Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-27 15:43:10    
Kwa nini Thamani ya Dola ya Kimarekani Inaendelea Kushuka?

cri
    Kuanzia mwaka 2001, Marekani iliingika katika kipindi kipya cha kudidimia kwa uchumi, katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Bush kiwango cha thamani ya dola ya Kimarekani kwa Euro kimeshuka chini kwa 49%.

    Lakini kwa nini thamani ya dola za Kimarekani inaedelea kushuka? Jibu ni kupasuka kwa mapovu ya dola za Kimarekani yaliyotokea mwishoni mwa karne iliyopita; sera ya serikali ya Bush kwa dola za Kimarekani; nakisi kubwa katika biashara na bajeti na sera za Bush katika mambo ya nchi za nje.

    Kwanza, chanzo cha kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani kinatokana na hali ya mapovu ya uchumi katika miaka ya 90, kisha mapovu hayo yalivunjika moja baada ya jingine katika soko la hisa na biashara ya majumba. Hali ambayo Marekani ilijivujnia uimarishaji wa dola za Kimarekani imekuwa mbaya kila kukicha.

    Pili, Baada ya Bushi kushika madaraka, serikali ya Marekani ilitekeleza sera ya kudhoofisha thamani ya dola ya Kimarekani. Serikali ya Marekani iliwahi kutaka kugeuza hali hiyo ambayo thamani ya dola za Kimarekani inaendelea kushuka, lakini waziri wa fedha wa Marekani John Snow alisema, kitu cha kuamua kima cha mabadilishano ya fedha za kigeni ni soko, na serikali haifai kutia mkono katika soko hilo. Kutokana na kauli hiyo watu wanaamini kuwa serikali ya Bush inakubali kwa hiari hali hiyo.

    Tatu, thamani ya dola ya Kimarekani haiwezi kuimarika kutokana na hali ya nakisi kubwa ya bajeti ya Marekani. Kutokana na makadirio ya Wizara ya Fedha ya Marekani, nakisi ya bajeti nchini Marekani itazidi dola bilioni 500 mwaka 2004, nakisi kubwa hiyo inalazimisha mitaji ya nchini kukimbilia nchi nyingine. Kutokana na takwimu za Wizara ya Biashara ya Marekani, nakisi ya biashara ya Marekani itazidi dola za Kimarekani bilioni 489.4 mwaka huu. Hivi sasa nakisi hiyo kubwa katika bajeti na biashara imetikisa msingi wa kuimarisha thamani ya dola za Kimarekani.

    Zaidi ya hayo, uchumi wa nchi zinazotumia Euro unakua haraka, hii ni sababu nyingine ya wawekezaji kukimbilia katika nchi hizo na kutoweza kuimarisha thamani ya dola ya Kimarekani.

    Kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani kumeleta upepo mbaya katika uchumi wa dunia. Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Ulaya Bw. Trichet alisema kuwa hali ya kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani na kupanda kwa thamani ya Euro "haikaribishwi" na " katili". Chansela wa Ujerumani aliwahi kutahadharisha kuwa kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani kutailetea dunia hali mbaya ya kuhatarisha biashara ya Ulaya. Nchi nyingi za Asia pia zimeathirika na na hali hiyo ya kushuka kwa thamani ya dola za Kimarekani, kwa sababu wanatumia dola za Kimarekani wanazozipata kutoka biashara yao ya kimataifa kununua dhamana za serikali ya Marekani.

    Lakini kinyume na hali hiyo, kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani kutailetea Marekani faida kuliko hasara. Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya serikali ya Marekani kuiachia hali ya kushuka kwa thamani ya dola za Kimarekani bila kuishughulikia, moja ya sababu ni kwa ajili ya kuzuia wateja wa nchini kununua bidhaa zilizoagizwa kutoka nchi za nje ili kupunguza nakisi, sababu nyingine ni kuwa kudhoofisha thamani ya dola za Kimarekani kunaweza kuongeza nguvu ya ushindani wa bidhaa za Marekani katika soko la kimataifa. Jarida la Uingereza "Mwanauchumi" lilisema kuwa kutokana na kupunguza ushuru na kuanzisha vita, deni za Marekani kwa nchi za nje limefikia dola za Kimarekani trilioni 2.7. Nia ya serikali ya Marekani kuiachia hali hiyo ya kushuka kwa thamani ya dola za Kimarekani ni kwa ajili ya kupunguza baadhi ya madeni ya dola za Kimarekani kwa nchi za nje.

    Wachambuzi wanaona kuwa serikali ya Marekani kuiacha hali ya kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani kuendelea bila kuishughulikia ni kitendo cha serikali ya Marekani "kutowajibika ipaswavyo" na ni kitendo cha "kunyang'anya fedha". Wataalamu wanaona kuwa kutokana na hali ya wasiwasi wa uchumi mwaka huo, kuna uwezekano wa kutokea kwa msukosuko wa dola ya Kimarekani kote duniani, na msukosuko huo ukitokea kweli, utaathiri uchumi wa dunia unaoanza kufufuka na uchumi wa Marekani hali kadhalika.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-27