Mashambulizi ya mabomu ya kujiua yaliyotokea kwenye kambi ya jeshi la Marekani huko Mosul nchini Iraq yamefuatiliwa sana na watu wengi nchini Marekani. Tofauti na hali ya zamani ni kuwa, washambulizi wa kujiua walipita kwenye ukaguzi mbalimbali na kuingia kwenye ukumbi wa chakula wa kambi hiyo ya jeshi la Marekani, na kuzusha mlipuko wakati askari walipokusanyika na kula chakula, na kusababisha vifo vya watu 22 wakiwemo askari 18 na raia mmoja wa Marekani. Mashambulizi hayo yaliishtusha sana nchi nzima ya Marekani.
Uchunguzi mpya wa maoni ya raia umeonesha kuwa, asilimia 56 ya raia wa Marekani wanapinga vita vya Iraq. Mashambulizi hayo kabla ya sikukuu ya Krismasi yalizidi kuchochea hasira ya wamarekani kwa vita vya Iraq. Mmarekani Bw. Laura Costas anayeishi kwenye jimbo la Maryland aliandika barua kwa gazeti la "New York Times" kuipinga serikali ya Marekani kutekeleza sera mbaya ya kidiplomasia na mikakati yenye makosa mengi ya kijeshi. Aliwataka wamarekani wanaopinga vita watoe maoni yao kwa uthabiti na kuiomba serikali ya Marekani iondoe jeshi lake kutoka Iraq. Watu wengine waliishutumu serikali ya Marekani kutolinda vizuri usalama wa askari, na kuwauliza maofisa wa Marekani kwa nini hawapeleki watoto wao kwenda kushiriki kwenye vita vya Iraq.
Baada ya kushambuliwa kwa kambi ya jeshi la Marekani huko Mosul, kazi muhimu ya kwanza ya jeshi la Marekani ni kuulinda usalama wa vikosi vyake. Lakini baadhi ya wamarekani waliainisha kuwa, serikali ya Marekani si kama tu haiwezi kuboresha hali ya usalama wa Iraq , bali pia haiwezi kulinda usalama wa askari wake. Tukio hilo limeonesha kuwa si rahisi kuulinda usalama wa askari wa Marekani nchini Iraq.
Kwanza, wapinzani wa Iraq walipata habari sahihi, na kujua utaratibu wa kambi ya jeshi la Marekani. Kwa hivyo wairaq wanaofanya kazi kwenye kambi ya jeshi la Marekani wanatuhumiwa. Lakini kambi ya jeshi la Marekani inahitaji wairaq wengi wa kufanya kazi kutafsiri, kushughulikia kazi za utengenezaji na ujenzi na kusaidia kazi za majikoni. Watu wa jeshi la usalama wa Iraq huingia na kutoka kwenye kambi ya jeshi la Marekani. Si rahisi kwa Marekani kuchunguza kama wairaq haoa wana uhusiano na wapinzani au la.
Wachambuzi walionesha kuwa, kuimarisha usalama wa kambi za jeshi la Marekani kutakuwa gharama kubwa, na hii itapunguza maliasili zinazotarajiwa kutumiwa katika mapambano dhidi ya wapinzani. Aidha hatua nyingi za kupita kiasi za usalama zitawashinikiza askari na kuwaathiri sana. Walieleza kuwa, siku zote kuzatitiwa kikamilifu kukwepa mashambulizi kutaleta shinikizo kubwa mioyoni, jambo ambalo askari wa Marekani hawawezi kulivumilia.
Tukio hilo la Mosul limetokea kabla ya uchaguzi mkuu wa Iraq utakaofanyika mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2005. Ili kutuliza hali ya usalama nchini Iraq kabla ya uchaguzi huo, jeshi la Marekani linapaswa kufanya msako wa wapinzani. Lakini kuna mjadala mkali nchini Marekani kuhusu sera ya kuwasaka wapinzani hao, hili vilevile ni tatizo kubwa linaloisumbua serikali ya Bush.
Habari zinasema kuwa, wizara ya ulinzi ya Marekani inapenda kukusanya nguvu za askari halafu kuwasaka wapinzani sehemu moja baada ya nyingine kama ilivyofanya huko Fallujah. Lakini kufanya hivyo ni rahisi kushambuliwa kwa sehemu kadha wa kadhaa zilizotuma askari.
Baadi ya watu wamelitaka jeshi la Marekani kuongeza askari kwa kiasi kikubwa nchini Iraq, lakini maofisa wa wizara ya ulinzi wa taifa wanaona kuwa kufanya hivyo pia kutaleta hatari. Kwa upande mmoja, hatua hii itazidisha chuki za watu wa Iraq kwa jeshi la Marekani, na kwa upande mwingine kuongeza askari wengi kupita kiasi kutakuwa ni kuongeza shabaha zaidi kwa wapinzani katika mashambulizi.
Baada ya vita vya Iraq kuanza mwaka jana, Marekani iliwahi kutumai kuwa maendeleo kadhaa makubwa yatapunguza upinzani wa watu wa Iraq. Lakini hali halisi ni kuwa, mashambulizi yanazidi kuongezeka siku hadi siku. Aidha wanajeshi wa Iraq waliofundishwa na Marekani hutoroka vitani. Kutokana na hali hiyo, hakuna matumaini kuwa hali ya usalama itabadilika kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Iraq.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Bw. Donald Rumsfeld tarehe 22 katika mkutano na waandishi wa habari alikuwa bado anazungumzia "Iraq-nchi yenye amani, demokrasia na ustawi", lakini alikiri pia kuwa " kutarajia kujitokeza kwa Iraq yenye amani baada ya uchaguzi mkuu kutakuwa ni kosa". Kwa hivyo, kushambuliwa kwa jeshi la Marekani huko Mosul kumesababisha malalamiko na wasiwasi miongoni mwa watu wa Marekani kwa vita vya Iraq, na kuonesha kuwa serikali ya Marekni haijui la kufanya inapokabiliana na hali yenye vurugu nchini Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-24
|