
Uchaguzi wa serikali za mitaa wa Palestina ulianza jana katika eneo la kando ya magharibi ya Mto Jordan. Hii ni mara ya kwanza kwa Palestina kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa katika kipindi cha miaka 28 iliyopita. Maoni ya raia yanaonesha kuwa, uchaguzi huo ni mazoezi ya uchaguzi wa mamlaka ya utawala wa Palestina utakaofanyika mwezi Januari mwakani.
Kwa kuwa Israel imeweka kizuizi cha kijeshi kwa baadhi ya maeneo ya Palestina, hivyo uchaguzi huo utafanyika katika vipindi vitatu. Uchaguzi uliofanyika jana ulikuwa ni wa kipindi cha kwanza, na kipindi cha pili cha uchaguzi huo kitafanyika katika sehemu nyingine za magharibi ya Mto Jordan baada ya miezi miwili. Uchaguzi wa mwisho utafanyika kwenye mitaa 10 ya eneo la Gaza tarehe 27 mwezi Januari, mwaka 2005.
Katika uchaguzi uliofanyika jana, wagombea 1003 walishiriki kugombea viti 603 vya ujumbe wa serikali za mitaa 26 ya eneo la kando ya magharibi ya Mto Jordan. Siku hiyo, kutokana na hamu kubwa ya wapiga kura wa Palestina, vituo vingi vya upigaji kura vilikuwa na misururu mirefu, na kazi ya upigaji kura iliyopangwa kumalizika saa moja usiku wa siku hiyo iliongezwa kwa saa mbili. Inakadiriwa kuwa kiasi cha watu waliojitokeza kupiga kura kitafikia asilimia 90.
Mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya chama cha ukombozi wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas alisema kuwa, uchaguzi huo ni hatua ya kujenga heshima ya mamlaka ya utawala wa Palestina. Aliwasihi Wapalestina kulinda haki ya kidemokrasia na kujitokeza kupiga kura ili kuhimiza ujenzi wa kidemokrasia na mfumo wa sheria wa Palestina. Waziri mkuu wa serikali ya Palestina Bw. Ahmed Qureia alijipigia kura katika wilaya ya Abu Dis anayoishi. Alisema kuwa katika uchaguzi huo, watu watatoa uchaguzi wao. Uchaguzi huo ni mazoezi ya uchaguzi wa mamlaka ya utawala wa Palestina utakaofanyika Januari 9 mwakani na mazoezi ya uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria, pia ni hatua ya kwanza kupigwa na Palestina katika kutimiza demokrasia na kuanzisha nchi ya Palestina.
Karibu pande zote za Palestina ikiwemo Hamas zimewateua wagombea wao ili kushiriki katika uchaguzi. Hamas ilitangaza kuwa, itashiriki katika uchaguzi ili kwa kupitia njia hiyo "inaweza kutia damu changa kwa mamlaka ya utawala wa Palestina." Hali hiyo inaonesha kuwa ushindani ni mkali. Habari zinasema kuwa, katika nyanja nyingi, Fatah itakabiliana na changamoto kubwa kutoka kwa Hamas. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, wapiga kura wanazingatia zaidi mchango unaotolewa na wagombea kwa mitaa yao. Kwa muda mrefu Hamas imeanzisha jumuiya nyingi za misaada ili kupata uungaji mkono kutoka kwa watu, hivyo wagombea wake wengi wana nguvu kubwa. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya raia uliofanyika kabla ya hapo, Hamas inaweza kupata ushindi katika baadhi ya sehemu kwenye eneo la Gaza. Wachambuzi wanaona kuwa, kama Hamas itashinda, basi inaweza kumleta matatizo zaidi Bw. Abbas katika juhudi zake za kuhimiza pande zote za Palestina kufikia makubaliano ya kusimamisha vita. Lakini waziri mkuu Bw. Qureia bado alikaribisha Hamas kushiriki katika uchaguzi. Alisema kuwa, mamlaka ya utawala wa Palestina inaona kuwa Hamas kushiriki katika uchaguzi wa serikali ya mitaa ni kitendo kizuri, hali hiyo pia inaonesha kuwa Hamas inapenda kushiriki katika maamuzi ya sera za Palestina.
Aidha, katika uchaguzi huo, wanawake wengi wanavunja minyororo ya mawazo ya jadi na kuwa wagombea kushiriki katika uchaguzi. Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa mitaa inayotungwa na mamlaka ya utawala wa Palestina, wanawake lazima wapate asilimia 16 ya viti kwa uchache katika idara za serikali za mitaa. Mgombea mmoja mwanamke alisema kuwa, wanawake wanachukua asilimia 52 katika kijiji anachoishi, hivyo lazima waweze kutoa sauti katika idara za serikali za mitaa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-24
|