Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-27 16:44:01    
Bingwa wa Utafsiri Gong Jieshi

cri
Gong Jieshi mwenye umri wa miaka 41 ni bingwa wa kutafsiri, anajulikana katika nyanja ya ufasiri wa lugha za kigeni nchini China, na amewahi kushiriki kwenye kazi ya kutafsiri nyaraka nyingi muhimu kuhusu China kurudisha tena mamlaka yake kwa Hong Kong na Macau, na waraka kuhusu Beijing kugombea kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki mwaka 2008. Kadhalika pia amewahi kushiriki kwenye kazi ya kukagua na kupitisha tafsiri ya nyaraka 17 za serikali ya China.

    Bw. Gong Jieshi alizaliwa katika familia ya wakulima mkoani Henan, sehemu ya katikati ya China. Kutokana na kuwa na matokeo mazuri ya mtihani mwaka 1981 alijiunga na Chuo Kikuu cha Beijing kujifunza lugha ya Kifaransa. Alikuwa na furaha kubwa kupata nafasi ya kusoma katika chuo hicho ambacho kinapendwa sana na wanafunzi nchini China. Lakini mwanzoni baada ya kujiunga na chuo hicho aligundua kuwa elimu yake ilikuwa finyu ikilinganishwa na ya wanafunzi wenzake waliotoka mijini, na lafudhi yake ilikuwa ya kikwao. Alisema, "Nilitoka kijijini, wanafunzi wanaotoka vijijini huwa wanakuwa na elimu finyu kutokana na kusoma na kuona machache. Niliposikiliza wenzangu wakizungumza kuhusu riwaya maarufu "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" na kutoa maoni yao kuhusu namna ya kumtathmini mwenyekiti Mao, nilitambua kuwa niko nyuma, kwani sikuweza kujiunga nao katika mazungumzo bila kuwa na ujuzi wowote. Tokea hapo nilijitahidi kusoma ili niwe karibu nao kielimu."

    Ingawa tofauti hiyo ya kielimu ilikuwa ya muda mfupi, lakini ilimwingilia sana akilini, alitumia muda mwingi kusoma. Mwaka 1985 Bw. Gong Jieshi kwa mafanikio alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Beijing na kuanza kufanya kazi ya utafsiri katika Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni, Beijing. Baadaye alitumwa kwenye Chuo Kikuu cha Aix-Marseille I cha Ufaransa kusoma, katika muda wa mwaka mmoja tu alijipatia shahada ya pili ya isimu.

    Katika miaka 20 iliyopita, Bw. Gong Jieshi alitafsiri maandishi mengi ya viongozi wakuu wa China na nyaraka nyingi za serikali ya China, kutayarisha vitabu vya kufundishia Kifaransa na kanda za redio kwa ajili ya wanafunzi wa Kifaransa nchini China. Hivi sasa amemaliza kutafsiri vitabu zaidi ya 30 kutoka Kichina kuwa Kifaransa au kutoka Kifaransa kuwa Kichina. Alitumia miaka minane kumaliza "Kamusi ya Kifaransa-Kichina na Kichina-Kifaransa" ambayo inakubalika kuwa ni kamusi inayoaminika zaidi. Bw. Gong Jieshi alisema, "Kazi ya kutafsiri ni ngumu, kwanza lazima uelewe maana ya yote yanayozungumzwa na kuyatafsiri kikamilifu, wala sio kutafsiri neno kwa neno, kwani tafsiri ya neno kwa neno haieleweki kwa wasomaji. Wakati wote tunakabiliana na matatizo ya tofauti ya utamaduni katika tafsiri yetu. Kwa mfano, neno fulani la Kichina likitafsiriwa moja kwa moja kwa neno la Kifaransa, pengine litawababaisha Wafaransa, watakuwa hawapati maana hasa kutokana na tofauti ya utamaduni, hivyo inakupasa utumie neno jingine bila kupotosha maana."

    Bw. Gong Jieshi alisema, umuhimu wa tafsiri ni kama hewa kwa binadamu, Popote penye binadamu hapakosi kazi ya utafsiri. Utamaduni kati ya China na nchi nyingine unatofautiana sana, ni kazi ya maana sana kuzifanya tamaduni tofauti ziwasiliane, kuzidisha maelewano na urafiki kati ya mataifa. Kutokana na maana hiyo alijifunza mwenyewe Kiingereza, Kilatina na Kikorea.

    Bw. Gong Jieshi ni mkurugenzi wa Ofisi ya Kifaransa katika Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni, na vitabu vyote vilivyotafsiriwa katika ofisi hiyo anawajibika kuvishughulikia. Bw. Gong pia ni katibu mkuu wa kitengo cha Ufaransa katika Kamati ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Shirikisho la Wafasiri la China, na pia ni mwanakamati wa Kamati ya Kupima Mitihani ya Lugha ya Kifaransa ya wafasiri wa Kifaransa wanaotahiniwa kwa ajili ya kupata shahada ya kutafsiri nchini China. Kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa Utamaduni wa China na Ufaransa, Bw. Gong anaona kuwa hana muda kutokana na kuwa na shughuli nyingi. Alisema, "Tumetayarisha vitabu vingi kwa ajili ya mwaka huu wa utamaduni, kama vile seti moja ya vitabu "Kukutana Paris", seti nyingine ni "Mandhari na Utamaduni Nchini China", na vitabu vya "Fasihi ya China" vikiwemo maandishi ya waandishi wakubwa Ba Jin, Wang Meng na Shen Congwen, jumla vitabu vya aina kumi kadhaa."

    Bw. Gong Jieshi alisema, mwaka wa utamaduni kwa China na Ufaransa ni wa maana sana. China na Ufaransa zote ni nchi zenye utamaduni mkubwa, lakini maelewano baina ya wananchi wa nchi hizo mbili hayatoshi. Kwa kufanya shughuli za utamaduni kwa mwaka, maelewano na ushirkiano utaimarishwa.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-27