, uhusiano wa nchi hizo mbili unakabiliwa na changamoto tena.

    Bw. Faisal alisema kuwa, "ingawa kumetokea jambo baya", lakini Waislamu duniani watafanya hija katika miji mitakatifu ya Makkah na al-Madinah nchini Saudi Arabia mwezi ujao. Ili waislamu wa Libya waweze kufanya hija nchini humo, ubalozi wa Saudi Arabia nchini Libya utaendelea kufanya kazi, na ubalozi wa Libya nchini Saudi Arabia pia "unaweza kuendelea kufanya kazi".

    Mwezi Juni mwaka huu, gazeti la New York Times lilidokeza kwanza kuwa, katika mwezi Agosti hadi mwezi Novemba mwaka jana, idara za upelelezi za Marekani, Saudi Arabia, Uingereza na Misri zilifichua mpango mmoja wa kumwua mrithi wa mfale wa Saudi Arabia Bw. Abdullah Ibn Abdul-Aziz, na kuwakamata watuhumiwa wawili na wanachama wanne wa kundi la Al-Qaeda la Saudi Arabia. Watuhumiwa walikiri kuwa, walitumwa na wapelelezi wa Libya, na mpango huo ulikuwa uamuzi wa kiongozi wa Libya Bw. Omar Muammar al-Gadaffi.

    Abdel Rahman al-Amoudi ni mmoja wa watuhumiwa aliyekiri kwanza kuhusu mpango huo kwanza. Alipohukumiwa alisema kuwa, alikutana na Bw. Gadaffi mara mbili katika majira ya joto mwaka jana, na kumtaka aharakishe hatua ya kumwua Bw. Abdullah.

    Serikali ya Libya imekanusha maneno ya watuhumiwa hao. Mtoto wa Bw. Gadaffi na waziri wa mambo ya nje wa Libya Bw, Abdul Rahman Mohammad Shalgam wote wamesema kuwa maneno hayo si ya kweli.

    Tangu Bw. Gadaffi ashike madaraka mwaka 1969, uhusiano wa Libya na Saudi Arabia unaendelea kuwa mbaya. Bw. Gadaffi aliupindua utawala wa mfalme tarehe mosi mwezi Septemba, na siku zote hapendi nchi za kifalme za Ghuba. Mwaka 1999, Saudi Arabia na Afrika ya Kusini zilisuluhisha mgogoro wa ajali ya ndege ya Lockerbie na kuboresha uhusiano kati ya Libya na nchi za magharibi, na uhusiano kati ya Libya na Saudi Arabia pia uliboreshwa. Lakini baada ya tukio la tarehe 11 mwezi Septemba kutokea nchini Marekani, Bw. Gadaffi aliilaani mara kwa mara Saudi Arabia kuwa ni chanzo cha watu wenye siasa kali wa kundi la Al-Qaeda, na Saudi Arabia inailaani Libya kwa kuharibu umoja wa nchi za kiarabu, na uhusiano wa nchi hizo mbili uliendelea kuwa mbaya. Tarehe mosi mwezi Machi mwaka 2003, Bw. Gadaffi na Bw. Abdullah walibishana vikali kwenye mkutano wa wakuu uliofanyika huko Sharam el-Sheikh nchini Misri, hata nchi hizo mbili karibu zilitaka kusimamisha uhusiano wa kibalozi. Na kitendo cha walinzi wa Libya kumwonea na kumpiga waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia bw. Faisal kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu uliofanyika mwezi Septemba mwaka jana kumeufanya uhusiano wa nchi hizo mbili kuwa mbaya zaidi.

    Wachambuzi wanaona kuwa, hivi sasa hali ya Mashariki ya Kati ni nyeti sana, na inahitaji nchi za kiarabu kuimarisha umoja na ushirikiano. Saudi Arabia na Libya ni nchi za kiarabu zenye athari kubwa, hivyo bila shaka uhusiano mbaya wa nchi hizo mbili utaathiri vibaya umoja wa nchi za kiarabu na kupunguza uwezo wake wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-23