Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-24 20:59:40    
Afganistan yaunda baraza mpya la mawaziri

cri

    Rais Hamid Karzai wa Afganistan jana alitangaza orodha ya majina ya wajumbe wa baraza la mawaziri, na waziri wa ulinzi na waziri wa fedha wamebadilishwa. Aidha, Rais Karzai aliongeza wizara ya kupambana na dawa za kulevya ili kuondoa tatizo la dawa hizo nchini humo.

    Akiwa Rais wa nchi hiyo aliyechaguliwa na umma, Bw. Karzai ana uhuru mkubwa katika kuteua mawaziri, hana haja ya kufanya majadiliano na makundi mbalimbali ya kijeshi, na hali hiyo inasaidia kujenga serikali kuu yenye nguvu kubwa halisi. Lakini makundi mbalimbali ya kijeshi hayataki kupoteza hadhi katika serikali mpya., makundi hayo yanadhibiti siasa, uchumi na utozaji kodi katika sehemu mbalimbali nchini Afganistan na kuwa tishio kubwa kwa serikali kuu. Hivyo si rahisi kuunda baraza mpya la mawaziri lisiloshirikisha makundi ya kijeshi na kuwa na uwiano kati ya pande mbalimbali nchini humo.

    Kutokana na orodha ya majina iliyotangazwa, Rais Karzai amewaondoa viongozi wa makundi ya kijeshi kutoka kwenye baraza hilo na kuteua watu wengi wenye utaalamu maalum watakaoweza kuaminiwa na nchi wafadhili na wawekezaji.

    Waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo Bw. Mohammed Fahim nafasi yake imechukuliwa na naibu waziri Bw. Abdul Rahim Wardak, waziri wa zamani wa fedha Bw. Ashraf Ghani amebadilishwa na nafasi yake imechukuliwa na mkuu wa benki kuu ya   serikali Bw. Anwar ul-Haq Ahadi, na waziri wa mambo ya nje na waziri wa mambo ya ndani wataendelea na nyadhifa zao.

    Bw. Fahim ni kiongozi wa kundi la muungano wa kaskazini, na aliwahi kutoa mchango mkubwa katika kuupindua utawala wa Taliban, kabla ya hapo, alikuwa makamu wa Rais wa Afganistan na waziri wa ulinzi. Bw. Wardak aliyeteuliwa kuwa waziri wa ulinzi ni m-Pushtu na aliwahi kupewa mafunzo ya kijeshi nchini Marekani.

    Kiongozi wa kundi kubwa la kijeshi la magharibi ya nchi hiyo Bw. Ismail Khan ameteuliwa waziri wa maji na nishati. Wachambuzi wanaona kuwa kuteuliwa kwake kunaweza kupingwa, hasa na nchi za magharibi na jumuiya ya haki za binadamu. Kwa upande mmoja, alisadikiwa kuwa alifanya vitendo vingi vya kukiuka haki za binadamu, kwa upande mwengine, chini ya utawala wake, mikoa ya magharibi ya nchi hiyo ilikuwa na maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni.

     Aidha, kwa mujibu wa katiba ya Afganistan, mawaziri hawaruhusiwi kuwa na uraia wa nchi nyingine na wanatakiwa kuwa na shahada ya kwanza au zaidi. Masharti hayo yameweka vikwazo kwa Rais Kazai kuteua mawaziri. Ofisa wa serikali ya nchi hiyo amedokeza kuwa, baraza hilo limejumuisha wataalamu wengi, na wanasiasa muhimu wasiotimiza sharti la kuwa na shahada wanapewa hadhi zilizoko chini kidogo tu kuliko uwaziri.

   Kinachofuatiliwa sana kuhusu baraza hilo jipya ni wizara ya kupambana na dawa za kulevya iliyoongezwa. Kutokana takwimu mpya za Umoja wa Mataifa, kilimo cha dawa za kulevya nchini Afganistan kimeongezeka kwa kasi katika miaka ya karibuni, na nchi hiyo imezidi Colombia na kuwa kituo kikubwa kabisa duniani cha kutengeneza dawa za kulevya. Mwaka jana, kilimo cha kasumba kimeleta dola bilioni 2.3 za kimarekani kwa nchi hiyo, ikivuka nusu ya mapato ya jumla ya taifa. Nchini humo, kuondoa kilimo na biashara ya dawa hizo kunahusiana kwa karibu na kupambana na ugaidi na kuondoa umaskini. Kuanzishwa kwa wizara hiyo kutaongeza nguvu ya kupambana na kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya.

    Kwa mujibu wa katiba ya Afghanistan, baraza jipya la mawaziri lazima lipitishwe na bunge la umma la nchi hiyo. Kutokana na mpango uliowekwa, uchaguzi wa bunge utafanyika mwezi Aprili mwaka kesho. Upigaji kura kuhusu baraza hilo la mawaziri walioteuliwa na Rais Karzai utafanyika baada ya kuundwa kwa bunge la umma.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-24