Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-28 11:04:46    
Barua za wasikilizaji 1228

cri
Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Emirates ametuletea barua akisema kuwa, akiwa kama mmoja wa wasikilizaji wa Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, angependa kutoa shukrani zangu za dhati kwetu, kutokana na ushirikiano mzuri kati yake, wasikilizaji na radio China Kimataifa katika kipindi chote cha mwaka 2004.

Anasema kwa kweli kulikuwa na matukio mengi ya kusisimua katika mwaka wa 2004. Matukio hayo yaliwafanya wasikilizaji wetu wawe karibu zaidi na Radio China Kimataifa, kwa kushiriki moja kwa moja kutoa maoni yao juu ya matukio hayo muhimu ya kihistoria, pamoja na kujifunza mengi kuhusu matukio hayo.

Anasema Maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Maadhimisho ya kutimiza miaka 100 tangu kuzaliwa muasisi wa China ya leo marehemu mzee Deng Xiaoping, maadhimisho ya miaka 55 tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China pamoja na ushindi mkubwa wa wanamichezo wa China katika mashindano ya michezo ya Olimpiki iliofanyika mjini Athens Ugiriki, kwa kweli yote hayo ni matukio yaliyomsisimua sana katika mwaka 2004 na kumshawishi aendelee kuwa karibu na Radio China Kimataifa. Kwani kutokana na kutayarisha vipindi na makala mbalimbali, lilikuwa ni jambo lenye maana sana kwake na kujihisi kwamba Radio China Kimataifa imempatia "kibarua" anachopenda kukifanya.

Bwana Mbarouk anasema shukrani zake ni kwa wahusika na watayarishaji wote wa vipindi na makala zilizohusika na matukio hayo kwa mwaka 2004, na ni matarajio yake makubwa kwamba mwaka wa 2005, Radio China Kimataifa itaendelea kuwapatia "utamu" wa vipindi na makala zitakazohusu mambo muhimu kabisa ya kihistoria, yatakayoweza kukuza urafiki na maelewano baina yetu pamoja na kujenga nguzo imara ya mapenzi baina ya Radio China Kimataifa na mamilioni ya wasikilizaji wake kote duniani.

Bwama Mbarouk anasema katika barua yake nyingine kuwa, licha ya kwamba takwimu zimeonesha uchumi wa Jamhuri ya Watu wa China umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa kwa asilimia zaidi ya tisa kila mwaka katika kipindi cha miaka 25, tangu pale marehemu Mzee Deng Xiaoping alipoasisi sera za kufufua uchumi nchini China mwaka 1978, ulimwengu una kila sababu ya kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Jamhuri ya Watu wa China katika kuinua hali ya uchumi kote duniani.

Leo hii bidhaa mbalimbali za kiufundi, kielektroniki, nguo, vitu vya matumizi ya nyumbani, vyombo vya usafiri na kadhaa wa kadhaa, zimekuwa zikitengenezwa nchini China kwa ufundi wa Hali ya juu na kuuzwa kwa bei muafaka katika kila pembe ya dunia, jambo ambalo yeye anaona kuwa sio tu limesaidia sana kuwanufaisha mamilioni ya watu duniani, lakini pia limechangia sana kuinua sekta ya kiuchumi kwa mataifa mengi duniani hususan mataifa yanayoendelea.

Bwana Mbarouk anasema yeye binafsi ni mfanyakazi wa kampuni moja ya kuuza vitu vya kompyuta mjini Dubai na amekuwa akishuhudia jinsi gani bidhaa kutoka Jamhuri ya Watu wa China zinavyofurika katika masoko ya Kompyuta mjini Dubai na kuchukua nafasi ya kwanza kibiashara, ambapo wanunuzi kutoka nchi mbalimbali za mashariki ya kati, Afrika na Ulaya mashariki wamekuwa wakifika nchini Falme za kiarabu kununua bidhaa hizo.

Kwa mantiki hiyo, China inaweza kuhesabiwa kama ni mchangiaji mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi duniani, hivyo kukua kwa sekta hiyo ni kukua kwa uchumi wa dunia nzima. Anasema hongera kwa juhudi, maarifa na nguvu za mamilioni ya wananchi wa China ambao usiku na mchana wamekuwa wakichapa kazi ili kukuza maendeleo ya kiuchumi chini ya sera za Hekima za marehemu Mzee Deng Xiaoping kwa zaidi ya miaka 25 sasa.

Anasema , pia angependa kuishukuru Radio China Kimataifa kwa mchango wake mkubwa wa kuwaelezea wasikilizaji wake kote duniani juu ya mafanikio ya kiuchumi ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia vipindi vyake mbalimbali, pamoja na kuwatumia makala, majarida na vitabu ambavyo vinaelezea jinsi gani ustawi wa kiuchumi wa China unavyopasua mawimbi kila kukicha. Anatumai kuwa Radio China Kimataifa itaendelea kuwafahamisha wasikilizaji wake mengi juu ya ufanisi wa kiuchumi nchini China.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyo Mbarouk Msabah kwa barua alizotuletea mara kwa mara na hisia za dhati na urafiki kwa nchi ya China na watu wake pamoja na uungaji mkono wake kwa sisi watangazaji na watayarishaji wa vipindi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Kila tunaposoma barua yake hutiwa moyo na kufurahia sana, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu waliopo popote pale duniani wataendelea kutuandikia barua, kutoa maoni na mapendekezo na kutusaidia katika kazi zetu mbalimbali. Tumedhamiria kufanya kazi vizuri zaidi katika mwaka 2005 ili kuwahudumia vizuri zaidi wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-28